Linapokuja swala la fedha, kuna vitu vikuu viwili;

Cha kwanza ni mapato, kile ambacho unapata kutoka kwenye kazi au biashara ambayo unaifanya.

Kitu cha pili ni matumizi, namna ambavyo unatumia kile kipato chako.

IMG-20170314-WA0002

Changamoto kubwa sana kwenye fedha huwa inaanza pale matumizi yanapozidi mapato, hapo ndipo wengi hujikuta wanaingia kwenye mikopo, ambayo inawaumiza zaidi ya kuwasaidia. Hivyo hatua ya kwanza ni ya muhimu kabisa kwa yeyote ambaye yupo kwenye changamoto za kifedha, ni kubana matumizi. Kuanza kuangalia yale matumizi yake, kuona yapi ni ya muhimu kabisa na yapi siyo ya muhimu. Baada ya kujua yale muhimu, unaondokana na yale yote ambayo siyo muhimu.

Kwa kuchukua hatua hii, mtu anapata ahueni, angalau sasa anajikuta halazimiki tena kuingia kwenye madeni, kama ilivyokuwa awali. Anafurahia maisha na uhuru alioupata kwenye fedha. Lakini haichukui muda, anajikuta tena matumizi yanazidi kipato, anarudi tena kwenye madeni, na kufikiria labda amekosa nidhamu ndiyo maana ameanguka tena.

SOMA;  Mipango Siyo Matumizi…

Ukweli ni kwamba huenda hajakosa nidhamu, ila kuna kosa moja analofanya ambalo ni kufikiri kubana matumizi ni mbinu ya kutajirika. Hili ni kosa linalofanywa na wengi, na hata baadhi ya waandishi wamekuwa wanasisitiza bada matumizi ili uwe tajiri. Huwezi kuwa tajiri kwa kubana matumizi pekee. Sawa na ilivyo kwamba huwezi kutibu homa ya malaria kwa kutumia paracetamol. Hiyo inatuliza tu, matibabu kamili lazima yafuate baada ya kuwa umetuliza tatizo.

Inapokuja kwenye utajiri, mbinu au njia pekee ya kujijengea utajiri ni kuongeza kipato kupitia mifereji mbalimbali ya kuingiza kipato. Na siyo kubana matumizi pekee kama wengi wanavyofikiri.

Kubana matumizi ni hatua ya kuanza, lakini changamoto yake ni kwamba, kuna kikomo kwenye kubana matumizi. Yaani huwezi kubana matumizi mpaka yakafika sifuri kabisa. Kwa sababu kuna mambo ya msingi kwenye maisha lazima ufanye, kula, kuvaa na maisha mengine. Hivyo bana matumizi uwezavyo, lakini kuna ukomo. Kitu chochote chenye ukomo, hakiwezi kukuletea utajiri, sawa na mshahara, una ukomo ndiyo maana huwezi kutajirika kwa mshahara pekee.

Kitu kisicho na ukomo ndiyo kinacholeta utajiri, na kati ya matumizi na kipato, unahitaji kuweka mkazo zaidi kwenye kipato. Kuongeza kipato chako zaidi na zaidi kila siku ndiyo njia ya kujijengea utajiri kwenye maisha yako.

Unahitaji kuangalia njia tofauti tofauti za kuongeza kipato chako, na siyo ile uliyonayo kwa sasa pekee. Kwa sababu unapokuwa na njia moja pekee kuna wakati inaweza kufikia kikomo. Hivyo kuwa na mifereji mingi ya kukuingizia kipato ni njia muhimu ya kukufikisha wewe kwenye utajiri.

SOMA; Makadirio Ya Matumizi Na Faida.

Unapokuwa na mifereji mingi inakusaidia wewe kuepuka changamoto za mfereji wa aina moja. Mfano wakati eneo moja la kipato chako linapitia changamoto, maeneo mengine yanakuwa yanaendelea kuingiza kipato.

Mara zote unapofikiria kuwa na uhuru wa kifedha na kufikia utajiri, kuongeza kipato chako kunastahili kupewa kipaumbele kikubwa. Sisemi usizingatie kudhibiti matumizi, hili lazima ulifanye kila wakati, lakini kumbuka siyo jawabu, jawabu kamili ni kuongeza kipato.

Kama kudhibiti matumizi kunakuwa kugumu kwako, ipo njia moja ya kuyafanya matumizi yako kuwa chanzo chako cha utajiri. kwa mfano kuna gari zuri sana umeliona, umependa kuwa nalo, ila halitakuzalishia chochote, hivyo kuchukua fedha zako ambazo kwa sasa zinazalisha na kwenda kununua gari ile, hayatakuwa maamuzi sahihi. Lakini bado hupati usingizi ukifikiria gari hiyo. Sasa cha kufanya hapo, ni kugeuza hitaji hilo la gari kuwa chanzo cha kuongeza kipato. Na unachofanya ni kuangalia kwa pale ulipo sasa, kitu gani unaweza kufanya na kikakuongezea kipato kitakachokuwezesha kununua gari hiyo?

Unaona hapo, hubadili chochote unachofanya sasa, wala huondoi fedha popote, unachofanya ni kutafuta chanzo kipya cha fedha, ili uweze kukidhi matumizi yako mapya. Hivyo unaweza kutumia biashara zako ulizonazo sasa, kutengeneza fedha zaidi na kuhakikisha unafikia kiasi unachotaka kununua gari. Au kuangalia fursa nyingine unazoweza kutumia na ukaweza kununua gari hiyo.

Nafikiri unaona namna ambavyo ukipiga hatua zaidi tu ya kudhibiti matumizi unaweza kufaidika zaidi. Kwa mfano kama hukuwa na wazo la kuongeza kipato, wazo la kununua gari ungeliondoa kabisa, kwa sababu siyo matumizi muhimu. Ila unapofikiria kuongeza kipato, wazo la kununua gari linakuwa kichocheo kwako kuongeza kipato ili uweze kununua kile unachotaka.

Mwisho kabisa nimalizie na kukukumbusha kwamba unapofikiria kuongeza kipato, anza kwa kufikiria eneo gani unaweza kuongeza thamani zaidi. Angalia wapi unaweza kutatua matatizo zaidi, au wapi unaweza kutimiza mahitaji yao. Kwa kuanzia kwenye kazi yako, biashara yako na hata maisha yako ya kila siku, utaziona fursa nyingi za kufanya hivyo. Muhimu ni wazo hili liwe kwenye akili yako mara zote. Maana wanasema macho hayawezi kuona kile ambacho akili haijui. Unaweza kuwa unaishi na kitu kila siku lakini hujui ni fedha, ila akatoka mtu huko na kuja kunufaika nacho.

Unapofikiria utajiri, dhibiti matumizi yako kama sehemu ya kuanzia, ila weka mkazo sana kwenye kuongeza kipato chako, na kuongeza njia zako za kutengeneza kipato.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog