Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi nzuri sana ya siku hii ya leo katika maisha yako kwani leo ni siku bora na ya kipekee sana katika maisha yako. Hivyo basi, unaalikwa kutumia vizuri muda wako ili uweze kuvuna matunda mazuri unayotarajia kwenda kuyapanda asubuhi ya leo.

 

Mpendwa msomaji, nipende kutumia nafasi hii kuweza kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja mambo mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Hivyo basi, nakusihi sana tuweze kusafiri kimawazo wote kwa pamoja hadi pale nukta ya mwisho ya somo letu la leo. Katika somo letu la leo ninakwenda kukushirikisha somo lenye kichwa cha habari kinachosema bidhaa isiyoshuka thamani sokoni, je ungependa kujua ni bidhaa gani hiyo? Karibu sana ndugu msomaji tuweze kujifunza.

Huenda umekuwa na shauku sana kutaka kujua ni bidhaa gani hiyo isiyoshuka thamani sokoni ili uweze kuchangamkia fursa, bidhaa ambayo tokea watu waanze kuishi hapa duniani basi yenyewe haijawahi kushuka thamani. Watu wengi wanaogopa kuinunua bidhaa hii na kutumia majumbani mwao kwa sababu ya kuogopa gharama yake kwani yenye huwa haishuki hata siku moja sokoni. Kama tunavyojua kuwa katika uchumi bidhaa inayopatikana kirahisi huwa haina thamani, sasa bidhaa yenyewe huwa haitikiswi na kitu chochote hata kama uchumi ukiyumba.

SOMA; Mambo Yanayokuzuia Kupata Furaha Ya Kweli Maishani Mwako.

Rafiki, watu wengi walioweza kuishi karne za zamani waliweza kupigania sana bidhaa hii adimu isishuke thamani lakini watu wengi wanaopenda kutumia bidhaa hii huwa wanachukiwa katika jamii yoyote ile. Watu wanaosimamia kutumia bidhaa hii huwa wanaonekana ni watu wa ajabu na hata kuchukiwa. Wengine wanapoteza mpaka uhai wao kwa sababu ya kutetea kutoshuka kwa bidhaa hii. Hii bidhaa huwa inapingwa na viongozi mbalimbali wasiopenda kujali maslahi ya taifa lao lakini pia waliokosa uzalendo wa dhati.

Mpendwa msomaji, bidhaa isiyoshuka thamani sokoni ni bidhaa gani hiyo? Bidhaa yenyewe ninayozungumzia hapa nayo ni UKWELI. Ukweli ni moja ya bidhaa ambayo huwa haishuki thamani sokoni tokea Mungu aumbe dunia yake basi, nafikiri ukweli ndiyo bidhaa iliyoweza kusimama bila kushuka thamani mpaka leo. Ukweli huwa unachukiwa na watu wengi kwa sababu huwa haubembelezi mtu wala kujali huyu ni mtu mwenye cheo, wadhifa gani katika jamii yake. Kila siku wanaibuka wapinzani wengi kuwapinga wale wote wanaosimamia ukweli katika sehemu yoyote ile.

Ndugu msomaji, ukweli ni kama sheria ya asili hata ukisema ufiche ukweli lakini habari njema ni kwamba ukweli haufichiki hata siku moja. Ukweli ni mtetezi wa watu wote hapa duniani licha ya kupingwa na watu wengi wanaopinga ukweli. Ukweli ni bidhaa inayoogopwa kununuliwa na watu wengi kwa sababu ni ghali ukilinganisha na uongo, watu waliozoea kutumia bidhaa isiyokuwa na thamani kama kudanganya, kulaghai n.k kamwe hawawezi kuinunua hii bidhaa na kutumia katika maisha yao ya kawaida.

SOMA; Kama Unafikiri Vitu Hivi Ndivyo Vitakupa Furaha Ya Kweli Katika Maisha Yako, Unajidanganya Mwenyewe.

Hivyo basi, tunaona wazi katika dunia ya sasa watu walivyochoshwa na kudanganywa na wanasiasa hili tumeliona katika mataifa mbalimbali kabisa jinsi mambo yanavyokwenda ndivyo sivyo katika uchanguzi. Kwa mfano, Donald Trump katika kampeni zake yeye aliweza kusimamia bidhaa hii na kuiuza kwa watu na kweli watu wakainunua wakaona ni ya thamani. Watu wengi kwa sasa wanaendelea kuamka hivyo kama ukiendelea kusimamia na kutumia bidhaa hii basi utakuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako.

Ukweli ni uaminifu, uadilifu, nidhamu binafsi kwani kama mtu akiwa mwandilifu ni lazima basi atasimamia ukweli. Dunia ya sasa watu wamechoshwa na uongo, watu wanataka kusikia ukweli hivyo ni fursa kwako kuweza kuitumia kwa karni ya sasa kwani ukianza kuiuza utapata faida ila ukae tayari kupingwa na kuonekana adui kwa wapinzani wako wanaoupinga ukweli.

Hatua ya kuchukua leo, ukitaka kupata watu sahihi katika maisha yako basi anza kuuza bidhaa hii ya ukweli, usihangaike kumbembeleza mtu anunue ukweli kwani ukweli huwa unajiuza mwenyewe hata ukiuficha chumbani huwa unajiuza. Anza kutumia bidhaa hii ya ukweli katika maisha yako kwani ndiyo bidhaa isiyoshuka thamani na usiogope kupata wapinzani wanaokupinga kwa sababu ya kusimamia ukweli.

Mwisho, ukweli ndiyo bidhaa isiyoshuka thamani katika maisha yako hata katika falsafa na vitabu vya dini vinaweka wazi hili kwa kusema kweli itakuwa huru. Kwahiyo, tunaalikwa kutumia ukweli ili ituweke huru katika maisha yetu kwani bila ukweli tunakuwa watumwa.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza kila siku. Asante sana.