Nafikiri kula biskuti ni moja ya vitu rahisi sana hapa duniani. Kwa sababu hata kama huwezi kutafuna, ukiweka mdomoni kwa muda tu italainishwa na mate na unachofanya ni kumeza tu. Hapo bado hujazungumzia utamu wake mdomoni ambao hauchoshi.

Leo nilikuwa nafikiri kama yupo mtu ambaye analipwa kwa kula biskuti. Yaani unaajiriwa mahali, na kazi yako ni kula biskuti, na mshahara unapewa. Rahisi kabisa na utamu mwanzo mwisho. Au unafungua biashara ambapo wewe unachofanya ni kula biskuti, na wateja wanakulipa.

Sijui kama unanipata tunapoelekea hapa, kwa sababu nataka uone mwenyewe ni namna gani unaweza kuwa unachekesha au kujidanganya pale ambapo unatamani kazi yako ingekuwa rahisi, isingekuwa na changamoto. Au pale unaposema nataka biashara ambayo ina faida kubwa kwa muda mfupi, isiyoniumiza kichwa.

Na jibu langu nitakuambia, nenda kale biskuti. Kwa sababu ndiyo kitu pekee rahisi kufanya na chenye utamu. Huhitaji nguvu ya ziada kufanya hivyo na utamu unaupata hapo hapo, ila tu, hakuna mtu yeyote duniani atakulipa kwa kufanya hivyo.

Vitu vyote halisi kwenye maisha, unahitaji kuweka kazi, unahitaji kuwa mvumilivu, utakutana na uchungu na utapoteza. Na kwa namna hiyo ndiyo unatengeneza thamani kwa wengine, na wao wanakuwa tayari kukulipa wewe.

SOMA; Kazi Na Ajira…

Unaajiriwa kufanya vitu ambavyo ni vigumu, kutatua matatizo ambayo yamewashinda watu na kuboresha zaidi kile kinachofanyika.

Unaanzisha biashara kutatua changamoto za watu, au kuwapatia mahitaji yao, kitu ambacho hakitakuwa mteremko tu.

Jiandae pale unapoingia kwenye shughuli yoyote ya kukuingizia kipato, haitakuwa rahisi na mambo hayataenda kama unavyotaka wewe mwenyewe.

Lakini kama utasisitiza kwamba unachotaka wewe ni urahisi, hutaki shida kabisa, basi cha kufanya ni hiki, chukua biskuti na weka mdomoni, bila hata ya kutafuna, italainika na utamu utaupata. Halafu jiulize, nani yupo tayari kukulipa kwa hicho ulichofanya?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog