Jarida la Forbes limejizolea umaarufu kwa utaratibu wake wa kutoa orodha ya mabilionea wa dunia kila mwaka. Mwaka huu 2017 limetoa orodha ya mabilionea ambapo kwa sasa wapo mabilionea 2,043 ambapo ni ongezeko la asilimia 13 kutoka idadi ya mabilionea mwaka 2016 ambao walikuwa 1,810. Utajiri wa mabilionea hao kwa pamoja ni dola za kimarekani trilioni 7.67. Katika orodha ya mwaka huu, kumekuwepo na mabilionea wapya 195.
Kwa mwaka huu 2017 Afrika kuna mabilionea 25 ikiwa ni ongezeko la mmoja kutoka 24 wa mwaka 2016. Mohammed Dewji wa Tanzania ndiye bilionea mdogo zaidi kutoka Afrika akiwa na utajiri unaokadiriwa na Forbes dola za kimarekani bilioni 1.09 billion. Wapo wanawake wawili mabilionea kwenye bara la Africa ambao ni Isabel dos Santos kutoka Angola na Folorunsho Alakija wa Nigeria. Namba moja bado inashikiliwa na Aliko Dangote wa Nigerian ambaye utajiri wake unakadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni $12.2. vyanzo vya utajiri wake ni biashara ya sementi, unga, sukari na chumvi.
Huu ni mwaka wa 31 kwa forbes kutoa orodha hii tangu mwaka 1987 ambapo ndiyo walianza zoezi hili.
Haya hapa ni mambo 31 niliyojifunza baada ya kupitia orodha yao inayopatikana kwenye tovuti ya Forbes.
- Mwaka 1987 palikuwa na mabilionea 140 duniani na utajiri wao kwa pamoja ulikuwa dola bilioni 295. Kati ya hao ni mabilionea 20 pekee ambao wameweza kuwepo kwenye kila orodha kila mwaka.
SOMO; Kwenye utajiri kuna kupanda na kushuka.
- 1988 mabilionea 191 walikuwepo kwenye orodha, jumla ya utajiri dola bilioni 338. Wauza madawa wakubwa wa Colombia wakiongozwa na Pablo Escober waliingia kwenye orodha.
SOMO; Njia zisizo halali zinaweza kukuletea utajiri, ila hautadumu maana wote waliishia vibaya.
SOMA; Zipo Fedha Za Kutosha Kila Mtu Kuwa Bilionea…
- Mwaka 1989 palikuwepo na mabilionea 198, jumla ya utajiri wao dola bilioni 435.
- Mwaka 1990 palikuwa na mabilionea 269 wakiwa na jumla ya utajiri wa dola bilioni 542. Mwaka huo, Donald Trump aliondoka kwenye orodha ya mabilionea baada ya kuwepo kwa miaka miwili. Alifilisika kwenye biashara zake.
- Mwaka 1991 kulikuwa na mabilionea 273 wakiwa na utajiri wa dola bilioni 582. Mfanyabiashara kutoka Mexico Carlos Helu aliingia kwenye orodha hii kwa mara ya kwanza, miaka 19 baadaye akawa tajiri namba moja duniani.
- Mwaka 1992, mabilionea 288 jumla ya utajiri dola bilioni 602, mmoja wa mabilionea Sam Walton mwanzilishi wa Wal-Mart alifariki. Warithi wa biashara hiyo kwa sasa wana utajiri wa dola bilioni 118.6
- Mwaka 1993, mabilionea 310 jumla ya utajiri dola bilioni 565. Mexico pekee inaingiza idadi ya mabilionea 13.
- Mwaka 1994, mabilionea 349, jumla ya utajiri dola bilioni 762. Mwafrika wa kwanza kaburu kutoka Afrika kusini anaingia kwenye orodha, ni Harry Oppenheimer, mfanyabiashara wa dhahabu na almasi.
- Mwaka 1995, mabilionea 365, jumla ya utajiri dola bilioni 892. Bill Gates kwa mara ya kwanza ndiyo anakuwa mtu tajiri kuliko wote duniani, kabla ya hapo namba moja wote walikuwa wajapani.
- Mwaka 1996, mabilionea 447, jumla ya utajiri dola trilioni 1.1. mabilionea wengi wa miaka ya 1980 wanaondoka kwenye orodha, mwaka huo mabilionea wa kijapani walikuwa 41, sasa wapo 33.
- Mwaka 1997, mabilionea 486, jumla ya utajiri dola trilioni 1.2. mabilionea wa kwanza kutoka urusi wanaingia kwenye orodha, mwaka huo walikuwa wanne, mwaka huu wapo 96.
- Mwaka 1998, mabilionea 454, jumla ya utajiri dola trilioni 1.1. mabilionea kutoka Asia wanapungua kutokana na mdororo wa fedha na mafua ya ndege.
- Mwaka 1999,mabilionea 465, jumla ya utajiri dola bilioni 819. Bilionea mpya anaingia kwenye orodha, Ty Warner kwa faida ya biashara ya midoli ya watoto.
- Mwaka 2000, mabilionea 470, jumla ya utajiri dola bilioni 898. Hisa za kampuni ya Oracle zinapanda thamani kwa asilimia 500 na kumfanya mmiliki kuwa tajiri namba mbili duniani akiwa na utajiri wa bilioni 47.
- Mwaka 2001,mabilionea 538, jumla ya utajiri dola trilioni 1.8. Mmiliki wa televisheni ya BET anakuwa mmarekani mweusi wa kwanza kuingia kwenye orodha. Mwaka 2009 anaondoka kwenye orodha ya mabilionea.
- Mwaka 2002, mabilionea 497, jumla ya utajiri dola trilioni 1.5. Mabilionea 83 wanaondoka kwenye orodha baada ya anguko la biashara ya mtandao, lililojulikana kama DOT-COM CRASH.
- Mwaka 2003, mabilionea 476, jumla ya utajiri dola trilioni 1.3. Oprah Winfrey anakuwa mwanamke wa kwanza mmarekani mweusi kuingia kwenye orodha hii.
- Mwaka 2004, mabilionea 587, jumla ya utajiri dola trilioni 1.9. Waanzilishi wa google, Sergey Brin na Larry Page wanaingia kwenye orodha hii, wakiwa na miaka chini ya 30.
- Mwaka 2005, mabilionea 691, jumla ya utajiri dola trilioni 2.2. Martha Stewart anaingia kwenye orodha mwezi mmoja baada ya kutoka jela alipofungwa miezi mitano.
- Mwaka 2006, mabilionea 793, jumla ya utajiri dola trilioni 2.6. Hind Hariri, mtoto wa kiongozi wa Lebanon aliyeuawa anaingia kwenye orodha akiwa na miaka 22.
- Mwaka 2007, mabilionea 946, jumla ya utajiri dola trilioni 3.5. Mjapani Yoshiaki Tsutsumi ambaye alikuwa namba moja wakati orodha hii inaanzishwa anaondoka kwenye orodha ya mabilionea.
- Mwaka 2008, mabilionea 1,125, jumla ya utajiri dola trilioni 4.4. Warren Buffett anampiku Bill Gates na kuwa mtu tajiri zaidi duniani.
- Mwaka 2009, mabilionea 793, jumla ya utajiri dola trilioni 2.4. Mdororo wa uchumi duniani unapunguza utajiri kwa dola trilioni 2, na asilimia 30 ya mabilionea wa mwaka uliopita wanaondoka kwenye orodha.
- Mwaka 2010, idadi ya mabilionea 1,011, jumla ya utajiri dola trilioni 3.6. Warren Buffett na Bill Gates wanatangaza kutoa sehemu kubwa ya utajiri wao kama msaada kwa wenye uhitaji.
- Mwaka 2011, mabilionea 1,210, jumla ya utajiri dola trilioni 4.5. Moscow inakuwa jiji la mabilionea, mabilionea 79 wanatokea Moscow, idadi kubwa zaidi kutokea kwenye jiji lolote.
- Mwaka 2012, mabilionea 1,226, jumla ya utajiri dola trilioni 4.6. Elon Musk anaingia kwenye orodha ya mabilionea, kupitia kampuni zake za magari ya umeme, nishati ya jua na safari za angani.
- Mwaka 2013, mabilionea 1,426, jumla ya utajiri dola trilioni 5.4. Isabel Dos Santos mtoto wa raisi wa Angola, anakuwa mwanamke tajiri zaidi Africa, akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.
- Mwaka 2014, mabilionea 1,645, jumla ya utajiri dola trilioni 6.4. Bilionea kutoka Brazili, Eike Batista anafilisika kutoka utajiri wa dola bilioni 30 mpaka dola milioni 300, baada ya kampuni yake ya mafuta kufilisika.
- Mwaka 2015, mabilionea 1,826, jumla ya utajiri dola trilioni 7.1. Mchezaji maarufu wa zamani Michael Jordan anaingia kwenye orodha akiwa na utajiri wa dola bilioni 1.
- Mwaka 2016, mabilionea 1,810, jumla ya utajiri dola trilioni 6.5. Bilionea wa kwanza kutokana na biashara ya ndege zisizo na rubani (drones) anatokea china.
- Mwaka 2017, mabilionea 2,043, jumla ya utajiri dola trilioni 7.7. Wanawake mabilionea wanachukua asilimia 2.7 ya mabilionea wote duniani, wakati muongo uliopita walikuwa chini ya asilimia 1.
Kama tulivyoona kwenye hiyo orodha ya miaka yote;
- Mabilionea wanatokea kwenye kila aina ya biashara, kuanzia kwenye uchuuzi, teknolojia, madini na kadhalika.
- Watu wamekuwa wanaingia na kutoka kwenye orodha hii.
- Orodha ya mabilionea na utajiri imekuwa inaongezeka kila mwaka kasoro kipindi ambacho kumekuwa na mdororo wa uchumi, kama anguko la dot com mwaka 2000, na mgogoro wa mwaka 2008. Hivyo tuna uhakika wa mabilionea kuendelea kuongezeka na utajiri wa dunia kuongezeka zaidi, na hii inatoa nafasi kwa kila mtu kuweza kuwa bilionea.
- Wakati mwingine utajiri wa watu unaongezeka au kupungua siyo kwa sababu zao bali kwa sababu za kiuchumi zinazoathiri dunia.
- Mabilionea wanatokea hata kwenye mataifa yanayoendeshwa kijamaa. Hii inaonesha kwamba kila sehemu ipo fursa ya kutajirika, hata kama uchumi umebanwa kiasi gani.
- Watu wanafikia ubilionea kwa miaka tofauti, wapo wanaoingia na miaka ishirini na, na wa po wanaoingia na umri mkubwa.
- Ukiacha wachache ambao wameingia kwenye orodha kwa biashara zisizo halali, wengi wameingia kwa biashara zenye manufaa kwa watu wengi.
Nimekushirikisha orodha hii rafiki, kukupa sababu ya kupigana zaidi ili kuweza kufanya makubwa kwako na kwa wengine pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Samahani kocha mimi nashindwa kujua vigezo gani wanatumia kujua utajiri hyo
Mfano mwenye biashara ya uchuuzi unakuta hela nyingi ipo kwenye mali
Naomba Ufafanuzi kocha
LikeLike
Habari Jilala,
Forbes wanaangalia vitu vingi, na wanatumia makampuni ya watu hao ambayo yanandaa hesabu zake za kila mwaka.
Pia wanaangalia maeneo ambayo mtu amewekeza. Mfano amenunua hisa za kampuni fulani, amenunua ardhi au anamiliki majengo.
Vyote hivyo wanavifuatilia kwa umakini na ndiyo wanakadiria utajiri.
Nakumbuka siku za nyuma kidogo, mwakilishi wa forbes Africa alikuwa anamlalamikia Reginald Mengi kwamba inakuwa vigumu kwao kumfuatilia. Landa kwa sababu vitu vyake vingi havipo wazi.
LikeLike