Kama unazalisha bidhaa zako mwenyewe, au unaandaa huduma zako mwenyewe, kupanga bei ni eneo muhimu sana. Tofauti na wale wanaochuuza, yaani kununua kwa jumla na kuuza kwa reja reja, wao wanakuwa na wigo wa bei tayari umeandaliwa. Lakini wewe unayeandaa mwenyewe, unahitaji kuwa makini wakati unapanga bei.

Unaweza kuweka bei kubwa ukitaka kupata faida kubwa na ukaishia kukosa wateja wa kununua bidhaa au huduma zako. Pia unaweza kuweka bei ndogo kuwavutia wateja wengi, ukajikuta unatumia rasilimali nyingi na faida ni kidogo au hakuna faida kabisa.

Unaweza pia kuanza na bei kubwa na ukaja kupunguza na watu wakakosa imani na wewe, hasa wale walionunua mwanzo wakati bei ipo juu. Au kuanza na bei ndogo na kuja kuongeza na watu wakaona una tamaa ya kupata faida kubwa.

Hivyo swala la bei, siyo rahisi kama wengi wamekuwa wanafikiri. Huamki tu na kusema bei ni hii, ukijaribu hivyo utapata shida baadaye na kupoteza imani na wateja wako na hatimaye kuwapoteza kabisa.

Hivyo leo tunakwenda kujifunza mambo matano muhimu ya kuzingatia pale unapopanga bei ya bidhaa au huduma unazoandaa wewe mwenyewe. Iwe ni vitu unazalisha, kama vyakula, mavazi, vitabu au huduma unatoa kama za ushauri, elimu, malazi na kadhalika.

Yafuatayo ni mambo muhimu ambayo unapaswa kuyazingatia unapopanga bei.

  1. Wajue washindani wako kwenye soko wanatoa nini na kwa bei gani.

Hata kama biashara unaibuni mpya, wapo watu ambao wanatoa kile ambacho unatoa wewe pia. Hawa ni washindani wako, hata kama hushindani nao moja kwa moja, kwani wateja wako wanavutiwa kwenda kwao pia.

Hivyo wakati unapanga bei, unahitaji kufanya utafiti na kuwajua vizuri washindani wako. Jua ni vitu gani hasa wanavitoa, ubora wa bidhaa au huduma zao na bei wanayouza wewe.

Ukishapata taarifa hizi, una hatua mbili za kuchukua;

Ama uweke ubora zaidi ya wao, uweke vitu vingi zaidi na uuze kwa bei sawa na wao au kubwa zaidi, lakini hapa unahakikisha mteja ananufaika kweli.

Au utoe ubora kama wanaotoa wao, ila uuze kwa bei rahisi. Uwape wateja kile kile ila kwa bei ndogo zaidi ya washindani wako.

Katika hayo mawili, nakushauri ufanye la kwanza, toa thamani zaidi, na utapata wateja wengi zaidi na wanaonufaika. Ukitumia njia ya kupunguza bei, washindani wako nao wanaweza kupunguza na wote mkaumia.

SOMA; Usipunguze Bei, Ongeza Thamani…

  1. Kama utaweka bei kubwa, jiandae kutoa makubwa pia.

Mteja anapoona bidhaa au huduma mbili zinazofanana lakini moja ni bei juu na nyingine ni bei chini, moja kwa moja anachukulia ile ya bai juu itakuwa na vitu vya ziada kuliko ile ya bei chini. Hivyo kama unataka kuweka bei juu kwenye bidhaa au huduma zako, jiandae kuweka thamani kubwa sana. Hakikisha unafikia matarajio ya mteja wako na hata kuyapita kabisa.

Kwa bei ghali utawavutia wateja wachache wanaojali kweli kile unachofanya na wanaokielewa na ambao utawahudumia vizuri na biashara kwenda vizuri.

  1. Kama utaweka bei ndogo, jiandae kushawishi zaidi.

Kama tulivyoona kwenye namba mbili hapo juu, ukiweka bei ndogo, watu wanapata picha kwamba ubora nao utakuwa mdogo. Hivyo unaweza kuwavutia wengi, lakini wakawa siyo watu wanaojali sana kile unachofanya. kwa sababu wanaojali, huwa wanachagua chenye ubora na huanza kupima ubora kwa bei ya kitu.

Hivyo kama unalenga kuweka bei ndogo uwavutie wengi, jua utawakosa wanaojali zaidi na hivyo unahitaji ushawishi mkubwa kuwapata wateja ambao utadumu nao kwa muda mrefu. Toa huduma bora sana kiasi kwamba mteja atapenda kurudi yeye mwenyewe. Usiweke bei ndogo na ubora wa hovyo, utajiumiza mwenyewe.

  1. Tengeneza uhaba wa kile unachotoa.

Sheria ya uchumi ni kwamba, kadiri kitu kinavyopatikana kwa urahisi, watu hawakithamini sana na bei yake inakuwa ndogo. Kikemia, chuma ni bora kuliko dhahabu, lakini kiuchumi thamani ya dhahabu ni kubwa kuliko chuma, kwa sababu ni vigumu kuipata dhahabu ukilinganisha na kuipata chuma, chuma inapatikana kwa wingi kuliko dhahabu. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara yako, kama unafanya kitu ambacho mteja anaweza kupata popote anapoenda, hakuna atakayekuwa tayari kulipa bei kubwa kupata unachotoa.

Hivyo ni jukumu lako wewe mfanyabiashara kutoa vitu adimu kabisa, ambavyo mteja hawezi kupata kwingine ila kwako tu, na hapo atakuwa tayari kulipa bei unayopanga wewe. Hata kama bidhaa ni ile ile, ila ambatanisha huduma bora kabisa ambayo inapatikana kwako tu.

SOMA; Gharama Ya Bei Unazoweka Kwenye Biashara Yako…

  1. Tengeneza jina la biashara yako.

Zipo biashara ambazo zinauza bidhaa zake ghali, kwa sababu tu ya jina, na hamna kingine. Kinachotokea ni kwamba watu wanakuwa wanaliamini sana jina na hivyo kuwa tayari kufanya biashara na mtu au kampuni hiyo. Hii ni kutokana na sifa ambayo biashara hiyo inakuwa imejijengea, kwenye uaminifu, ubora wa bidhaa na huduma na kadhalika.

Hivyo ni jukumu lako wewe mfanyabiashara kujenga jina la biashara yako, chagua sifa ambazo unataka wateja wazifikirie wanaposikia jina la biashara yako. Mwanzoni hutakuwa na wateja wengi, lakini kadiri unavyokwenda, kwa kusimamia misingi yako ya kibiashara, na kutoa thamani kwa wengine, kwa uaminifu mkubwa, jina litajengeka na baada ya hapo haitakuwa tena kazi kubwa kwako kuwashawishi watu wanunue. Wakisikia tu jina lako, wanajihakikishia wapo mahali salama na kuwa tayari kulipa bei unayokuwa umepanga. Zingatia usije kutumia jina lako vibaya, maana kujenga jina itakuchukua miaka 10, lakini kulibomoa ni dakika moja tu.

Zingatia mambo haya matano katika kupanga bei ya bidhaa au huduma unazotoa. Mwanzoni itakuwa vigumu lakini kadiri unavyokwenda, utaona inakuwa rahisi, hasa ukishajenga jina na kujua thamani ipi kubwa unatoa kwa wengine. Jitahidi kupanga bei ambazo utaenda nazo wakati wote, epuka kupunguza na kuongeza bei mara kwa mara, wateja wanaweza kupoteza imani na wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog