Habari za asubuhi ya leo rafiki,
Ni siku nyingine nzuri sana ya leo, ambapo tumepata nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya.

IMG_20170102_073855
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA tunaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NANI AMEKULAZIMISHA?
Moja ya zawadi ya kipekee sana tuliyopewa hapa duniani, ni kuchagua. Vitu vingi sana ambavyo tunavyo na tunafanya hapa duniani, tumechagua sisi wenyewe. Japo wengi utawakuta wakilalamika, kama vile wamelazimishwa kufanya.

Kama unalalamikia tabia ulizonazo ambazo zinakuzuia kufanikiwa kama uvivu, ulevi, kukosa umakini, mimi nitakuuliza nani amekulazimisha uwe na tabia hizo? Ni wewe mwenyewe umechagua kuwa nazo na unaendelea kuzilea.

Kama unalalamikia kazi yako haikupi kipato cha kutosheleza, haikuridhishi na huipendi, swali langu kwako, nani amekulazimisha kuifanya? Siyo wewe mwenyewe uliyeenda kuiomba? Siyo wewe mwenyewe ambaye umekuwa unaifanya kwa mazoea?

Ukiniambia biashara unayoifanya haikulipi, kwamba hakuna unachopata, ni ngumu na ushindani ni mkali, tafadhali nioneshe kwanza aliyekushikia bastola kwenye kichwa chako na kukuambia usipofanya biashara fulani nakuua. Nina hakika hayupo, wewe mwenyewe ulikaa chini na kuamua kuifanya, labda kwa kuona wengine wakifanya au kwa kuamua kujaribu.

Kwa vyovyote vile, wewe mwenyewe ulichagua kufanya hicho unacholalamikia sasa. Hata umasikini nao, unaweza kuwa hukuchagua kuzaliwa nao, lakini umechagua kuendelea kuishi nao.

Hivyo rafiki, usitulalamikie na vitu ulivyochagua wewe mwenyewe, badala yake chukua hatua kubadili. Kwa kuwa bado unayo nguvu ya kuchagua, chagua sasa, kwa ubora zaidi.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.