Hisa ni moja ya aina ya uwekezaji ambapo unaweka fedha yako kwenye makampuni ya umma, fedha inatumika kwenye kuendesha makampuni hayo na baadaye unanufaika kwa thamani ya hisa kuongezeka na/au kupata gawio kutoka kwenye kampuni pale inapotengeneza faida.

IMG-20170301-WA0001

Uwekezaji kwenye hisa ni moja ya maeneo muhimu ambayo kila mwekezaji anapaswa kuwekeza, kutokana na urahisi wake na pia kuweza kuanza na mtaji kidogo. Pamoja na umuhimu huu wa uwekezaji kwenye hisa, watu wengi bado hawana uelewa juu ya uwekezaji kwenye hisa. Hii inapelekea wengi kuamua kutokuwekeza kabisa na hivyo kukosa fursa hii nzuri ya uwekezaji.

Uwekezaji kwenye hisa kwa Tanzania unasimamiwa na Soko la hisa la Dar es salaam (DSE). Katika soko hili la hisa makampuni 25 yamesajili hisa zake na kwa ujumla hisa hizo zina thamani ya TZS 24.5 trillioni, pia soko hili limesajili hati fungani za makampuni mbalimbali na serikali zenye thamani ya TZS 4 trillioni. Hili ni soko linalokua kwa kasi na hivyo ni fursa kwa kila mtanzania kuwa mwekezaji.

Sasa katika hisa hizo 21, unawezaje kuchagua hisa zipi uanze kuwekeza? Kupitia kwa wawekezaji wenye mafanikio duniani, kama Warren Buffet, nimejifunza mambo mengi kuhusu uwekezaji. Na hapa nitakushirikisha sheria tano za kufuata wakati unachagua hisa za kununua.

SOMA; Tengeneza Sheria Zako Mwenyewe….

Sheria ya kwanza; wekeza kwenye hisa ambazo biashara yake inaeleweka.

Kazi ya kwanza ya mwekezaji yeyote, ni kujua ule uwekezaji ambao anaufanya. Hivyo kabla hujanunua hisa za kampuni yoyote, unapaswa kuijua kampuni hiyo. Kitu cha kwanza kabisa kuangalia kwenye kampuni, ni mfumo wake wa biashara. Je ni biashara ambayo inaeleweka kwa kila mtu?

Zipo kampuni ambazo biashara zake ni rahisi kueleweka hivyo hata unapofuatilia, unajua wapi wanatoka na wapi wanakwenda. Hii inakuwezesha wewe mwekezaji kujua kwa hakika nini kinaendelea. Kwa zile biashara ambazo mfumo wake wa biashara siyo rahisi kueleweka na mtu wa kawaida, siyo nzuri kwako kuwekeza, kwa sababu hutakuwa na uhakika wa kile unachofanya.

Sheria ya pili; wekeza kwenye kampuni ambazo zimeshajijengea jina zuri.

Sifa ya kampuni unayokwenda kuwekeza ni muhimu, kwa sababu kampuni yenye sifa nzuri na jina ambalo limeshajengeka, ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi baadaye. Kampuni ambayo inaendeshwa vizuri na hivyo kufanya mambo yake kwa ubora wa hali ya juu, inakupa wewe urahisi wa kujua kama uwekezaji wako utakulipa au la.

Kuwekeza kwenye kampuni ambayo ina sifa mbaya, kutokana na uendeshwaji wake au maamuzi yanayofanywa, utakuwa umejipeleka kupoteza uwekezaji wako. Sifa ya kampuni ina mchango mkubwa kwenye ukuaji. Wateja wanaamini zaidi kampuni zenye sifa nzuri kuliko zenye sifa mbaya. Na hata kwenye majina, kampuni yenye jina kubwa, inapendelewa zaidi kuliko kampuni ambayo haina jina.

Sheria ya tatu; angalia ufanisi wa hisa kwa kipindi cha nyuma.

Unapotaka kuwa mwekezaji mwenye mafanikio, basi usiwe mvivu. Kwa sababu watu wengi wanapenda kuambiwa nunua hisa fulani na utafanikiwa. Wanakimbilia kununua bila ya kufanya utafiti wao wenyewe. Unahitaji kuangalia ufanisi wa hisa za kampuni kwa kipindi cha nyuma. Unahitaji kwenda nyuma miaka mingi kuona ufanisi wa hisa za kampuni hiyo upoje. Kama mara zote hisa za kampuni hiyo zinashuka, na hazijawahi kufanya vizuri hata wakati mmoja, siyo maamuzi mazuri kuzinunua.

Unaweza kuangalia mwenendo wa hisa za kampuni yoyote kwenye taarifa za hisa na makampuni kwenye tovuti ya sokola hisa la Dar es salaam. Tembelea tovuti yao http://dse.co.tz/listed-companies ukifungua hapo, unaweza kuchagua kampuni na kuangalia mwenendo wa hisa zake.

Hili haliwezekani kwa kampuni ambazo zinaingiza hisa zake kwa mara ya kwanza kwenye soko. Hivyo katika hali hiyo ya upya sokoni, tumia sheria nyingine tunazojadili hapa.

SOMA; Jinsi Ya Kuchagua Uwekezaji Unaokufaa Wewe Kulingana Na Mahitaji Yako.

Sheria ya nne; weka mkazo kwenye kampuni zinazotoa gawio.

Kwenye uwekezaji wa hisa, unaweza kunufaika kwa kuongezeka kwa thamani ya hisa na pia unaweza kunufaika kwa kupata gawio kutoka kwenye kampuni. Gawio hutolewa mwisho wa mwaka wa fedha wa kampuni, hivyo sehemu ya faida inagawanywa kwa wanahisa kulingana na hisa wanazomiliki.

Unapofikiria hisa za kununua, weka mkazo kwenye hisa za kampuni ambazo zinatoa gawio. Kwa njia hii unakuwa unanufaika kila gawio linapotolewa, huku hisa zako zikiendelea kubaki kama zilivyo. Kampuni zinazotoa gawio, unaweza kunufaika hata kama thamani ya hisa haijapanda, kutokana na sababu za kiuchumi.

Kujua kampuni kama inatoa gawio au la unahitaji kufuatilia mwongozo wake wa uwekezaji, ambalo inakuwa imeeleza kama inatoa gawio na inatoa kwa utaratibu gani.

Sheria ya tano; nunua hisa ambazo bei yake ipo chini, au ndiyo zinaingia sokoni.

Baada ya kufanya utafiti wako wa kina, na kuona baadhi ya makampuni ambayo yana sifa ambazo tumejifunza hapo juu, kitu muhimu cha kuangalia ni bei ya hisa na kwa muda gani hisa zimekuwepo sokoni.

Kuna wakati baadhi ya hisa huwa zinapanda bei na kufika wakati zikashuka bei. Kwa hisa za aina hii, ni vyema kuzinunua wakati bei ipo chini, kwani wakati huo wengi hukimbilia kuuza na hivyo kuweza kununua kwa bei ya chini zaidi. Lakini kumbuka zisiwe ni hisa ambazo zimekuwa chini muda wote.

Pia kama kampuni bado ni mpya kwenye soko la hisa, unaweza kununua hisa zake, kama unaweza kusubiri kwa muda mrefu. Hii itakunufaisha zaidi baadaye kwa sababu mara nyingi watu huwa hawachukui hatua kwa kampuni mpya, ila zinapoonekana kufanya vizuri, thamani ya hisa zake hukua haraka.

Hizi ndiyo sheria tano za kuzingatia pale unapofikiria ni hisa za kampuni gani ununue. Japo ni sheria lakini hazijaandikwa kwenye jiwe kiasi cha kusema hazibadiliki au hazipingiki. Hii ni sehemu tu ya kuanzia kwenye safari yako ya kufanya utafiti kabla hujawekeza kwenye kampuni husika. Kadiri unavyochimba zaidi utajifunza mengi na kuweza kufanya maamuzi sahihi.

Mwekezaji makini huwa na taarifa sahihi na kufanya maamuzi mazuri juu ya uwekezaji wake. Hakikisha unapata taarifa na maarifa sahihi kwenye uwekezaji wowote unaofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog