Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hii ni siku nyingine nzuri sana kwetu, ambapo tumepata nafasi nzuri ya kwenda kuweka juhudi kwenye kile tukichochagua kufanya, ili kuweza kupata matokeo bora na kufanikiwa sana.

Leo ndiyo leo, na hakikisha kuna tofauti unaiweka siku hii ya leo.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MATARAJIO NA UHALISIA…
Watu huwa wana matarajio kwenye jambo lolote wanalokwenda kufanya au wanalokwenda kupata.
Mara nyingi sana matarajio haya huwa makubwa sana, na wengi huweja juhudi na kusubiri kwa shauku kubwa wapate wanachotaka au kufika wanakotaka kufika.
Lakini uhalisia unapofikiwa, ndipo wengi huvurugwa hasa, pale uhalisia unapokuwa tofauti na matarajio.
Hasa pale matarajio yanapokuwa makubwa kuliko uhalisia, watu hukata tamaa na kuona haikuwa na maana kusubiri sana kitu hicho.
Lakini haya yote yanaanzia kwenye akili zetu,
Kwa sababu vitu vinatokea kaka ambavyo vinatokea, na siyo kutokea kama tunavyotaka sisi wenyewe.
Hivyo, ili kuondoa hali hii ya kuumizwa na uhalisia, hasa baada ya kuwa na matarajio makubwa, jua ni mambo gani unaweza kuyadhibiti na yapi huwezi.
Yale unayoweza kuyadhibiti, unaweza kuweka matarajio makubwa utakavyo na kisha kuweka juhudi kuhakikisha unafikia matarajio hayo.
Lakini yale mambo ambayo huwezi kuyadhibiti, usiweka matarajio makubwa, kwa sababu hakuna chochote unachoweza kubadili. Hivyo kuwa tayari kupokea chochote kinachotokea na angalia unawezaje kukitumia kufika kule unakotaka kufika.
Usitumie akili na mawazo yako mwenyewe kujiumiza kwa mambo ambayo hakuna tofauti unayoweza kuleta. Bali tumia kila unachopata kama njia ya kufika kule unakotaka kufika.
Uwe na siku njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.