Utajiri ni matokeo ya uwekezaji, hili nimekuwa nakuambia mara nyingi rafiki yangu. Nimekuwa nasema utajiri ni pale fedha inapokufanyia wewe kazi, na umasikini ni pale wewe unapoifanyia kazi fedha. Kwa maana hii kama kipato chako chote kinategemea mshahara au faida kwenye biashara moja tu, basi bado hujawa tajiri, haijalishi kipato hicho ni kikubwa kiasi gani. Kwa sababu hatari ya kipato kimoja ni kwamba kikikauka basi unakuwa huna kipato cha kuendesha maisha.

 

Hivyo utajiri unatokana na uwekezaji, pale ambapo fedha yako inafanya kazi hata kama wewe umelala.

Lakini pia uwekezaji upo wa aina nyingi, na kila aina ina hatari zake, kila aina nina faida na hasara zake na kila aina ina changamoto zake.

Unaweza kuwekeza kwenye masoko ya mitaji, kama hisa, vipande na hatifungani. Uzuri wa uwekezaji huu ni fedha inakuwa kwenye mzunguko na hivyo unaweza kuipata kwa urahisi, fedha yako inatumika kuzalisha na baadaye unalipwa faida kwa riba au gawio. Lakini uwekezaji huu una hatari na hasara pia uchumi ukiyumba na uwekezaji wako unayumba, taasisi uliyowekeza ikifanya vibaya unaweza kupoteza uwekezaji wako wote.

SOMA; Guide To Investing(Muongozo Wa Uwekezaji).

Unaweza kuwekeza pia kwenye mali na majengo. Hapa unakuwa na mashamba, viwanja na majengo ambayo unapangisha na/au kuuza. Huu ni uwekezaji wa uhakika ambao huwezi kupoteza fedha yako moja kwa moja. Kadiri siku zinavyokwenda thamani inaongezeka na unaweza kuutumia kupata mitaji zaidi kwa njia ya mikopo. Changamoto zake ni uhitaji wa mtaji mkubwa kuanzia, uhitaji wa muda mrefu mpaka uwekezaji huo uweze kulipa na pia uchumi ukiyumba bei zinaweza kupungua na kutokufikia matarajio ya uwekezaji.

Hivyo ndivyo hali ilivyo rafiki, kwenye kila uwekezaji una manufaa yake, na pia una hatari zake. 

Lakini upo uwekezaji mmoja ambao una manufaa yote, lakini hauna hatari hata moja, hauna hasara hata moja. Yaani wewe unawekeza na kuvuna matunda tu, hakuna cha kukubabaisha.

Swali langu kwako ni je ungependa kujua uwekezaji huu? Ungependa kujua namna unavyoweza kuanza kuutumia ili uweze kunufaika zaidi? Kama unapenda mambo mazuri kwenye maisha yako, kama unataka maisha bora, kama unataka utajiri, na kama unataka mafanikio, basi jibu lako litakuwa ni ndiyo, nataka kujua huo uwekezaji.

Kabla sijakuambia uwekezaji huu kwanza nikupe sifa zake zaidi; haujitaji mtaji au gharama kubwa kuanza kuufanya, unaweza kuuanza hata kwa bure kabisa. Ni uwekezaji ambao hauozi au kupitwa na wakati. Na kikubwa zaidi, ambacho kinanifanya mimi naupenda sana uwekezaji huu ni hichi; hata uchumi uyumbe namna gani, uwekezaji huu haukupi hasara.

Kama ambavyo umekuwa unasikia watu wakisema nyakati fulani ni ngumu, fedha hakuna, uchumi unadorora, na mengine kama hayo, yana ukweli kabisa kwa sababu viashiria vyote vinakuwa vinaonesha hilo, lakini ukiwa na uwekezaji utakaokwenda kujifunza hapa leo, hutaathiriwa na chochote. Kila wakati, uwe mzuri au mbaya, wewe utakuwa unatengeneza faida tu.

Uwekezaji ninaozungumzia hapa, ambao ni muhimu sana na umekuwa unaninufaisha sana mimi binafsi ni uwekezaji ndani yako binafsi, uwekezaji kwenye maarifa sahihi kwa kile ambacho unafanya na kwenye yale maeneo muhimu kabisa kwenye maisha yako.

Uwekezaji kwako binafsi, kwa kuhakikisha unakuwa na maarifa sahihi ya kukuwezesha kuchukua hatua kwenye maisha yako, ni uwekezaji muhimu sana kwako na utakaokulipa wewe mara dufu. Huu ndiyo utakaokuletea utajiri na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

SOMA; Sehemu Mbili (02) Muhimu Zilizosahaulika Katika Uwekezaji.

Ukiangalia kwa nje, hakuna tofauti kubwa ya tajiri na masikini, wote ni watu ambao wanafanya shughuli zao kwa juhudi, na wakati mwingine masikini wanaweka juhudi zaidi. Utawakuta wote wanafanya kazi ya aina moja, au biashara ya aina moja, au walianzia wote chini kabisa. Lakini mmoja anakuwa tajiri sana na mwingine anaishia kwenye umasikini.

Tofauti huwezi kuuona kwa nje kwa sababu uwekezaji huu muhimu sana niliokuambia hapa huwezi kuuona kwa nje. Uwekezaji huu upo ndani ya akili ya mtu. Hivyo kinachowatofautisha masikini na matajiri ni maarifa waliyonayo. Popote unapoona watu wawili wanafanya jambo linalofanana, ila mmoja amefanikiwa na mwingine hajafanikiwa, jua kwamba yule aliyefanikiwa kuna vitu anavijua ambavyo aliyefanikiwa havijui.

Nimekuwa nikisema pia ya kwamba kinachokuzuia kufika pale unapotaka kufika, ni kile usichokijua. Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kufika kule unakotaka kufika, ni kujua kila unachopaswa kujua ili uweze kufika huko.

Unapataje uwekezaji huu muhimu kwenye maisha yako?

Kwa kujifunza, na hatua ya kwanza kabisa kujifunza ni KUSOMA VITABU. Nimeandika kusoma vitabu kwa herufi kubwa kwa sababu hicho ni kitu muhimu kuliko vyote. Watu wamekuwa wanakwepa kusoma vitabu kwa kuamini wakishasoma makala inawatosha. 

Wanakosea sana. Unahitaji kusoma vitabu. Na kwa kuanza, kama ambavyo nimewahi kukuambia siku za nyuma, SOMA VITABU VITANO kwenye kila eneo unalotaka kuwa bora na kufanikiwa.

Kama unataka kufanikiwa kwenye biashara, soma vitabu vitano vya biashara, vitabu ambavyo ni bora kabisa. Kama unataka kufanikiwa kwenye uwekezaji, soma vitabu vitano vya uwekezaji. 

Kadhalika kwenye taaluma nyingine na hata maisha kwa ujumla.

Sasa ninaposema vitabu vitano simaanishi usome vitabu vitano halafu ndiyo umehitimu na huhitaji tena vitabu vingine. Hivi vitabu vitano ni vya kuanzia tu, yaani ndiyo unafungua ufahamu wako juu ya kile unachotaka. Kujifunza ni zoezi endelevu, zoezi la kila siku na hakuna kuhitimu kama ilivyo kwenye mfumo wa elimu.

Kupata vitabu vya kujisomea ili kupata maarifa sahihi bonyeza maandishi haya.

Baada ya kusoma vitabu sasa, unaweza kusoma makala zinazohusiana na kile unachotaka. 

Makala hizo ziwe zinakupa mbinu na maarifa bora yanayokuwezesha kufanya maamuzi bora. 

Makala hizi unaweza kuzipata kwenye mitandao ya AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA.

Unaweza pia kujifunza kupitia kusikiliza vipindi vizuri vya kufundisha, kuangalia vipindi vizuri na hata kusikiliza vitabu vilivyosomwa (AUDIO BOOKS). Kama unapenda kupata vitabu vilivyosomwa, bonyeza maandishi haya.

Wito wangu kwako rafiki ni huu, kila siku jifunze, kila siku ongeza maarifa, haya yatakuwezesha kufanya maamuzi sahihi na kuziona fursa nyingi ambazo wengine hawazioni. Maarifa ndiyo uwekezaji pekee ambao hauwezi kukutupa hata mambo yawe magumu kiasi gani. Na pia huhitaji kuwa na fedha nyingi ili kuanza kuwekeza kwenye maarifa, vitabu na makala zinakutosha kuanzia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.