Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa sana.

Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu ULEVI WA MAFANIKIO….
Mafanikio kidogo mara nyingi huwa ni sumu ya mafanikio makubwa.
Yaani watu wanapopata mafanikio kidogo, yanawazuia kuweza kufanikiwa zaidi.
Wanajiona tayari wanajua kila kitu, na hivyo hawahitaji kujifunza tena.
Wanajiona tayari wameshategua kitendawili hivyo hawahitaji kuweka juhudi kubwa tena.
Wanajiona wameshajua njia ya uhakika hivyo hawawezi kushindwa tena.
Huu ni ulevi wa mafanikio, ambao umekuwa unawafanya watu kuchukua maamuzi ya hovyo na hatimaye kuanguka au kushindwa kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Usikubali kabisa mafanikio yakulevye, yakufanye ushindwe kuona uhalisia, ya kwamba;
Hata kama umefanikiwa kiasi gani, kujifunza ni lazima.
Hata kama umefika juu kiasi gani, bado unahitaji kuweka juhudi kubwa.
Na kadiri unavyokwenda juu zaidi, ndivyo hatari ya kuanguka inakuwa kubwa zaidi.
Mafanikio kidogo kwako yasiwe sumu ya kukuzuia kupata mafanikio makubwa.
Bali yawe kichocheo cha mafanikio makubwa zaidi.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.