Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

IMG_20170102_073855
Leo hii tunakwenda kuweka NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ili tuweze kufikia ndoto za maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NEGATIVE NEWS….
Wanasema, mbwa akimng’ata mtu ni habari, ila mtu akimng’ata mbwa ni habari ya kusisimua.
Sasa watu wa habari wanachopenda ni habari za kusisimua, kwa sababu habari za kawaida watu wamezizoea.
Hivyo juhudi zao kubwa, ni kupata habari za kusisimua na kuziweka mbele kabisa ili watu waendelee kuwafuatilia.

Ukifuatilia habari tu unaweza kuhisi kama dunia inaelekea mwisho, kila kitu kinaonekana ni hatari.
Habari zenye hofu zinauza na kufuatiliwa na wengi kwa sababu wanadamu wana hofu nyingi.
Hivyo basi rafiki, unahitaji kujiondoa kwenye huu mnyororo wa habari hasi na habari zenye hofu.

Iwe ni mbwa kang’ata mtu au mtu kang’ata mbwa, kama wewe huhusiki siyo habari kwako. Weka vipaumbele vyako kwenye ndoto zako kwanza, na siyo kwenye habari kwanza.
Na kosa kubwa unaweza kufanya, ni kusona kurasa za mbele za magazeti na kuondoka ukiamini una habari, au kama wengi wanavyojidanganya kwa kiingereza, NIPO INFORMED.
Ni mara chache sana utakuwa informed kwa habari, hasa zile za kuripoti matukio mbalimbali.
Anza siku yako kwa kujiripotia matukio yako mwenyewe, na siyo kuanza na habari.
Pia maliza siku yako kwa kujiripotia yale yaliyotokea kwenye siku yako na siyo kusubiri uripotiwe habari.
Kama ipo habari muhimu kwako, itakutafuta wewe, na siyo wewe upoteze muda kuitafuta.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.