Hakuna mtu ambaye hapendi kuwa bora, kila mtu anapenda kufanya mambo makubwa, kuwasaidia wengi, kupata mafanikio na pia kukumbukwa na wengi kwa namna walivyofanya makubwa.

IMG-20170228-WA0004

Kila mtu ana ukuu ndani yake, ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo ya kipekee hapa duniani, mambo ambayo hakuna mwingine awezaye kuyafanya, mambo ambayo dunia kwa sasa haijapata kuyaona.

Nimekuwa nasema pia watu wengi wanaidhulumu dunia. Kwa sababu wana vitu vizuri sana ndani yao, wana kazi kubwa ambazo kama wangezifanya basi dunia ingenufaika sana. Lakini hawazifanyi, wanakufa na ukuu huo ndani yao, na hii ndiyo inapelekea sehemu kubwa yenye utajiri duniani kuwa makaburini.

Hebu kuwa mwaminifu kwako na jipe majibu ya swali hili muhimu; ni mambo gani makubwa unayotamani kufanya kwenye maisha yako, lakini bado huyafanyi? Ni ndoto gani kubwa ambazo umekuwa nazo kila siku, lakini unajiambia huo ni utoto, huwezi kuzifikia? Kwa kazi unayofanya, umekuwa unajiona wapi kupitia kazi hiyo ili kuhesabu mafanikio makubwa? Vipi kwa biashara yako? Unataka kuniambia kweli kabisa ukilala unapata usingizi mzuri kwa hapo ulipo? Si unazo ndoto kubwa zaidi? Za kuwa na biashara kubwa zaidi, kuwafikia wengi zaidi?

Sasa kwa nini unashindwa kuanza kufanyia kazi ndoto zako hizo kubwa? Kwa nini unaendelea kuwa hapo ulipo, ukifanya kile unachofanya sasa? Kwenye makala hii ya leo, tutakwenda kuchimba ndani kabisa na kuja na majibu ambayo hayatakufurahisha, lakini lazima uyachukue na uyafanyie kazi, kama kweli unataka kufanikiwa na kuishi maisha ya ndoto yako.

Majibu haya hayatakuwa ya kubembeleza, na wala hayatakuwa rahisi, ndiyo ukweli ulivyo siku zote. Wale wasio na kifua huwa hawapendi kuuangalia na hivyo hugeukia upande rahisi, ambao siyo ukweli.

Haya ndiyo yanayokuzuia kufanya kazi bora sana itakayokupa mafanikio makubwa. Yajue na chukua hatua stahiki ili uweze kufika unakotaka kufika.

SOMA; Njia Mbili Za Kupima Ukuu Wako.

  1. Unataka kumridhisha kila mtu.

Jambo lolote utakalochagua kufanya kwenye maisha yako, hata liwe zuri kiasi gani, watajitokeza watu na kukupinga kwa kulifanya, au kwa namna unavyolifanya. Wengine watakuja na maoni ambayo watataka wewe uyafanyie kazi, kwa sababu kwa mtazamo wao maoni hayo unayahitaji sana, la sivyo hutafika mbali. Hakuna kitu utakachofanya waache kujitokeza watu wa aina hii, hata kama utafanya kitu kidogo kiasi gani.

Chukua mfano huu na ufanye hata kesho tu, chukua shilingi elfu 10 na tafuta chenchi uwe na shilingi mia tano mia tano. Kisha fika eneo la barabara lenye watu wengi, na kila anayepita mpe shilingi mia tano. Msalimie na mpe mia tano yake. wewe umefanya tu kwa sababu zako binafsi na wala hutaki chochote kutoka kwa yeyote. Sasa subiri maoni na upingwaji utakaoupata kutoka kwa wengi. Wengine watasema hujui namna ya kutumia fedha zako, wengine watasema unazipoteza, wengine watasema kama kweli ulitaka kutoa msaada ungeenda kituo cha watoto yatima na kutoa, wengine watasema una ndugu zako hujawasaidia ila unasaidia usiowajua. Yaani utapata maoni na ushauri mwingi kuliko hata unavyoweza kuufanyia kazi.

Sasa turudi kwenye biashara yako, au kazi unayofanya na unataka kuiboresha zaidi ili ufanikiwe. Hapo kuna maoni mengi sana utakayopata kutoka kwa kila mtu, akikuambia namna gani unaweza kuifanya vizuri zaidi. Maoni hayo ni mazuri sana, lakini mwenye maono ya biashara yako ni wewe mwenyewe. Wewe ndiyo una picha halisi ya wapi unataka kufika. Wale wengine wanaona kwa nje tu, na wanaona hatua za haraka za kuchukua. Lakini zile hatua ngumu za kufika mbali, hawawezi kuziona.

Hivyo kusikiliza maoni ya kila mtu, na ukayafanyia kazi kwa sababu yanaonekana ni mazuri, unakuwa umepiga hatua ya kwanza ya kukuzuia wewe kufanya kazi bora. Kwa sababu unajikuta unazika ndoto yako na kuanza kufanya yale ambayo watu wanasema. Au kuanza kushindana na soko, kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Unaondoka kwenye njia yako maalumu na unaingia kwenye njia ya wengi. Na huko ndiyo unakutana na kelele nyingi na kupotezwa na kelele hizo, usikumbuke tena unakotaka kwenda.

Hatua ya kuchukua;

Najua una ndoto na maono makubwa juu ya biashara unayofanya sasa. Najua ni wewe pekee ambaye unaielewa sawasawa ndoto hiyo. Hivyo basi, iandike ndoto hiyo kwa maneno, tengeneza picha ya ndoto hiyo, ambayo utaiona kila siku. Halafu panga hatua za kuchukua ili kufikia ndoto hiyo. Sasa wanapokuja watu na maoni yao, yasikilize, yanadike vizuri, ila rudi kwenye ndoto yako na mpango wako mkuu wa utekelezaji, halafu angalia kama maoni hayo yanaweza kuboresha chochote katika mpango wako wa utekelezaji. Kama yanaweza kuboresha yaingize pale yanapofaa. Kama maoni hayo hayawezi kuboresha, basi achana nayo na wala usiyafikirie tena. Weka muda kwenye kufanya yale ambayo ni sahihi kwako kwa wakati huo.

SOMA; Maadui Kumi(10) Wa Ubora Wa Hali Ya Juu.

  1. Unajionea huruma sana.

Mwandishi mmoja alitoa mfano kwamba alikuwa anaongea na rafiki yake, akamwambia anapenda sana kujifunza kuogelea. Rafiki yake akamwambia safi sana, twende tukanunue mavazi ya kuogelea na twende baharini tukaogelee. Mwandishi yule akaonesha mshangao, kwamba hajawahi kuogelea kabisa halafu mara moja akaogelee baharini? Rafiki yake akamwambia jifunze utakavyo, lakini kama hutaingia baharini na kuogelea, hutakuja kujua kuogelea.

Njia ya mafanikio siyo rahisi, chochote unachotaka kuwa bora sana, siyo rahisi. Kitakuwa kigumu wakati unapoanza, kitakuwa kigumu zaidi kabla hakijawa rahisi. Sasa kinachotokea ni nini? Mambo yanapokuwa magumu wengi hujiambia kwa nini nijitese? Wanaacha na kurudi kufanya yale ambayo ni rahisi. Na mimi nakuambia, kimbilia kufanya marahisi utakavyo, lakini hutakuwa bora, na hutafanikiwa kama hutafanya mambo magumu, yanayowatisha wengine.

Kama unajionea huruma na kuona unastahili kupumzika au kuwa na maisha mazuri kama ya wengine, hutauona ukuu. Kama ukitoka kazini au kwenye biashara yako, jioni unakaa na marafiki mkipata moja moto na moja baridi, hutauona ukuu. Utaishia kwenye ngazi hizo hizo. Ukuu unahitaji kazi, ukuu unahitaji muda, ukuu unahitaji kujitoa. Ni kwa kiasi gani unajitoa?

Ukitaka kujua kama unajitoa au la, angalia marafiki zako wanakuchukuliaje. Kama wanakuambia umekuwa adimu kupatikana, unafanya kazi sana, au huna muda wa kupumzika, ni dalili umejitoa. Lakini kama hawana malalamiko yoyote kwako, kila wakati wanakupata kama watakavyo, haupo hata karibu na ukuu, umeshaacha njia ya ukuu na unakazana kuwa kawaida.

Hatua ya kuchukua;

Chagua muda ambao utajitoa sana kwenye kile kikubwa ambacho unataka kufanya. Chagua muda wa kuwa mbali, muda wa kuweka juhudi kubwa ambao hautaingiliwa na wengine. Mambo yanapokuwa magumu ndiyo unahitaji kuendelea zaidi, ugumu ndiyo unapaswa kuwa hamasa kwako. Usikimbie wala kurudi nyuma, kwa sababu dawa ya kushinda ugumu, ni wewe kuwa mgumu zaidi. Usijionee huruma, hakuna ambaye atatoka hapa duniani akiwa hai, hivyo pambana kufikia ukuu.

  1. Bado hujawa na roho mbaya ya kutosha.

Nafikiri kama unaishi kwenye jamii ya kawaida, utakuwa unajua mtazamo wa jamii juu ya waliofanikiwa, kwamba wana roho mbaya. Huenda na wewe ulikua ukiamini hivyo, kwamba waliofanikiwa wana roho mbaya, matajiri wana roho mbaya. Au huenda mpaka sasa bado una imani hiyo, kwamba waliofanikiwa wana roho mbaya.

Wala usiishangae jamii kwenye hilo, kwa sababu roho mbaya kwa jamii, ni pale mtu anapofanya jambo ambayo wao hawataki. Au mtu anapokataa kufanya jambo ambalo wao wanataka. Hivyo basi, kama unaonekana una uwezo kifedha, na akaja mtu kukuomba umsaidie fedha, ukagundua kwamba hata ukimpa fedha hazitamsaidia kama anavyofikiri, ukimwambia huwezi kumpa, utaambiwa una roho mbaya. Na pale mtu huyo anapokuwa ndugu wa karibu, ndivyo roho yako inavyoonekana kuwa mbaya zaidi.

Kila mtu kwenye jamii anataka wewe ufanye kile anachotaka yeye. Mtu anataka akupigie simu muda wowote anaotaka yeye, ana upokee na kuongea naye. Au aje kwenye kazi au biashara yako, muda wowote anaojisikia yeye na umsikilize hata kama kilichomleta siyo kazi au biashara. Utakapojaribu kusema tu HAPANA, basi hapo ndipo utakapoonekana una roho mbaya.

Na mimi nakuambia, unahitaji kuwa na roho mbaya zaidi, kwa maana kwamba unahitaji kusema HAPANA. Watu watakuja kwako na mapendekezo mengi sana, mengine mazuri mengine siyo mazuri. Usikimbilie tu kusema NDIYO ili kuwaridhisha watu na usionekane una roho mbaya. Jua kabisa huwezi kufanya kila kitu ambacho kila mtu anataka ufanye. Hivyo jibu lako la kwanza linahitaji kuwa hapana. Hapana itakupa wewe muda wa kuweka juhudi kwenye lile eneo ambalo unataka kuwa bora zaidi.

Kwa jambo lolote linalohitaji muda wako wewe, na ili upate muda lazima uache kufanya lile ambalo ndiyo unataka kuwa bora zaidi, sema hapana. Kuwa bahili sana wa muda wako, hakikisha unachokubali ni kile muhimu sana, na ambacho kina msaada kwa wengine na kinafaa kufanya na kuweka pembeni kwa muda kile ambacho ni muhimu zaidi kwako. Na amini, hakuna kabisa, au ni vitu vichache sana, vyenye hadhi ya kuchukua muda wako wa kufanya kile ambacho unataka kuwa bora.

  1. Unachinja ng’ombe wako kwa oda ya maini.

Au pia unamuuzia ng’ombe mteja ambaye ameyapenda maziwa yako. Kwa mfano kama hivyo inaonekana ni jambo la kijinga sana kufanya. Hivi kweli mtu  na akili yake, anaweza kumchinja ng’ombe wake kwa sababu kuna mtu ameweka oda ya maini? Au mteja wa maziwa kasema maziwa yako ni mazuri na anataka umuuzie ng’ombe kabisa! Kweli mtu anauza?

Labda tuangalie upande wa pili. Thamani ya ng’ombe yako ni shilingi laki tano, mteja kakuambia anahitaji sana maini, na yupo tayari kulipa milioni moja apate maini hayo. Au yule wa maziwa anakuambia anakupa milioni moja umuuzie ng’ombe wako ambaye thamani yake ni laki tano. Hapo vipi? Si unaweza kufikiria tofauti, kwamba unaweza kwenda kuwa na ng’ombe wengine wengi zaidi?

Sasa tukija kwenye uhalisia, hayo ni mambo ambayo watu wamekuwa wanafanya kila siku, huenda na wewe unafanya pia. Mtu anakubali kuajiriwa na kuzika ndoto zake kubwa za maisha ambazo alikuwa nazo nje ya ajira. Au mtu anaanzisha biashara yake, au kampuni yake, na mmoja wa wateja anamwambia nataka kununua kampuni yako kabisa. Kuna wakati unaweza kuona ni hatua nzuri kufanya hivyo, lakini nikuambie wazi, hutafikia ukuu kwa kwenda hivyo. Lazima uchague eneo unalotaka kuwa bora zaidi, na weka juhudi zako zote kuhakikisha unafanya jambo kubwa. Usikatishwe na wale wanaokuonesha mambo mazuri lakini ya muda mfupi, jitoe kukosa hayo mazuri kwa muda, lakini ujihakikishie kupata makubwa zaidi huko mbeleni.

Rafiki, hayo ni mambo ambayo yanawazuia wengi kufikia ukuu, yamekuwa yanatuzuia wote, hivyo ni wajibu wetu kupambana kuhakikisha mambo haya hayawi kikwazo kwenye safari yetu. Fanyia kazi haya ambayo tumejifunza hapa leo ili kuweza kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog