Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Umeianzaje siku hii njema na bora sana ya leo?
Ni imani yangu umeianza siku hii ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Hongera sana kwa hilo rafiki.
Ukumbuke msingi wetu muhimu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA maana msingi huu ndiyo utatuwezesha kufika tunakotaka kufika.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SELF-FULFILLING PROPHECY au UNABII WA KUJITENGENEZEA MWENYEWE….
Watu wengi wamekuwa wanatafuta manabii wa kuwatabiria maisha yako, na kusahau ya kwamba nabii mkubwa wa maisha yao ni wao wenyewe. Wewe mwenyewe, unajitengenezea unabii mkubwa sana wa maisha.
Unabii huu unaanza na mawazo yako, halafu unaenda kwenye matendo yako. Mwisho unaona matokeo ya unabii huo.
Hakuna unabii mkubwa na wenye nguvu kama ule ambao unajitengenezea mwenyewe. Unabii huu hauwezi kuvunjwa na yeyote, unakushika vizuri kabisa na hautoki mpaka uubadili mwenyewe.
Unabii huu unatokana na yale mawazo ambayo unayaruhusu yatawale akili yako.
Kama unaamini huwezi kuwa tajiri, na mawazo yako yote ni umasikini, ukiwaona matajiri unaona ni watu wabaya. Matajiri wakipata matatizo unafurahia. Tayari umejitengenezea unabii wako mwenyewe, na hata ufanye nini, huwezi kuwa tajiri.
Kama umeshajijengea kwamba wewe ni mtu wa kisirani, wewe ni mtu wa kukosa kila wakati, wa kuonea na kudhulumiwa. Nakuhakikishia, kwenye kika jambo utakutana na kisirani, kuonewa na kudhulumiwa.
Kila kitu ulichonacho kwenye maisha yako sasa, ukianza na furaha, matatizo, changamoto, kukwama na hata wanaokuzunguka, yote hayo ni matokeo ya utabiri wako mwenyewe.
Kadiri unavyoendelea kutabiri, kwa mawazo unayojipa na imani ulizojijengea, unazidi kuimaridha utabiri wako na kupata matokeo ya kile unachojitabiria.
Kwa kuwa kila kinachotokea kwenye maisha yako kinaanza na mawazo yako, kwa nini usiwe na mawazo mazuri. Kwa kuwa kila kitu kinaanza na unabii wako, kwa nini usiwe na unabii mzuri kwako wewe mwenyewe?
Badala ya kuwaza umasikini, waza utajiri.
Badala ya kuwaza kushindwa, waza ushindi.
Badala ya kuwaza maisha ya chini, waza maisha ya chini.
Badala ya kujiambia hili sitaweza, jiambie utaweza.
Badala ya kuchukulia kila hali kama mbaya kwako, chukulia kila hali kama nzuri au kama fursa.
UNAKUWA KILE UNACHOFIKIRI, hii ni falsafa ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na ni sahihi kabisa. Hapo ulipo umepatengeneza. Kama hupapendi, tengeneza pengine, tengeneza upya.
Uwe na siku njema sana rafiki yangu,
Ianze siku hii kwa kauli chanya ya kuianza siku. Na tengeneza utabiri mzuri wa siku yako.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info