Habari za leo rafiki yangu,

Ni matumaini yangu kwamba uko vizuri na unaendelea kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa. Lakini licha ya juhudi unazoweka, yapo mambo ambayo huenda unayafanya, na bila kujua yamekuwa yanakurudisha nyuma, yamekuwa yanaharibu juhudi zozote unazoweka na hivyo kushindwa kufikia mafanikio ambayo unakazana kuyafikia kila siku.

 

Kwa mfano kama lipo dumu la maji unachota bombani, na dumu hilo chini limetoboka, sehemu kubwa tu ambao inavujisha maji mengi. Je unafikiri dumu hilo linaweza kujaa maji? 

Haiwezekani, kwa sababu kadiri maji yanavyoingia, ndivyo yanavyotoka. Hivyo kuendelea kusubiri dumu lijae bila ya kuziba pale linapovuja, ni kuendelea kupoteza maji zaidi.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio, unaweza kuweka juhudi sana, lakini kuna mambo yanapoteza zile juhudi zako. Unaweza kuonekana unajituma sana, lakini hakuna hatua yoyote unayopiga. Hii ni kwa sababu kuna mambo unakuwa umechagua kufanya, ambayo yanarudisha juhudi zako nyuma.

Leo tutakwenda kujifunza mambo haya matano, yajue namna yanavyokurudisha nyuma na chukua hatua ya kuondokana nayo.

1. Kulalamikia yeyote unayefikiri anakukwamisha.

Tabia yetu binadamu ni hii, iwapo kuna kitu tunataka, lakini hatukipati, basi tunajiaminisha kwamba, yupo ambaye amesababisha tusipate. Hivyo jukumu letu la kwanza ni kuhakikisha tunamjua mtu huyo na kumtupia lawama zetu zote.

Wa kwanza kabisa kulaumiwa ni serikali, jambo lolote ambalo serikali inafanya, lina namna ya kulaumiwa na watu kama sehemu ya kukwama kwao. Labda ni kodi au sera mbovu, watu huona namna ambavyo hayo yanawakwamisha.

Kundi jingine linaloongoza kwa kulaumiwa ni waajiri, watu wengi wanaomba kazi wao wenyewe, na kuwa na moyo sana wanapotaka kazi, ila wakishaanza kazi, ndipo vimbwanga vinaanza. Mwajiri atapewa kila aina ya lawama. Ni kama watu wanakabidhi maisha yao kwa waajiri wao, hivyo yasipokuwa bora, wa kulaumiwa ni mwajiri.

Wazazi nao pia wamekuwa wanalaumiwa, utamsikia mtu mzima kabisa anasema kama wazazi wangu wasingefanya kitu fulani, au wangefanya kitu fulani, leo nisingekuwa hapa.

Nikukumbushe tu rafiki, kama kwa namna yoyote ile, unaona wengine ndiyo wanaohusika na wewe kutofanikiwa, tayari umeshaaga mashindano, yaani umeshatoka kwenye mstari wa mafanikio. Kwa sababu utaridhika na sababu hizo na hutachukua hatua.

Nakubaliana na wewe kwamba serikali ina makosa yake, waajiri wana matatizo yao na hata wazazi kuna mambo walifanya au hawakufanya, ambayo yamekuwa na mchango kwa hapo ulipo sasa. Lakini swali langu ni KWA HIYO? Ndiyo serikali, mwajiri, wazazi wamekufikisha hapo ulipo, KWA HIYO? Kwa hiyo unataka kubaki hapo ulipo sasa au unataka kuchukua hatua?

Kama unataka kubaki hapo ulipo, endelea kuwalaumu, kama unataka kuchukua hatua, acha kuwalaumu na angalia kipi unachoweza kufanya.

SOMA; Mambo Kumi(10) Muhimu Usiyojua Kuhusu Mafanikio, Na Jinsi Yanavyokurudisha Nyuma.

2. Kutopenda kujifunza.

Watu wengi wamekuwa wanafanya kile wanachofanya leo, kwa sababu jana walifanya na juzi walifanya, na kesho wataendelea tena kufanya. Wanafanya yale yale kwa njia ile ile kila siku, halafu watashangaa kwa nini hawapigi hatua. Sikiliza rafiki, kwenye hii dunia kila kitu kinabadilika, na zama hizi, mambo yanabadilika kwa kasi ya ajabu mno. Chochote unachofanya leo, kwa uhakika kabisa, miaka 10 ijayo kinaweza kisiwepo kabisa. Na miaka miwili ijayo, kuendelea kukifanya kama unavyofanya sasa, utakuwa unapotea tu muda wako.

Unahitaji kupenda kujifunza kila siku na kila wakati. Kitu chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha una maarifa na taarifa za kutosha kuhusu mabadiliko yanayotokea. Jifunze njia bora zaidi za kufanya kile unachofanya. Jaribu njia mpya, kila siku boresha kitu ili uweze kupata matokeo ya tofauti.

Kufanya kitu chochote kwa mazoea, hata kama unafanya usiku na mchana, unapoteza muda wako kwa sababu wakati utakuacha tu.

3. Kufuatilia mambo ya wengine.

Wazungu wana usemi maarufu ambao ni MIND YOUR OWN BUSINESS, kwa kiswahili tunaweza kusema jali mambo yako. Lakini huku kwetu tunaweza kubadili msemo huo kwa namna tunavyofanya mambo yetu, watu wanajali sana mambo ya wengine kuliko yao. Watu wanafuatilia sana maisha ya wengine kuliko wanavyofuatilia maisha yao. Majungu na umbea umbea ni kama sehemu ya kawaida kabisa ya maisha ya kila siku ya walio wengi.

Watu wanajua kwa hakika nani anakosea kwa kile anachofanya, ila hawajui wao wanakosea wapi. Na ujio wa hii mitandao ya kijamii, ndiyo umewasha moto zaidi kwenye hili la kufuatilia maisha ya wengine. Watu wapo tayari kuwafuatilia wengine kwa kila wanachofanya, lakini hawana muda wa kufanya mambo yao wenyewe.

Watu wanajua msanii fulani ana pesa kiasi gani, lakini wao wenyewe hawajui kipato chao kwa hakika ni kiasi gani na wanawezaje kukikuza. Watu wanajua kocha wa mpira wa miguu amekosea wapi kupanga kikosi chake mpaka akafungwa, ila hawajui wao wanakosea wapi mpaka hawafanikiwi.

Nikuambie tu rafiki yangu, kama unajua wasanii maarufu wanalipwaje na maisha yao yakoje, ila hujui maisha yako yanaelekea wapi, kama unajua kocha aliyefungwa alikosea wapi kupanga kikosi chake, lakini wewe hujui unakosea wapi mpaka hufanikiwi, bado hujawa makini na maisha yako, na hujajitoa kwa ajili ya maisha ya mafanikio.

4. Kufuatilia mambo kwa ushabiki.

Hili ni janga kubwa zaidi, kila siku ni kama kumekuwa na jambo jipya la kishabiki linaendelea. Iwe ni kauli au mambo wanayofanya viongozi, au habari mbalimbali, unakuwa ni ushabiki unaovuma kwa kasi, lakini haudumu, baada ya siku chache unakuja ushabiki mwingine, watu wanaacha ule wa mwanzo na kudandia ushabiki huo mpya.

Kama na wewe umekuwa mtu wa kupelekwa pelekwa na mambo yanayoendelea, unajichelewesha kufanikiwa. Kwa sababu kila siku lipo jambo la kushangaza na kusisimua, na vyombo vya habari, pamoja na mitandao ya kijamii, inakutega sana wewe uingie kwenye ushabiki huo. Unaona ni muhimu sana na wewe uandike, kusambaza au kulaani kilichofanywa au kusemwa. Lakini wakati unajiona umefanya jambo la muhimu sana, linaibuka jingine kubwa na la kusisimua zaidi, unajikuta unahitajika tena kurudia zoezi lako la mwanzo.

Sasa inakuwa hivi kila siku, mpaka inafika wakati mtu unaamka na kujiuliza leo habari gani ya moto zaidi. Niseme tu kama na wewe upo kwenye mkumbo wa kufuata matukio, unajichelewesha kufanikiwa.

SOMA; Epuka Adui Huyu Mkubwa Wa Mafanikio Yako Anayekurudisha Nyuma.

5. Kutafuta njia ya mkato.

Wacha nikuambie kitu ambacho hupendi kukisikia, njia ya mafanikio ni ngumu na ndefu, inahitaji muda, uvumilivu na kujitoa. Na habari mbaya zaidi ambayo hutapenda kuisikia ni kwamba, hakuna mbadala. Lakini najua hutasikiliza hili, na kesho mtu atakuambia kuna hii biashara ambayo unakaa na kualika watu na mwisho wa mwezi utapata mamilioni, kwa kutafuta kwako mkato, unaingia kujaribu, unamaliza mwezi wako kwa kuhangaika na watu, lakini milioni huzipati. Baadaye wanakuambia mwezi ujao utakuwa bora zaidi, fanya hiki na kile na mwezi unaofuata unafanya tena, mwisho hamna kitu, mpaka akili yako ije kufunguka, umeshapoteza muda wa kutosha.

Wapo pia ambao wamekuwa wanaamini sana kwenye misaada na kuwezeshwa. Utamsikia kabisa kijana mwenye akili timamu na nguvu zake akisema nina mawazo mazuri lakini sijawezeshwa tu, au nikipata mfadhili nitafanya. Sasa huwa najiuliza jasho walipewa la nini?

Nisikilize rafiki, tena nisikilize vizuri kama bado unaendelea kusoma hapa, usitafute namna yoyote ya urahisi au mteremko kwenye kufanikiwa, usisubiri mtu yeyote aje kukunyanyua hapo ulipo, unahitaji kuweka juhudi zako wewe mwenyewe, juhudi kubwa sana, umwagike jasho la kutosha, iwe ni la mwili au akili. Ingekuwa rahisi kila mtu angeshafanya, na angeshafanikiwa. Ni ngumu na wasiokubali ugumu wanakazana kujaribu njia za mkato kila siku, okoa muda wako, jua kile unataka kufanya na weka juhudi kuanza kufanya. Usiendelee kusubiri.

Hayo ni matano ambayo nataka wewe rafiki yangu, uache kuyafanya mara moja, ili juhudi zozote unazoweka, zisipotelee chini. Zingatia sana haya, na mara zote jua unaenda wapi na unafikaje pale. Baada ya kujua hayo, weka juhudi, achana na kelele, achana na ushabiki na achana na kutafuta mkato. Mafanikio yapo ndani yako, kama utayaelewa na kuyafanyia kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.