Karibu mwanafalsafa kwenye makala zetu za falsafa mpya ya maisha, ambapo tunashirikisha na kujenga falsafa mpya ya maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Maisha yetu ni kile tunachotengeneza wenyewe, iwe tunajua au hatujui. Upo hapo ulipo sasa, kutokana na falsafa ambayo umechagua kuiishi, iwe ulichagua kwa kujua au kutokujua. Na ili uweze kufika sehemu tofauti na ulipo sasa, huna budi kuchagua kuishi falsafa ambayo itakufikisha sehemu hiyo ya tofauti. Hii ndiyo sababu ni muhimu sana utengeneze falsafa ya maisha yako.

IMG-20170314-WA0003

Leo tunakwenda kuangalia maana halisi ya kuwa mtu. Najua unaweza kujiuliza kwani kuna maana gani ya kuwa mtu? Unaweza kuona ni kitu rahisi kuwa mtu, lakini nikudokezee tu, hakuna kitu kigumu, na watu wanachokimbia kama kuwa mtu.

Viumbe wote hapa duniani, kasoro mmoja, wana mtiririko wa maisha yao, ambayo unayafanya maisha yao kuwa rahisi (labda) tangu wanazaliwa, wanakua, wanazaliana na hata kufa. Simba anapozaliwa tu, ni kama tayari ana programu katika akili yake ambayo inamwezesha kupona, hivyo anakuwa anajua namna ya kuwinda, hahitaji miaka mingi kufundishwa. Swala naye anapozaliwa, jukumu lake la kwanza ni kuepuka kuliwa na simba au wanyama wengine wakali. Hivyo hahitaji kuchukua muda kujifunza hilo, la sivyo ataliwa haraka sana na simba na maisha yake yatakuwa yameishia hapo.

SOMA; Hakuna Mkono Wa Mtu….

Viumbe wote hao, ukiacha binadamu, wanazaliwa na asili yao ambayo inayafanya maisha yao kuwa rahisi. Simba hana haja ya kukaa kufikiri atapataje chakula, asili yake inamwezesha kujua wapi swala na vitoweo vingine vinapatikana na kwenda kuwinda. Swala nao hawakai na kufikiria wanawezaje kuwatokomeza simba, bali dalili za simba kuwa karibu zinapowajia, ambazo tayari zipo kwenye asili yao, huanza kutimua mbio.

Lakini binadamu, amezaliwa kwenye mazingira ambayo hayampi asili ya maisha yake kuwa rahisi. Haamki tu na kwenda kuwinda, au kuepuka kuliwa. Binadamu yupo kwenye mazingira ambayo siyo rahisi kwake kuweza kupata kile ambacho ni muhimu kwake. Na hapo sasa ndipo inakuja kazi kuu kabisa ya binadamu, ambayo viumbe wengine hawawezi kuifanya. Kwa kazi hii binadamu anaweza kuwawinda viumbe wengine, kuepuka kuwindwa na kuweza kuyatumia mazingira yake vizuri. Ni kazi hii ambavyo inamwezesha binadamu kutawala viumbe wengine wote.

Kazi hii ya kipekee kabisa kwa binadamu ni KUFIKIRI.

Kufikiri ndiyo kazi kuu ya binadamu, ambayo yeyote anayeweza kuifanya vizuri, maisha yake yanakuwa bora sana. Ni kazi ambayo inatumia akili, kwa kukusanya taarifa zote ambazo zinamzunguka mtu, na mwisho kuja na hitimisho la hatua gani mtu achukue.

Pamoja na ilivyo rahisi kutamka kufikiri, hakuna kitu kigumu kufanya, na wengi wanakikimbia kama kufikiri. Watu watafanya lolote kuepuka kufikiri. Watu hupenda njia za mkato, za kufanya kidogo na kupata kikubwa. Watasikiliza kila mtu lakini hawatajipa muda wa kukaa chini na kufikiri kwa kina, kwa kutumia uwezo mkubwa ambao upo ndani yao.

Ukitaka kuliona hili kwa uwazi kabisa, angalia watu wengi wanaoshabikia au kufuata kitu. Unaweza kumwuliza mtu kwa nini anafanya hivyo, asiwe na jibu la uhakika. Ukichunguza amejiunga kwa sababu wengi wapo pale, na anakuwa na amani kwamba kama wengi wanakubaliana na hili, basi litakuwa sahihi.

Watu wamekuwa wanafanya mambo kwa mazoea, wanaficha kabisa uwezo wao wa kufikiri. Kwenye kazi, biashara na hata maisha, watu wanaendelea kufanya kile walichofanya jana, mpaka wanafika wakati kufanya kitu hicho hakuwasaidii tena na mwishowe kuwa wameachwa nyuma.

Kila kiumbe hapa duniani, huwa kinazaa matunda fulani. Mti wa embe huzaa embe, mti wa papai unatoa papai. Na hata miti ambayo haina matunda, huwa inatoa kivuli na mengine muhimu. Matunda ya binadamu kwenye hii dunia, ni kutumia fikra zake kuiboresha zaidi. Kuhakikisha dunia inakuwa sehemu salama na bora sana ya kuishi.

Tunaona matunda ya wachache waliofanya hivyo, walioandika falsafa nzuri ambazo watu wameweza kuziishi na zikawasaidia. Waliofikiri na kuja na njia bora za kufanya vitu, zikaja mashine na viwanda. Wakaendelea kufikiri na teknolojia ikaendelea kukua zaidi. Kila unachofurahia sasa, iwe ni simu, nguo, gari, nyumba na mengine, ni mazao ya binadamu waliofanya kazi yao. Ambao waliona mambo yanaweza kuwa bora zaidi, wakafikiri kwa kina na kuja na njia ya kufanya mambo kuwa bora zaidi. Walioona usafiri wa punda na farasi siyo wa uhakika, wakaja na magari moshi, baadaye magari na mpaka kufikia ndege. Vitu hivi havikuibuka tu, havikushushwa kutoka popote, bali ni mazao ya binadamu waliochagua kufanya kazi yao sawasawa.

Leo hii ukiumwa zipo dawa nyingi za kuweza kutibu ugonjwa wako. Lakini miaka 100 tu iliyopita, hakukuwa na dawa nyingi kama leo. Hakukuwa na dawa ya uhakika ya kuweza kuua bakteria (antibiotic) na watu walikufa, maelfu kwa maelfu kwa ugonjwa ambao leo unaweza kuutibu kwa dawa unayoweza kununua shilingi elfu moja kwa dozi nzima.

Binadamu anapofanya kazi yake, maisha yanakuwa bora kwake na kwa kila mtu. Binadamu anapokubali kukaa chini na kufikiri kwa kina, kwa kuyaangalia mazingira aliyopo, halafu akaweza taswira yake, ya namna yanavyoweza kuwa bora zaidi, anakuja na vitu bora sana vinavyomnufaisha kila mtu.

SOMA; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…

Lakini kwa nini inakuwa ngumu kwa binadamu kufanya kazi yake ya kufikiri?

Pamoja na urahisi wa kufikiri tulioona, pamoja na umuhimu wake kwenye maisha ya wanadamu wote. Bado ni wachache sana wanaoweza kufikiri kwa kina na kuja na majibu bora kwa matatizo ya watu. Kwa nini hali iko hivi?

Moja; inahitaji ujasiri wa kipekee kukaa chini na kufikiri. Unahitaji kujitoa kwenye kelele za wengi, kutuliza akili yako na kufikiri. Sasa, hakuna kazi ngumu kama kutuliza akili, kwa sababu kelele ni nyingi ambazo zinataka uzifuatilie. Na kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo kelele zinavyokuwa nyingi zaidi. Zamani ilikuwa ni tv na redio, sasa hivi ni mitandao ya kijamii na simu zetu. Masaa 24 tumezungukwa na kelele, tunaamka nazo na tunaenda kulala nazo.

Mbili; unahitaji kupingana na wengi. Vijana waliokuwa wanatengeneza ndege kwa mara ya kwanza, watu walisema wana ugonjwa wa akili. Walishangaa watu hao wameingiwa na pepo gani, kufikiri kwamba mtu anaweza kuruka hewani? Kwa kuwa hawakukubali kuacha, tumepata ndege zinazotusaidia sana sasa. Hivyo chochote kipya na kikubwa utakachofikiri, dunia itakupinga sana, lazima uwe mbishi na kuendelea, mpaka upate unachotaka.

Nimalize kwa kukuambia mwanafalsafa mwenzangu, tukae chini na kufanya kazi yetu sisi wanadamu, tufikiri kwa kina. Tutenge muda kila siku, tunapoianza siku yetu au tunapoimaliza, na tufikiri kwa kina, kupata suluhisho la changamoto tunazopitia sisi wenyewe na hata jamii kwa ujumla. Tuepuke kufuata kundi kubwa la wengi, ambao wanakimbia kufikiri. Sisi tujipe uhuru wa kufikiri tofauti, hata kama tunachekwa na kubezwa.

Wanaofikiri ndiyo wanaoijenga dunia, na wanaofikiri ndiyo wataiokoa dunia. Tufanye kazi yetu, tufikiri kwa kina.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog