Huwa najifunza mambo mengi sana kupitia watu ambao wanakuja kwangu wakiomba ushauri juu ya changamoto mbalimbali ambazo wanapitia kwenye kazi zao, biashara zao na maisha kwa ujumla. Na ili kuweza kuwashauri vizuri hatua zipi wachukue, huwa napenda kujua ni hatua gani wameshachukua mpaka pale walipofikia sasa. Kwa sababu kukimbilia tu kumshauri mtu kwa sababu ameshakuambia changamoto yake, haina msaada wowote.
Ninachojifunza kila siku ni kwamba kinachowazuia watu siyo ile changamoto ambayo wanayo, bali yale wanayofanya kuondokana na changamoto hiyo. Hayo ndiyo sumu kubwa sana, kwa sababu hayawasaidii kwa njia yoyote ile. Sasa hilo ndiyo linawaumiza watu zaidi, kwa sababu kadiri wanakazana kuondokana na changamoto hiyo, ndiyo wanazidi kudidimia. Sawa na mtu anayekimbia kwenye mchanga, kadiri anakazana kukimbia ndivyo anavyozidi kudidimia.
Uongo ambao nimekuwa nausikia kwa wengi ni huu; NIMESHAJARIBU KILA KITU, LAKINI SIPATI MATOKEO MAZURI. Ukikimbilia kushauri utaanza kwa kumwonea huruma sana, kwamba kila kitu amejaribu lakini bado yupo kwenye changamoto. Hapo unaweza kusema changamoto yake ni ya kipekee sana, na wengi huamini hivyo. Mtu yeyote mwenye matatizo, huamini matatizo yake ni makubwa kuliko ya mtu mwingine yeyote, ndiyo maana ni vigumu sana hata kwa mtu anayewashauri wenzake kwenye jambo hilo hilo hawezi kijishauri mwenyewe, kwa sababu anaamini hali yake ni tofauti. Kila mtu anaona tatizo lake ni ‘special case’.
SOMA; Sisi Ni Bora Kuliko Wao, Uongo Tunaojidanganya Mara Zote Na Kuharibu Mahusiano Yetu Ya Kijamii.
Tukirudi kwenye uongo huu maarufu, unapochimba ndani zaidi, unachogundua ni hichi, kila watu wanakuambia wameshajaribu kila kitu lakini hawapati matokeo mazuri, kumbe wamejaribu kile wanachojua wao, na hawajawahi kufikiria nje ya kile wanachojua wao. Na hapo ndipo wanapokwama kwa sababu kadiri wanakazana kuondokana na changamoto ndivyo wanazidi kuzama.
Sawa na mtu mmoja ambaye alikuwa na changamoto ya madeni ambayo hayaishi, amekazana sana kuondokana nayo lakini ameshindwa. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo wadeni wake wanavyozidi kumsumbua mpaka anakosa raha ya maisha. Tukaanza kuchimba hicho anachosema kafanya kila kitu ni kipi. Tulichoona sasa, anakwenda kukopa sehemu tofauti, kuja kuwalipa wale ambao wanamdai, hapo anatengeneza madeni zaidi. Anajaribu kupangilia mshahara wake wa sasa kulipa madeni, lakini bado haumtoshelezi. Anawaomba wanaomdai wamvumilie kwa muda, lakini haichukui muda wanaanza tena kumsumbua. Swali likawa moja, je umewahi kufikiria kutafuta njia nyingine ya kukutengenezea kipato kwa ajili ya kulipa madeni aliyonayo? Jibu likawa ni kujaribu biashara nayo ikashindwa. Lakini baadaye tukagundua alikuwa anajaribu kufanya yale yale aliyozoea kufanya. Palikuwa na mengi sana ambayo hajayafanya, ikiwepo kuangalia namna anaweza kulipwa zaidi kwenye kazi anayofanya sasa, kuangalia uwezekano wa kupata kazi ya muda ambayo itamwongezea kipato cha kulipa madeni hayo. Kuanza biashara ambayo ataweza kuisimamia vizuri kwa muda wake, maana aliyojaribu ilishindwa kwa kukosa usimamizi. Na mengine mengi ambayo hatuwezi kumaliza kuyaorodhesha hapa.
Hadithi zipo nyingi hasa za kukosa mtaji wa kuanzisha biashara, wengi watakuambia wameshafanya kila kitu lakini hawajapata mtaji wa kuanza. Na unashangaa inawezekanaje mtu amefanya kila kitu kweli akose pa kuanzia? Kweli mtu huyu alishajaribu kutembea na bidhaa nyumba kwa nyumba kutafuta wateja akashindwa? Unachokuja kugundua ni kwamba mtu alitaka mtaji apewe na ndugu au akopeshwe na benki, njia hizo zikishindikana basi anatangaza amefanya kila kitu na imeshindikana.
Ninachotaka kukukumbusha leo rafiki yangu ni hichi, pale unapokuwa kwenye changamoto, na ukaona kama huwezi kuondoka tena hapo ulipo, likishakuja tu wazo kwamba umeshajaribu kila kitu lakini imeshindikana, hapo hapo chukua karatasi na kalamu, kisha andika njia zote unazoweza kufikiri za kuondokana na changamoto hiyo. Andika kila kitu kinachokuja kwenye akili yako, hata kama siyo halali kufanya, wewe ruhusu akili yako imwage mawazo yote unayoweza kuwa nayo juu ya changamoto yako. Andika mpaka uwe hakuna unachofikiria tena juu ya changamoto hiyo. Orodhesha kila kitu. Jaza kurasa nyingi uwezavyo.
SOMA; Maadui Wakubwa Wawili (02) Wa Furaha Kwenye Maisha Yetu.
Baada ya hapo, anza kupitia kila ulichoandika, jiulize kwanza ni halali au siyo halali kufanya. Kile ambacho ni halali kiweke kwenye orodha nyingine mpya. Ambacho siyo halali jiulize kama kingekuwa halali ungekifanyaje. Kwa mfano kama changamoto yako ni mtaji wa kuanzia, na moja ya njia ulizoandika za kupata mtaji ni kumwibia mtu fedha, hii siyo njia halali. Sasa kwenye kujiuliza kama ingekuwa halali ungefanyaje? Na hapo unaweza kupata wazo kama kwenda kumwomba yule ambaye umekuwa unafikiria umwibie fedha. Nenda hivyo kwa kila wazo.
Ukishakuwa na orodha ya mawazo halali yote, anza kupitia wazo moja moja, angalia faida na hasara zake, angalia urahisi na ugumu wake, na angalia wapi unapoweza kuanzia na wazo hilo. Kila wazo lichambue kwa vigezo hivyo mpaka umalize mawazo yote. Ukifika mwisho, angalia ni mawazo yapi yanafanana na yakusanye pamoja. Kisha yape mawazo yako namba, kuanzia namba moja mpaka mwisho. Na huo ndiyo utakuwa mtiririko wako wa kujaribu mawazo hayo mapya. Unajaribu kila wazo na kutokukubali kurudi nyuma mpaka utoke kwenye ile changamoto.
Zoezi hili litakuhitaji sana kufikiri tofauti na ulivyozoea kufikiri. Litakutaka utoke nje ya mambo uliyozoea. Litakufanya ufanye vitu ambavyo siyo vya hadhi yako, kwa namna yoyote ile ulivyojishawishi hadhi yako ni ipi. Zoezi hili litakufanya uonekane wa tofauti kabisa, na wakati mwingine watu waone umepotea. Lakini wewe ndiye unayejua vizuri unataka nini na unakwenda wapi. Hivyo endelea kwenda na usikubali kwa namna yoyote ile kurudi nyuma.
Anza kufanyia kazi hili kwenye changamoto yoyote inayokusumbua kwa muda mrefu. Iwe ni biashara ambayo haiendi vizuri, kazi ambayo umekwama, madeni ambayo yanakusumbua, mahusiano ambayo hayaendi vizuri au kipato ambacho hakikutoshelezi.
Ninachomaliza nacho kukukumbusha ni kwamba tatizo lolote ambalo unalo sasa, hakuna namna yoyote litaondoka lenyewe kimiujiza, bali litaondoka baada ya wewe kuchukua hatua. Hivyo chukua hatua sasa kuhakikisha unabadili hali ya mambo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Kocha umeeleza kwa undani sana na kwakweli leo umenifundisha kitu kikubwa sana! Yaani hapa nilipo nimeanza kwa kuorodhesha changamoto zote ambazo zinanisumbua katika nyanja zote (kama eneo la kifedha, eneo la biashara, kazi, mahusiano, familia n.k) ……… Kinachofata baada ya hapa ni kuorodhesha nn cha kufanya kwenye kila changamoto!
Nimefarijika mno kusoma hii makala leo
Asante sana na Mungu akubariki
LikeLike
Vizuri sana kwa hatua hiyo uliyochukua.
Kila la kheri.
LikeLike