Moja ya tabia zinazotuzuia kufanikiwa, ni tabia yetu ya kusema ndiyo kwenye kila kitu ambacho tunaombwa na wengine. Katika makala ya mambo manne yanayokuzuia kufanikiwa (unaweza kuisoma kwa kubonyeza maandishi haya) nilieleza kwamba hujawa na roho mbaya vya kutosha. Nikikueleza umuhimu wa kusema hapana kwa yale mambo ambayo wengine wanakutaka ufanye, japo hayana mchango wowote kwako wala kwao, kwa kifupi ni kupotezeana muda.
Lakini naelewa ni namna gani ilivyo vigumu kusema hapana, hasa anayekutaka ufanye kitu ni mtu wa karibu kwako kimahusiano, au mzazi wako, au wakati mwingine mwajiri wako. Hivi nilikwambia unapaswa kumwambia hata mwajiri wako HAPANA? Ndiyo, hata yeye anastahili hapana, kwa sababu kuna wakati anaweza kujisahau, akakupa majukumu yanayokuzuia wewe kumaliza kazi muhimu ambayo ingeleta manufaa makubwa kwenu wote.
Leo tunakwenda kujifunza jinsi ya kusema hapana kistaarabu, kwa wale ambao hawawezi kusema hapana. Kile utakachokwenda kujifunza leo, kitakuwezesha kuepuka kusema ndiyo kwenye kila kitu, na kuhakikisha unaposema ndiyo, ni ndiyo yenye manufaa kwa kila mtu. Karibu sana tujifunze ili tuweze kulinda muda wetu na kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwetu na kwa wengine.
SOMA; Sababu Halisi Ya Watu Kukuambia HAPANA…
Njia tunayokwenda kujifunza hapa, ni kusema ndiyo taratibu sana, yaani unapoulizwa au kuombwa kitu, badala ya kukimbilia kusema hapana, ambacho ndiyo kitu tumezoea wote, unachukua muda kidogo kusema ndiyo, na kwenye huo muda unachofanya ndiyo bora zaidi, maana mara nyingi kinapelekea anayekuomba aseme hapana yeye mwenyewe kabla hata hujasema hapana.
Hivyo basi, anapokuja mtu na maombi au mapendekezo ambayo yanakutaka wewe utoe muda wako kwenye kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi, na kufanya mengine ambayo mtu yule amependekeza, chukua hatua zifuatazo;
Hatua ya kwanza; mshukuru kwa kukuchagua wewe ndiye umsaidie kile ambacho anataka umsaidie. Kama haifai kumshukuru, sema tu neno lolote kwake kutambua uwepo wako.
Hatua ya pili; mwulize maswali muhimu kwenye maeneo haya matatu;
Eneo la kwanza; kwa nini mimi?
Mwulize kwa nini amekuchagua wewe ndiyo ufanye kile anachokutaka wewe ufanye? Ni kipi hasa kimemfanya aje kwako?
Swali jingine muulize kama ameshauliza wengine, kama ameshafikiria kuhusu wengine.
Na swali muhimu zaidi, kama yupo mtu ambaye unajua ni mzuri au kile unachoulizwa kinamfaa, mwulize, umeshamwomba fulani?
Hili ni eneo la kwanza ambalo litamfanya mtu aache kukufikiria wewe tu na kufikiria wengine ambao wanaweza kumsaidia vizuri zaidi kuliko hata wewe.
Eneo la pili; kwa nini ni haraka?
Mara nyingi watu wanapokuja kwako na maombi, watakuambia wanahitaji msaada wako haraka. Na ndiyo maana watakuwa wanategemea useme ndiyo haraka. Sasa wewe chimba ndani na ujue haraka ni ya nini.
Uliza haraka hiyo ni kiasi gani, yaani inahitajika kuwa imekamilika mpaka kufikia lini? Uliza pia itachukua muda gani kufanya mpaka kukamilisha?
Muhimu zaidi uliza kama unaweza kufanya kwa sehemu tu, sehemu ipi ni muhimu zaidi?
Maswali haya, yatafanya anayekuomba afikiri zaidi kuhusu ombi lake, kwa sababu wengi huja na mapendekezo ambayo hata wao binafsi hawajayafikiria kwa kina.
Eneo la tatu; ipi picha kubwa?
Hapa unamwuliza yule anayekutaka wewe umsaidie, ipi picha kubwa, yapi maono yake baada ya kuwa umekamilisha kufanya? Pia mkumbushe vipaumbele vyako, na mwambie aangalie je ukiacha kufanya unachofanya, na kufanya kile anachotaka yeye ufanye, picha kubwa itakuwaje?
Hili ni eneo muhimu kuuliza, hasa kwa wale ambao wameajiriwa, kwa sababu inamkumbusha aliyekuajiri kuangalia matokeo yote. Mara nyingi wanajisahau na kukupa majukumu mengi ambayo siyo muhimu, na yangefaa kufanywa na wengine, huku wakikosa yale makubwa zaidi ambayo ungeweza kufanya.
SOMA; Waliokuambia Hapana…
Matokeo ya zoezi hili yanaweza kuwa kama ifuatavyo;
- Mtu atakujibu maswali yako yote na wewe utakuwa na furaha kusema NDIYO. Lakini hii ni mara chache sana kutokea mtu kukujibu maswali hayo yote na kwa usahihi.
- Mtu atakuambia asante kwa maswali mazuri, acha nikafikirie halafu nitakuja na majibu, na mara chache sana watarudi na majibu. Wengi wataondoka moja kwa moja na hutawaona tena wakirudi.
- Mtu anaweza kuachana na wewe na akaenda kumwulia mwingine atakayesema NDIYO haraka, ataona kama wewe unampotezea muda zaidi.
- Unaweza kuambiwa achana na hayo maswali na fanya kile nilichokuambia ufanye, hasa pale ambapo umeajiriwa, na hapo huna budi bali kufanya.
Kwa vyovyote vile, kutumia njia hii kutawafanya watu wajipande wanapokuja kwako. Hata kama utalazimika kufanya mara ya kwanza, wakati mwingine mtu anapokuja kukuomba ufanye kitu, atakuwa amejipanga kweli na atakuletea kile ambacho ni muhimu kweli na wewe tu ndiye unayeweza kufanya. Hivyo nakusihi jaribu njia hii mara kwa mara na kwa kila mtu. Itakuwezesha kununua uhuru wako na kusema HAPANA bila kumuumiza yeyote.
Wakati najifunza njia hii niliwahi kuitumia kwa ndugu yangu wa karibu, ambaye alikuwa kila akipata shida kidogo tu anawasiliana na mimi na kuhitaji nimsaidie fedha. Na mimi nikawa nafanya hivyo. Hii ilipelekea shida kuongezeka zaidi na maombi kuwa mengi. Siku moja alipoleta maombi yake niliandaa maswali muhimu ya kumwuliza. Nilitaka kujua hatua zipi ameshachukua kabla hajawasiliana na mimi, nilimtaka anipe matumizi yake ya fedha kwa kawaida, na tukachambua kila anachofanya. Tuliangalia lile tatizo pia na kuona njia nyingine angeweza kutumia kulitatua. Tulipofika mwisho, nilimpa kiasi ya kile alichoomba, lakini tangu siku ile, akija na shida, inakuwa shida kweli. Nafikiri labda ameweza kupata suluhisho, au amepata mtu mwingine anayemkubalia kiurahisi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Asante Kocha neno HAPANA linamana kubwa sana na Msaada mkubwa sana hata Mimi nina ndugu yang upo hi vyo
Lakni hapa nimejifunza Sana jinsi ya kusema HAPANA Japo najua itaniletea changamoto lakini inabidi nifanya hivyo
LikeLike
Ni kweli kabisa,
Hakuna jambo ambalo halina changamoto, Kusema NDIYO wakati ndani hutaki kuna changamoto pia.
Hivyo ni vyema mtu ukachagua aina ya changamoto unayoweza kuivumilia.
LikeLike
Ila sijajua ni jinsi tunavyojiweka kwa hawa ndugu na watu wengine wa karibu unapokua suala la fedha kwa nini mara nyingi aje kwangu tuu na shida hiyo hiyo mara kwa mara?
Unapotumia ndiyo nyingi unakaribisha matatizo mengi kwako kwa baadae wakishakuzoea
LikeLike
Kabisa,
Na wenyewe huwa wanajua, fulani huwa hakatai au hahoji, hivyo wakiwa na changamoto, hawatachukua hata muda kufikiria wanaitatuaje, wanajua kimbilio lao lilipo.
Ndiyo maana ni muhimu sana kutumia hapana na kuhoji mno kabla hujafika kwenye ndiyo.
LikeLike