Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, ambapo tumepata nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.

img-20161217-wa0002
Tutumie nafasi hii ya leo vizuri kwa kuwa na NIDHAMU, UADILIFU na pia KUJITUMA ili tuweze kupata kile tunachotaka.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu; KABLA HUJASEMA HAIWEZEKANI….
Ni kawaida kwetu pale tunapojaribu au kufanya jambo na likashindikana, kuona kwamba haiwezekani. Tunaweza kujiambia tumefanya sana, tumejitahidi sana lakini haiwezekani. Tunaacha jambo hilo na kuendelea na mengine.

KABLA HUJASEMA HAIWEZEKANI, kwanza hebu chukua muda wako na uangalie je hakuma ambaye ameshaweza kufanya kama hicho unachotaka kufanya?
Angalia kwa unaowajua na hata usiowajua, angalia kwa walio hai hata waliokufa, angalia kwenye historia, na ujihakikishie kama wapo au hawapo ambao wameshafanya.

Kama wapo ambao wameshafanya, hata kama ni wa nchi au bara jingine, basi uhakika ni kwamba inawezekana. Na unachohitaji wewe ni kujua wao walifanyaje mpaka wakapata kile walichopata, kisha na wewe ufanye ili upate.

Kama hakuna yeyote ambaye alishafanya, basi hapo ndipo penye fursa kubwa zaidi. Kwa sababu ukiweza kufanya, utafungua njia kwa wengine wengi, na utaacha alama kubwa hapa duniani.

Hivyo kwa vyovyote vile, fanya.
Usijubaliane na akili yako inapokwambia haiwezekani, ni njia ya kuogopa kupambana na hivyo kutafuta sababu ya kuachana na mapambano.
Kumbuka, hakuna chochote kizuri na cha thamani ambacho ni rahisi.

Uwe na siku ya kipekee leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.