Hongera rafiki kwa siku hii nzuri ya leo.

Nina imani umeimaliza siku yako ya leo vizuri, ukiwa na mengi ambayo umekamilisha na kujifunza pia.
Nikupe hongera kwa hilo.

img-20161217-wa0002

Nachukua nafasi hii kukukaribisha kwenye #GHAHAWA ya leo ambapo tunaendelea kuangalia namna tunavyofanya makosa kwenye kufikiri kwetu. Makosa haya ya kufikiri yanatufanya kufanya maamuzi mabovu ambayo yanatugharimu.

Leo tutaangalia namna gharama tulizoingia zinavyotuzuia kufikiri kwa makini na kufanya maamuzi mabovu.

💥Je umewahi kulipia kitu, lakini ukagundua hakina manufaa kwako, ila ukaendelea nacho kwa sababu tu umeshalipia?
💥Umeshawahi kukubaliana na mtu kitu, baadaye ukagundua makubaliano hayo hayana tena manufaa lakini ukaendelea nayo kwa sababu tu ulishafanya makubaliano hayo?
💥Je umewahi kuweka muda wako kwenye kufanya kitu, ukaja kugundua hakina tena manufaa kwako hata kama utaendelea, lakini ukaendelea kufanya kwa sababu tu umeshakifanya kwa muda mrefu?

Kama umejibu ndiyo kwenye swali lolote hapo, au hali inayofanana na hiyo, basi umeingia kwenye mtego unaitwa SUNK COST FALLACY.
Mtego huu ni pale unapoendelea kufanya kitu, kwa sababu tu umeshawekeza fedha, muda, nguvu na hata mapenzi yako.
Zile sababu za kufanya za awali hazipo tena, ila unaendelea kwa sababu tu umeshawekeza wana mpaka hapo.

Ni sawa na kubaki kuacha kushuka kwenye basi ambalo limebadili mwelekeo kwa sababu tu umeshalipa nauli 😄😄😄
Ni jambo la kushangaza lakini tunafanya hivyo kila siku…
Kwenye kazi zetu,
Kwenye biashara zetu,
Kwenye mahusiano yetu,
Kwenye vitu tunavyonunua.

Kuondokana na mtego huu, tunahitaji kufikiri kwa kina kwenye kila jambo tunalofanya. Tuone kama bado ile sababu ya kufanya ipo, au tunafanya tu kwa sababu tumeshaweka fedha, muda au nguvu zetu nyingi.
Kama kitu hakina maana tena, achana nacho mara moja, bila ya kujali tumeshagharamia kiasi gani. Kuendelea kukaa kwa sababu ya gharama tuliyoweka, tunaendelea kupoteza zaidi.

Nakutakia maandalizi mazuri ya siku yako ya kesho,
Ipangilie vyema leo kabla hujalala.

Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz