Rafiki yangu mpendwa,

Kitu kimoja kikubwa sana ambacho nimejifunza kuhusu mafanikio ya watu ni kwamba kila mtu ana ndoto kubwa ambayo ipo ndani yake. Kila mtu katika kipindi fulani cha maisha yake, aliwahi kujiambia nikiwa mkubwa nitakuwa…..

Lakini mchakato wa maisha ukafunika kabisa ndoto kubwa ambazo wengi walikuwa nazo. Labda ni mtazamo wa familia na jamii kwa ujumla kuhusu ndoto ambayo mtu amekuwa nayo. Au ni kushindwa masomo shuleni na hivyo mtu kuambiwa hawezi kuendelea na kile anachotaka.

Pamoja na mchakato wa maisha kuwazuia wengi kushindwa kufikia ndoto kubwa za maisha yao, bado kuna maadui wengine ambao wamekuwa wanawazuia watu kufikia ndoto kubwa walizonazo kwenye maisha yao.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Wapo maadui wakubwa wawili wa ndoto kubwa ulizonazo kwenye maisha yako.

Adui wa kwanza na ambaye ana ushawishi mkubwa sana kwako ni wewe mwenyewe. Wewe mwenyewe ndiye adui namba moja unayejizuia kufikia ndoto zako kubwa. Mawazo uliyonayo na hatua unazochukua au kutokuchukua ndiyo zimekufikisha hapo ulipo sasa.

Ukiwa na wasiwasi wowote juu ya matokeo unayokwenda kupata, ukianza kujiambia huwezi au haiwezekani, hakuna muujiza wowote unaoweza kufanyika kwako ukakuwezesha wewe kupata kile unachotaka. Ukikata tamaa wewe mwenyewe hakuna juhudi zozote za nje zinazoweza kukufikisha kwenye mafanikio unayotaka.

SOMA; Mambo Matano(05) Unayopenda Sana Kufanya Ambayo Yanakuzuia Wewe Kufanikiwa Kwenye Maisha Yako.

Adui wa pili na ambaye ana ushawishi mkubwa ni wale watu ambao wanakuzunguka. Watu hawa wanaweza kuwa sumu kubwa sana kwako, ambayo itakuzuia kabisa kupiga hatua kwenye maisha yako.

Wale watu ambao wanakuzunguka, watu wako wa karibu ambao muda mwingi unakuwa nao, ni watu ambao wana ushawishi mkubwa sana kwako. Ni watu ambao kwa kujua au kutokujua wanakukatisha tamaa kwenye ndoto zako kubwa. Ni watu ambao hawawezi kukuruhusu wewe upige hatua kubwa kwenye maisha yao kuliko hatua ambazo wamepiga wao.

Na kama ambavyo imekuwa ikisemwa, matokeo unayopata kwenye maisha yako ni wastani wa matokeo wanayopata watu watano wa karibu sana kwako. Kwamba huwezi kufanikiwa sana kuwashinda wale ambao wamekuzunguka. Wale wanaokuzunguka ni maadui wakubwa kwenye ndoto zako kubwa, iwe unajua au hujui.

Hivyo rafiki yangu, kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha hatua muhimu sana kwako kuchukua ili uweze kufikia ndoto zako kubwa na uzuie wengine wasivuruge ndoto hizo.

Hatua ninayokwenda kukushirikisha inakabili adui wa pili wa ndoto zako ambao ni wale watu anaokuzunguka.

Rafiki yangu, sehemu kubwa ya watu waliokuzunguka, hawana mipango yoyote mikubwa na maisha yao. Ni watu ambao wapo wapo tu, wanasukuma siku ya leo iishe na kama kesho ikiwakuta basi nayo wataisukuma iishe. Hawana popote pakubwa wanakokwenda na maisha yao, na hivyo hawana msukumo mkubwa kwao.

Sasa unapokuwa na watu wa aina hii, wewe una ndoto kubwa wao hawana, kitakachotokea ni wewe utapoteza na kuachana kabisa na ndoto zako kubwa ili uweze kuendana nao. Kwa sababu hamtaweza kwenda pamoja wakati wewe una ndoto kubwa na wao hawana.

Kwa sababu ndoto zako kubwa zitakutana wewe ujitoe hasa, uzingatie sana muda wako, upunguze sehemu kubwa ya vitu ambavyo umezoea kufanya ili upate muda mwingi wa kufanyia kazi ndoto yako kubwa.

Lakini wale wanaokuzunguka, ambao hawana ndoto kubwa na wala hawajui gharama za kufikia ndoto kubwa, hawatakuacha kabisa uendelee na ndoto hizo. Hivyo watahakikisha kwa kila namna kwamba unaachana na ndoto hizo.

Wataanza kukuambia kwa nini haiwezekani au utashindwa, na watakupa mifano na takwimu ambazo hata hazipo, za watu walijaribu kama wewe na wakashindwa.

Wataanza kukufanya ujisikie vibaya, pale wanapotaka wewe uwe nao na wewe una mambo ya muhimu kufanya. Watakuambia unajitenga nao, watakuambia huna maisha, watakuambia umebadilika na maneno mengine mengi yatakayokufanya ujisikie vibaya na kurudi kwenye kundi lao.

Rafiki, hatua pekee kwako kuchukua, hatua muhimu kwa ajili ya kufikia ndoto kubwa ulizonazo, ni kuwachuja upya wale watu ambao utaruhusu wawe karibu na wewe, watumie hata muda wako mdogo. Hivyo kwenye watu wote, ndugu, jamaa na marafiki, fanya mchujo wa kujua nani anastahili muda wako na nani hastahili.

Mchujo wako uangalie ndoto kubwa ambazo watu hao wanazo na hatua kubwa ambazo wanazichukua. Kama mtu hana kabisa ndoto kubwa anayofanyia kazi, kama mtu hana kinachomsukuma kila siku kuwa bora, basi mtu huyo ni tatizo na mwondoe kwenye kundi la watu wanaostahili muda wako.

SOMA; Ambatana Kwa Umakini Na Rafiki Huyu Mmoja Na Kwa Uhakika Lazima Utafanikiwa (Mambo 10 Ya Kuzingatia Ili Kufanikiwa Kwenye Kazi).

Kama mtu ana ndoto kubwa anazofanyia kazi, kama mtu anakazana kila siku kuwa bora, huyu ni mtu unayepaswa kuendelea naye kwa sababu hata kama hakupi moyo, basi anakuwa hakurudishi nyuma.

Hii ni hatua muhimu sana kuchukua, na hatua ngumu kwa wengi kwa sababu sisi binadamu tuna udhaifu mmoja mkubwa, huwa tunapenda kuwafurahisha wengine, huwa hatupendi kufanya kitu kitakachowaumiza wengine hata kama ni kitu sahihi kwetu. Na ndiyo maana watu wamekuwa wanakaa kwenye urafiki, kwenye mahusiano na hata kwenye ndoa ambazo zinawarudisha nyuma.

Lazima uweze kupima ukubwa na umuhimu wa ndoto uliyonayo kwako na kwa wengine, na uweze kuona kila anayekuzuia kufikia ndoto yako ni aduia kwako na wengine pia, hata kama ni ndugu wa karibu au rafiki.

Huhitaji kutangaza vita kwenye hili, wala huhitaji kuwaambia watu sitaki tena mazoea na ninyi, unachopaswa kufanya ni kuwaweka watu kwenye makundi fulani ambayo wewe mwenyewe ndiye unayekuwa unajua makundi hayo.

Unaweza kuwa na kundi la wale ambao wanajua wapi wanakwenda, wanakazana kuwa bora na hawa ndiyo ukawapa kipaumbele kwenye maisha yako. Pia unakuwa na kundi la wale ambao hakuna popote wanapokwenda, wapo wapo tu wanaishi kwa kusukuma siku iende. Hapa unapaswa kuwa na mahusiano nao ya juu juu tu, wanaweza kuwa marafiki wazuri lakini hawapaswi kujua ndoto kubwa unazofanyia kazi wala kujua hatua kubwa unazopiga, maana wataanza kuleta matatizo.

Halafu kuna kundi la watu hasi kabisa, wale ambao hawaamini kama unaweza kufanya kitu chochote kikubwa, hawa wanaamini kwamba maisha ni magumu na yataendelea kuwa magumu kwa sababu ndivyo tulivyopangiwa kuwa. Watu hawa ni matatizo na kazana sana kuwaondoa kabisa kwenye maisha yako. hakuna kikubwa unachoweza kufanya kwa watu wa aina hii, na hakuna namna unaweza kuepuka sumu zao kama utawapa muda wako. Hawa ni wahubiri wa habari mbaya, kila kitu wanaona ubaya wake na ukikaa nao, hata kwa dakika chache tu unaanza kuchoka na kukata tamaa. Wafute kabisa watu wa aina hiyo kwenye maisha yako.

Rafiki, nimalize kwa kusema kwamba kuwaweka watu kwenye makundi kulingana na ndoto kubwa uliyonayo siyo ubaguzi, kama kwa vyovyote vile umesoma hapa na ukajiambia huu sasa ni ubaguzi, basi wewe upo kwenye kundi la tatu, ambapo wengi watahitaji kujitenga sana na wewe. Siyo ubaguzi bali ni kutengeneza kipaumbele kwenye maisha yako, kuna watu zaidi ya bilioni saba duniani, huwezi kuenda na kila mtu na huwezi kuwakosa wale ambao ni sahihi.

Fanya zoezi hili rafiki yangu, ambatana na wale ambao wanajua wapi wanaenda na maisha yao na wanaochukua hatua kila siku ili kuwa bora zaidi. Wale ambao wapo wapo, hawana makubwa wanayofanyia kazi na hawakukatishi tamaa, unaweza kuwapa muda kidogo. Lakini wale waliokata tamaa na wanaokatisha wengine tamaa, waondoe mara moja kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji