Hongera kwa siku hii nzuri ya leo rafiki.
Umeshinda mengi na kujifunza mengi siku ya leo.
Hakikisha unakwenda kuyafanyia yale uliyojifunza ili uweze kuwa bora zaidi.

Karibu kwenye #GHAHAWA ☕ ☕ jioni ya leo, tuchangamshe akili zetu kwa kutikisa fikra zetu kidogo. Yapo maamuzi mengi ambayo tumekuwa tunafanya bila ya kufikiri kwa kina.
Tafiti nyingi zinaonesha kwamba, watu tunaamini sana kile wanachoambiwa na mamlaka yoyote. Hawathubutu kuhoji na hilo huwapelekea kufanya makosa kwenye maamuzi yao, hasa pale mamlaka hizo zinapokuwa pia zimekosea.
Kwa mfano, unapokwenda hospitali kutibiwa, daktari anapokupima na kuchukua hatua, huwa unamuuliza kwa nini anachukua hatua fulani? Kwa mfano kama anakupa dawa, huwa unamhoji kwa nini amekupa dawa husika? Au kama kuna namna nyingine ya matibabu?
Wengi hawathubutu kufanya hivyo kwa kuogopa yale mamlaka aliyonayo daktari, ukiongeza hapo na koti jeupe, basi wanaamini watakuwa sahihi.
Lakini ukweli ni kwamba nao pia huwa wanakosea, na kuuliza kunaweza kumpelekea afikiri zaidi kuhusiana na hali yako.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa mamlaka nyingine zote, watu wanakubali haraka bila ya kuhoji au kufikiri kwa kina, na hivyo kufanya mambo wasiyoyaelewa.
Kwenye dini, sheria, siasa, uchumi na kadhalika, mara nyingi mamlaka zimekuwa zinafanya maamuzi yanayowaangusha wengi wasiofikiri au kuhoji.
Chochote unachofanya, jiulize ni kwa sababu umefikiri kwa kina na kukielewa au kuna mamlaka inakupelekea kufanya hivyo?
Uwe na wakati mwema.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
http://www.makirita.info