Habari za jioni rafiki?
Hongera kwa siku hii njema uliyokuwa nayo leo?
Je ni ushindi gani umepeta leo?
Yapi umejifunza leo?


Haya ni maswali mawili ya kujibu ili kuimaliza leo vizuri.

Karibu kwenye #GHAHAWA yetu jioni ya leo, tushirikishane yale machache muhimu ya kutuwezesha kufikiri kwa makini, na kutoruhusu hisia zetu kuingilia fikra zetu.

Moja ya njia ambazo watu wanaotaka kupata kitu wanafanya, ni kutoa zawadi za bure. Dhehebu la Hare Krishna limekuwa likitumia sana njia hii. Wamekuwa wakikaa kwenye viwanja vya ndege, mmoja anakufuata na kukupa zawadi ya ua, ukikataa anakusisitizia hii ni zawadi yako. Ukipokea na kusogea mbele kidogo anajitokeza mwingine na kukuomba mchango, mara nyingi mtu anajikuta akitoa, bila hata ya kujiuliza kwa nini anatoa.

Hili limekuwa linatumika na wafanyabiashara, wanakupa kitu fulani cha bure, halafu unajikuta unanunua zaidi.
Nimewahi kulishuhudia hili siku za nyuma kidogo, tulikuwa na ndugu na jamaa, tukafika sehemu ya bar, yule mwenye bar akawa anajuana na mmoja kati ya wale ndugu, mwenye bar akasema wape hao wote vinywaji, tulikuwa zaidi ya watano. Nikajiuliza huyu atapataje faida? Ninachokumbuka niliondoka nikiwaacha watu wanaendelea kuagiza, zaidi na zaidi..😄😄

Hili pia linatumika na wanasiasa wakati wa uchaguzi, inapokaribia kupiga kura, wanawapa wananchi fedha, hata kama ni kiasi kidogo sana. Sasa mtu anapofika kwenye boksi la kura, akiona picha ya yule aliyempa fedha, roho inamuuma na kujikuta anampigia kura (sahau sana kuhusu kula kwa fulani kura kwa fulani, wengi wanapeleka kura walikokula, unahitaji nguvu kubwa sana kushinda hiyo saikolojia).

Njia bora ya kuondokana na hili, ni kutokukubali zawadi ya bure. Kama hutaki kuishia kulipa gharama ambazo hukupanga, basi mtu anapokupa zawadi ya bure, kataa, kwa sababu utajikuta unalazimika kulipa kwa gharama ambazo huna au hukuwa umepanga.

Nikutakie wakati mwema rafiki.
Kocha Makirita Amani,

http://www.makirita.info