Rafiki yangu mpendwa,
Kama kuna kitu kinaumiza basi ni pale wewe unapochagua kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako, lakini wale uliotegemea wakuunge mkono ndiyo wanakuwa wa kwanza kukukatisha tamaa na kukukosoa.
Unapanga kufanya makubwa na kuwashirikisha wengine mipango hiyo, ukitegemea wataipokea kwa hamasa kubwa na kukupa moyo. Lakini badala yake wanaipokea kwa wasiwasi, wakikuonesha kwa nini haiwezekani, kwa nini utashindwa au kwa nini unachotaka ni tamaa tu na hakina maana.
Unapokutana na hali kama hii ni rahisi sana kukata tamaa, ni rahisi kujiambia hakuna maana ya kujaribu kufanya tofauti. Wakati mwingine unajiambia hutawaambia watu mipango yako mikubwa, lakini unapoifanyia kazi wanajua una mipango mikubwa na wanahakikisha huendelei.
Kama kipo kikwazo kikubwa kwa wengi kupiga hatua, basi kukatishwa tamaa na wengine nako kunachangia kwa kiasi kikubwa sana watu kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.
Rafiki yako leo nimekuandalia njia bora ya kuwazuia watu wasikuseme vibaya na kukukatisha tamaa kwenye yale makubwa unayopanga na kufanya kwenye maisha yako.
Lakini nitaanza hili kwa kukuangusha kidogo, kwa kukuambia ukweli kwamba huwezi. Huwezi kuwazuia watu wasikuseme vibaya au kukukatisha tamaa, ni kazi ngumu sana unayojipa na iliyo nje ya uwezo wako kabisa.
Huwezi kuwalazimisha watu wakuchukulie kama unavyotaka wewe, watu watachagua kukuchukulia wanavyotaka wao, na mara nyingi watajitumia wao kukupima wewe.
Hivyo chochote utakachochagua kufanya, aina yoyote ya maisha utakayochagua kuishi, lazima kutakuwa na watu ambao hawakubaliani na hicho, na watakuwa wa kwanza kukukosoa na kukukatisha tamaa.
Ukiwa na malengo makubwa na kuweka juhudi sana wapo watakaosema una tamaa, huna utu na kadhalika. Usipokuwa na malengo makubwa na ukawa unajiendea tu wapo watakaosema huna maisha, hujui unachofanya na kadhalika.
Ukiwa mtu wa kuongea sana wapo watakaosema una maringo na majitambo, ukiwa mtu wa kutokuongea wapo watakaosema ni msiri na usiyeamini wengine.
Ukiwa mwema sana na kujali kila mtu wapo watakaotumia wema wako kujinufaisha wao wenyewe. Usipoonesha wema sana wapo watakaosema una roho mbaya na hujali.
Ukisimamia kile unachoamini na kusema hapana kwa vile ambavyo siyo muhimu kwako wapo watakaosema ni mkorofi na usiyejali. Usipokuwa na cha kusimamia na ukasema ndiyo kwenye kila kitu watasema wewe ni dhaifu na usiyefaa kutegemewa.
Rafiki, na usije ukafikiri kwamba labda ukiwa katikati ndiyo utawavutia wale ambao wanakupinga. Badala yake kuwa katikati ndiyo utaongeza idadi ya wanaokukosoa na kukukatisha tamaa. Maana ukiwa katikati, unakuwa umeondoka kwenye kila upande na hujaenda kwenye upande wowote, hivyo kila upande utakuwa unakushambulia.
SOMA; Chukua Hatua Hii Muhimu Sana Ili Kulinda Ndoto Kubwa Ya Maisha Yako Na Isivurugwe Na Wengine.
Hivyo tukubaliane huwezi kuwafanya watu wakuchukulie kama unavyotaka wewe, huwezi kukubalika na kila mtu hata ungefanya nini.
Lakini pia hii siyo kusema kwamba huna cha kufanya, siyo kusema inabidi tu ukubali kila mtu akukosoe na kukukatisha tamaa.
Badala yake ipo njia bora kabisa kwako kuzuia wengine wasiwe kikwazo kwako kufanikiwa. Kupitia njia hii, utaweza kufanya yale muhimu kwako, utaweza kuishi maisha yako, bila ya kujali wengine wanasema nini juu yako.
Njia hiyo ni kuwa ‘bize’ sana na maisha yako na yale unayofanya kiasi kwamba huna muda wa kujua hata wengine wanasema nini juu yako. Yaani unakuwa umetingwa sana kwenye kufanyia kazi ndoto zako kiasi kwamba hujui hata wengine wanaongelea nini kuhusu wewe.
Kwa njia hii, akili na nguvu zako zote zinakuwa kwenye kile unachotaka, kiasi kwamba wale wanaokupinga na kukukatisha tamaa hujui hata kama wapo hapa duniani. Hupati hata fikra iwapo kuna watu wanakazana kukurudisha wewe nyuma, kwa sababu nguvu zako umezipeleka kwenye kile unachotaka.
Ukitumia njia hii, unaweza kufanya chochote unachotaka, na kuishi maisha yoyote unayotaka na hakuna atakayeweza kukuzuia kufanya unachotaka. Na pia kama utaishi hili vizuri, mwanzoni watu watakerwa sana na yale unayofanya, lakini kadiri unavyokwenda, watajifunza kukuheshimu sana.
Endesha maisha yako kwa kuangalia kile tu unachotaka, kupeleka rasilimali zako zote kwenye yale unayojali wewe na kuwaacha wengine wahangaike na yale wanayojali wao.
Usipoteze muda wako kuanza kufuatilia nani anasema nini juu yako, nani anakupenda na nani hakupendi.
Kama kuna mtu hakupendi hayo ni matatizo yake binafsi na siyo matatizo yako. Kama unaishi maisha yako, unafanya kile unachojali hasa, halafu kuna mtu anachagua kukuchukia kwa namna unavyoishi, unafikiri nani mwenye matatizo? Haiwezi ikawa wewe ambaye unaishi maisha yako, bali mwenye matatizo atakuwa yule anayefuatilia maisha yako.
Ishi hivi rafiki yangu, na hakuna nguvu yoyote hasi itakayoweza kukurudisha nyuma. Chagua kupeleka nguvu zako kwenye yale muhimu zaidi kwako, na hutasikia kelele za wanaokukatisha tamaa.
Pia usipoteze muda wako kuhangaika na maisha ya wengine, waache watu wachague aina ya maisha wanayotaka kuishi. Usichukizwe na maisha ya wengine au yale wanayofanya, kwa sababu matatizo yatakuwa yako na siyo yao.
Kama utaondoka na kitu kimoja tu kwenye makala hii, basi ondoka na kauli hii, ambayo mimi binafsi nimekuwa najiambia kila siku;
“Nimechagua kuishi maisha yangu, nimechagua kufanya yale ambayo ni muhimu sana kwangu na kutoa mchango bora kwa wale wanaonizunguka na dunia kwa ujumla. Kama kuna mtu hanipendi kwa sababu ya nilivyochagua kuyaendesha maisha yangu, hilo ni tatizo lake binafsi, na siyo tatizo langu.” – Kocha Dr. Makirita Amani.
Ishi maisha yako rafiki, toa mchango mkubwa kwa wale wanaokuzunguka na dunia kwa ujumla, na kama wapo wanaokukosoa, kukukatisha tamaa na kukuchukia, waonee huruma, maana hayo ni matatizo yao wanajaribu kuyaleta kwako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL