Habari za leo rafiki,

Karibu kwenye makala yetu ya NYEUSI NA NYEUPE ambapo tunakwenda kuuangalia ukweli kama ulivyo. Kipaumbele cha kwanza kwa binadamu siyo ukweli, na hii ni kwa sababu ukweli unaumiza, ukweli haubembelezi. Hivyo hapa kwenye nyeusi na nyeupe, nimekuwa nakupa ukweli kama ulivyo, japo unakuumiza lakini sijali hilo, kwa sababu nataka wote tuuangalie ukweli kama ulivyo, japo unatisha.

 

Leo tunakwenda kuangalia baadhi ya mambo ambayo kila mtu siku hizi anafanya, ambayo hayana afya kwa kila mtu mmoja mmoja na hata jamii na taifa kwa ujumla.

Tangu iwe rahisi kwa watu kumiliki simu zenye uwezo mkubwa ‘smartphone’ na tangu mitandao ya kijamii iwe sehemu ya maisha yetu ya kila siku mambo yamebadilika sana. Siku hizi kila mtu anajua kila kitu na anaweza kufanya atakavyo, hakuna wa kumpangia kipi cha kufanya. Na watu wana kiburi na kujivuna kabisa kwamba simu nimenunua mwenyewe, bando nimeweka mwenyewe, usinipangie cha kupost.

Ni kweli kwamba hakuna mtu anapaswa kumpangia mwingine chochote cha kupost. Lakini kwenye kila jambo ambalo tunafanya, kuna mipaka. Wanasema uhuru bila mipaka unakuwa siyo uhuru tena bali ni uhuni. Kwamba kila mtu ana haki, lakini haki yako haipaswi kuingilia haki ya mwingine. Lakini tangu mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku, hayo yamekuwa hayana maana tena.

Siku hizi kila mtu ni mwandishi wa habari, anaweza kuripoti chochote kwa namna anavyojisikia yeye. Kila mtu ni mchambuzi wa kila kitu, anachambua siasa, michezo, mahusiano, kilimo, ufugaji na kila kitu anachojisikia. Hapo bado ushauri na ukosoaji wa mambo mbalimbali yanayokuwa yametokea. Siku hizi ni kama kumekuwa na mashindano ya kupost, kwamba nani alikuwa wa kwanza kutoa taarifa au kutuma picha za jambo fulani ambalo limetokea. Hasa linapokuwa jambo kubwa la kusisimua na kutisha kama ajali ambayo inapelekea mauti kwa watu wengi. Tumekuwa tunakazana kutuma picha za watu waliofariki kwa ajali, bila hata kuzingatia maadili katika kufanya hivyo. Wengi tumekuwa tunafanya hivyo tukiona tunawapasha wengine habari, kumbe tunafanya hatari kubwa ambayo siyo nzuri kwa kila mtu.

SOMA; Kwa Nini Habari Hasi Zinavuma Na Kupendwa Sana Na Wengi, Na Jinsi Ya Kujitoa Kwenye Mkumbo Huo.

Kwenye haraka hii hii ya kutaka kuonekana wa kwanza kuripoti kitu fulani, watu wamekuwa wakisambaza habari za uongo, ambazo hata hawajazidhibitisha. Kwa kuwa mtu kaona tu mahali, basi na yeye anatuma pengine. Watu wamekuwa wanasambaza hofu ambayo hata haipo, kuzua taharuki isiyo na maana na kufanya watu washindwe kufanya mambo yao kwa utulivu.

Hii ni hali ambayo ni changamoto kubwa sana kwenye jamii zetu, hasa kwa watu wengi ambao ndiyo wameijua mitandao na hawana elimu ya kutosha kuhusu mitandao. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu kwa sababu hata serikali, pamoja na kuweka sheria kali, inaonekana kushindwa kuwa na njia bora ya kuwawezesha watu kutumia mitandao vizuri. 

Kwa kuwa hii ni kazi ngumu, kauli nyingi tunazosikia kutoka kwa viongozi wa serikali ni kutaka kuzimwa au kuondolewa kwa mitandao hii, kitu ambacho bado hakitakuwa na manufaa, na hakitadumu kwenye dunia hii inayokwenda kwa mabadiliko ya kasi.

Je ni hatua zipi za kuchukua ili kuondokana na hali hii?

Zipo hatua tunazoweza kuchukua sisi binafsi, na kwa wengine ili kuhakikisha tunaepuka matumizi haya mabaya ya mitandao ya kijamii. Haya hapa ni yale baadhi muhimu zaidi.

1. Tujizuie kuendeshwa na mitandao hii ya kijamii.

Mitandao ya kijamii ina uteja fulani, kuanzia kwenye kuitembelea, kila wakati unataka utembelee ili usipitwe na yanayoendelea. Na unapoingia kwenye mitandao hii wanakuuliza unafikiria nini, tuambie hapa. Haraka sana unajikuta unaandika pale chochote ambacho unafikiria, hata kama siyo cha maana.

Tunahitaji kuondoka kwenye mtego huu, tusiwe watumwa wa mitandao ya kijamii, badala yake sisi tuitumie kufanya yale ambayo ni ya muhimu kwetu. Siyo lazima uwepo kwenye mitandao hii kila wakati, kufanya hivyo ni kupoteza muda wako.

2. Muda wa kazi zima mitandao ya kijamii.

Ndiyo, izime kabisa, zima data au bando kama wengi wanavyosema. Unapopanga muda wako wa kufanya kazi, zima kabisa mitandao ya kijamii. Na hata uwe na msukumo mkubwa kiasi gani ndani yako wa kutaka kuwasha na kuona nini kinaendelea, usifanye hivyo. Wewe chapa kazi na tenga muda baada ya kazi kuangalia ili ujue nini kinaendelea.

SOMA; Kitabu Muhimu Sana Kwako Kusoma Katika Kipindi Hichi Cha Habari Zisizo Na Mwisho.

Lakini kama wewe unafanya kazi, huku kila baada ya dakika 10 unachungulia nini kinaendelea, utakutana na habari ambazo zitakufanya ushindwe kuendelea na kazi yako, na wakati huo huwezi kufanya lolote. Kwa mfano, majuzi imetokea ajali ya watoto wa shule, muda mchache baada ya ajali ile, picha zilianza kusambaa kwa kasi sana. Sasa tuseme wewe upo kazini, ni saa tano asubuhi na unafanya kazi. Ukasema wacha niangalie mtandaoni kuna nini, ukakutana na picha zile za kutisha za watoto waliofariki kwenye ajali, hutaweza kurudi kwenye kazi yako tena kwa utulivu. Badala yake utataka uendelee kuwa kwenye mtandao, ujue nini kinaendelea, je wapo waliofariki zaidi, je hatua gani zinachukuliwa, je yupo unayemfahamu na kadhalika. Sasa kuanzia saa tano mpaka muda wako wa kazi unaisha, nakuhakikishia, hutaweza tena kufanya kazi yenye maana. Cha kusikitisha sasa, kuzipata kwako taarifa hizo mapema, hakujabadili chochote. Hakuna hatua yoyote ya haraka unayoweza kuchukua pale ulipo, hasa pale ambapo hakuna hata mmoja ambaye ni ndugu yako wa karibu amepatwa na matatizo kama hayo. Lakini kama ungekuwa umezima data na kufanya kazi, ungemaliza kazi yako vizuri na baadaye ungeweza kupata taarifa iliyokamilika kwa muda mfupi, badala ya kutumia siku nzima kufuatilia.

3. Kama kitu hujadhibitisha wewe mwenyewe, usisambaze, wacha mamlaka husika zitoe taarifa sahihi.

Moto kwenye mitandao ya kijamii huwa unachochewa na wale wanaosambaza. Mtu anapokea taarifa au habari na yeye anaisoma, inamsisimua na haraka sana anaisambaza kwa wengine. Hachukui hata dakika chache kutafakari iwapo habari hiyo ni ya kweli, na ina usahihi kiasi gani. Yeye anakimbilia kusambaza akiamini kuna jambo muhimu analofanya, lenye msaada kwenye jamii, kumbe anaharibu kabisa.

Kuepuka hili, taarifa au habari yoyote unayopokea, usikimbilie kuisambaza. Hutaiokoa dunia kwa kusambaza habari fulani, acha kujidanganya. Wewe kaa na subiri na wenye mamlaka watatoa habari kamili, kama ni kweli au la. Na kama utakuwa umezima mtandao na kufanya kazi yako, wala hutapatwa na hicho kiherehere cha kusambaza, maana utakuja kukuta habari kamili imeshapatikana.

4. Hata kama umeshuhudia jambo, kama huna uelewa wa kutosha, usikimbilie kusambaza.

Unaweza ukashuhudia kabisa jambo linatokea, lakini bado kusambaza kwako kukawa siyo sahihi. Hivyo kama huna uelewa, ni vyema kusubiri wenye uelewa au mamlaka kufanya kazi yao. Labda upo kwenye ajali na watu wameumia na kufariki. Unaweza tu kutoa taarifa ya ajali, lakini kutuma picha za majeruhi au waliofariki isiwe jukumu lako. Kwa sababu unaweza kutuma picha za kila aina, na kupelekea wengine kuzisambaza na zisiwe na msaada kwa wengine.

5. Maoni yako hayahitajiki kila mahali, wala hakuna anayeyajali.

Siku hizi kwenye kila jambo linalotokea, kila mtu ana maoni yake. Hata wasio na uelewa wowote nao wana maoni, ambayo yanaendeshwa na hisia tu wala siyo kitu kingine. Hivyo kwenye mambo yanayotokea, usikimbilie kutoa maoni yako, bali jiulize ni lazima na mimi nitoe maoni? Ni lazima na mimi niseme kitu? Je ninachosema kinaongeza thamani yoyote, yupo atakayejali. Ukijiuliza maswali haya utagundua maoni yako hayahitajiki kama unavyofikiri, hivyo utakaa kimya na kujifunza.

Kwa hiyo rafiki yangu, ni jukumu langu mimi na wewe, kwanza kuhakikisha sisi wenyewe hatuendeshwi na mitandao ya kijamii na pia kuwazuia wengine kutuendesha sisi kupitia mitandao hii ya kijamii. Tuitawale mitandao hii na kuitumia kwa manufaa na siyo kupoteza muda na kusambaza hofu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.