Habari za leo rafiki?

Ni wakati mwingine mzuri ambao tunakutana hapa kwa ajili ya kushauriana juu ya changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye maisha yetu. Maisha yana kila aija ya changamoto, ukitatua moja inakuja nyingine. Na hivyo suluhisho siyo kukimbia changamoto, bali kuzitatua ili kukua zaidi.

 

Kwenye ushauri wa leo tunakwenda kugusia eneo la masoko kwa wale wanaofanya biashara ya mali, yaani ardhi na majengo. Hii ni biashara ambayo imekuwa na ukuaji mkubwa wa miaka ya hivi karibuni, wengi wameingia na kujikuta wakiwa na changamoto ya kupata wateja wa mali walizonazo. Leo tutakwenda kuangalia kwa kina namna gani mtu anaweza kupata wateja kwenye biashara hii.

Lakini kabla hatujaingia ndani na kujifunza zaidi, kwanza tusome maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ametuandikia akiomba ushauri kwenye hili;

Ninafanya Biashara ya Real estate, hasa ninapima viwanja na kuuza. Changamoto yangu ni Masoko nashindwa kuyafikia vizuri japo Nina viwanja sehemu mbalimbali za Dar na Pwani na Kwingineko. Matokeo muda mwingi Nina Mali (viwanja ) lakini Sina Cash money ya kuendesha Kampuni. Maselle N. M.

Kama alivyotuandikia rafiki yetu Maselle hapo, amejitahidi kufungua kampuni, na sasa changamoto ni masoko. Huenda mwanzo changamoto ilikuwa anawezaje kujiajiri, sasa ameweza na kugundua masoko hakuna.

Kwanza kabisa nikupongeze sana ndugu Maselle kwa kuweza kuchukua hatua ya kujiajiri kupitia biashara ya uuzaji wa mali, kama inavyojulikana kwa Kiingereza Real Estate. Ni fursa nzuri sana kwa wakati huu ambapo watu wengi wana mwamko wa kuwa na viwanja na nyumba maeneo ya mjini kwa ajili ya kazi au biashara.

Masoko au kama wengi wanavyoita kupata wateja, ni changamoto ya biashara nyingi. Hii imekuwa hivyo kwa sababu watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa mazoea, wanaingia kwenye biashara kwa sababu wameona watu wengine nao wanafanya biashara ile. Hawakai chini na kujipanga vizuri na kuwa na mkakati madhubuti wa uendeshaji wa biashara zao. Kwa kuwa wanaona wengine wanaendesha biashara, na wao wanaingia mpaka pale wanapojikuta kwenye changamoto ambazo hawakutegemea ndipo hugundua kuna vitu hawakujipanga.

Hapa nakwenda kukushirikisha njia unazoweza kutumia kufikia watu wengi na kupata wateja wa biashara yako ya uuzaji wa mali.

SOMA; KILIMO CHA NYANYA; Utunzaji Wa Shamba, Uvunaji Na Masoko Ya Nyanya.

1. Chagua soko lako utakalolielewa na kulifanyia kazi vizuri.

Mwulize mfanyabiashara yeyote mteja wako ni nani na atakuambia kila mtu. Hapo ndiyo utagundua mfanyabiashara huyo hayupo makini na biashara yake na hana wateja kabisa. 

Biashara ambayo kila mtu ni mteja siyo biashara, bali majaribio. Kila biashara ina wateja ambao inawalenga.

Kwenye biashara yako ya mali, kuna aina nyingi za wateja, kulingana na sifa zao, upatikanaji wao na uwezo wao. Unahitaji kuchagua wateja wapi unawalenga, ili uweze kuwahudumia vizuri.

Kwenye biashara hii ya mali, unaweza kuwagawa wateja kwa makundi mengi, lakini kwa kuanzia tumia vigezo hivi.

Kuna kundi la vijana ambao wameajiriwa na wanajipanga kuanza maisha yao. Hawa wanapenda kuwa na viwanja vyao na nyumba zao.

Kuna kundi jingine la vijana ambao hawajaajiriwa ila wana shughuli zao binafsi za kujiajiri au biashara, hawa nao pia wanapenda kuwa na viwanja na nyumba zao.

Lipo kundi la watu wazima, ambao wapo kwenye kazi au wanaelekea kustaafu. Pia wapo wenzao ambao hawajaajiriwa ila umri unakwenda na wanataka kuwa na mali zao.

Lipo kundi la wastaafu, ambao wamemaliza kazi zao na wakalipwa mafao yao. Hawa wapo ambao hawakufanya hayo mapema na wanataka kuyafanya kwa wakati huo.

Yapo pia makundi madogo madogo kama watu wanaotaka kufanya biashara kwenye mali.

Ni muhimu uchague kundi moja au machache ambayo utayalenga, kisha jipange kuwafanyia kazi.

Kwa nini ni muhimu uchague kundi?

Kwa sababu kwa kufanyia kazi kundi moja la watu, ni rahisi kujenga nao mahusiano mazuri. 

Kwa mfano kama umechagua kundi la wastaafu, ambao wamepokea mafao na kutafuta mali, unajipanga utawapata wapi, utajengaje nao mahusiano na unawezaje kuwasaidia kupata kile wanataka.

Kama umechagua kundi la vijana ambao ndiyo wanaanza kazi zao, unajua kabisa hawana uwezo mkubwa wa kulipa mara moja kununua viwanja au nyumba. Hivyo hawa unaweza kuwatengenezea mpango mzuri wa kulipa kwa awamu na wakajipatia mali wanazotaka.

2. Tengeneza jina lako kibiashara. (branding).

Kila biashara inategemea sana kwenye jina ambalo imejijengea, lakini kwenye biashara ya mali, hili ni muhimu zaidi. Jina linajenga uaminifu kwa watu na wanajisikia vizuri pale wanapofanya biashara na biashara yenye jina linaloaminika. Kununua kiwanja au nyumba siyo sawa na kununua nguo au gari, mtu anaogopa sana kukoseka kwani makosa hayo yanaweza kumgharimu muda mrefu.

Hivyo unahitaji kuwa na nembo yako ya biashara ambayo utaitumia vizuri, unahitaji kutengeneza kadi zako za kibiashara ambapo utawapa kila mteja unayekutana naye. Popote unapokuwa, hakikisha picha ya biashara yako inajijenga kwenye akili za watu. Hili linajenga aminifu na watu wanapokuwa na uhitaji wanakuja kwako.

3. Watumie wateja ambao tayari walishanunua kwako.

Hakuna mgodi wa dhahabu kwenye biashara kama wateja ambao tayari wameshanunua, halafu wakaridhishwa na manunuzi yao. Hawa ni wateja ambao unahitaji kuendelea kuwauzia zaidi na hata kuwatumia kupata wateja zaidi.

Hakikisha kila mteja anayenunua kwako una mawasiliano yake, kuwa na namba yake ya simu na email yake pia. Jua taarifa zake kwa ufupi pia, itakusaidia sana siku za baadaye.

Unapopata mali mpya, angalia katika wale wateja wako, wapi ambao mali ile inaweza kuwafaa zaidi. Wasiliana nao hao kuwaeleza mali mpya iliyopo na kuwakaribisha kuona.

Pia watumie wateja waliokwisha kununua kwako kupata wateja wengi zaidi. Watu hao wana ndugu jamaa na marafiki zao, waombe wakutambulishe kwa watu wao wa karibu ambao wanahitaji mali unazouza wewe pia. Njia ya kuambiwa au kushuhudiwa na mteja ina nguvu sana.

SOMA; Hivi Ndivyo Mawazo Hasi Yanavyoua Biashara Yako.

4. Tumia intaneti na mitandao ya kijamii.

Watu wengi wanaofanya biashara bado wanafanya kwenye ulimwengu wa zamani. 

Hawajaweza kutumia intaneti na mitandao ya kijamii kukuza zaidi biashara zao. Kila siku nimekuwa nasema kitu kimoja, kila biashara sasa hivi ni biashara inayohusu intaneti, kwa sababu karibu kila mtu yupo kwenye intaneti.

Kwa biashara ya mali, unahitaji kuwa na tovuti ambayo ina maelezo ya kampuni yako, huduma mnazotoa na hata mali zinazopatikana kwa wakati huo. Muhimu zaidi unahitaji kuwa na blogu, na kupitia blogu ndiyo utaweza kuwafikia wateja wengi zaidi. Sasa usitumie blog yako kimakosa kama wengi, kutangaza tu mali zilizopo. Badala yake toa elimu kuhusiana na mali unazouza kupitia blog yako. Andika makala zinazohusu viwanja, jinsi ya kuchagua kiwanja, taratibu za kisheria kwenye mali, kunufaika zaidi na mali ambazo mtu anazo na kadhalika. Wapo watu wenye shida za aina hiyo, wakifika kwenye blogu yako na kupata ufumbuzi watakuwa wanakufuatilia.

Kwenye mitandao ya kijamii, tengeneza akaunti za kibiashara, na huko pia usitumie tu kutangaza mali ulizonazo. Bali washirikishe watu taarifa na maarifa muhimu kuhusu biashara ya mali. Na mara moja moja wape watu matangazo ya mali zinazopatikana. Tumia mitandao ya kijamii kujenga mahusiano bora na wateja wako, ambao watakuamini na kununua kwako.

Muhimu sana; kama mpaka sasa huna akaunti za biashara yao kwenye mitandao ya kijamii, fungua. Kama mpaka sasa huna blog ya biashara yako, ambapo unaandika makala za kuwaelimisha watu kuhusu mambo mbalimbali ya biashara yako, anza leo hii, usisubiri siku iishe. Ukitaka msaada zaidi tuwasiliane kwa simu 0717396253.

5. Kuwa mtaalamu kwenye biashara unayofanya.

Usiishie tu kuwa mfanyabiashara wa viwanja na nyumba, badala yake kuwa mtaalamu. 

Maana yake jua kila kitu kinachohusiana na biashara yako. Mteja anapouliza swali lolote, hakikisha unalitafutia suluhisho au jibu kamili. Maswali na changamoto nyingi za wateja zinajirudia rudia, zijue kwa undani na jua unawezaje kuwasaidia.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii na intaneti, hasa kwenye blogu yako, unaweza kujitengeneza kama mtaalamu, na watu wanapokuwa na shida yoyote wanakutafuta wewe. 

Watu hawa wanakuamini na kuwa wateja wako.

6. Tafuta nafasi ya kuwa na makala kwenye magazeti.

Magazeti mengi yanatoa nafasi za watu kutoa maarifa ya utaalamu walionao. Unaweza kuandaa maarifa unayoweza kuwa unayatoa, na kuwasiliana na magazeti mbalimbali. Wewe utakuwa unawapa makala kila wiki na mwisho wa makala wanakupa nafasi ya kutaja biashara yako na mawasiliano yako. Ukiwa na magazeti mengi utaweza kuwafikia watu wengi. Muhimu ni kutoa maarifa ambayo watu hawapati sehemu nyingine.

7. Nenda sehemu ambazo wateja wako wanapatikana.

Ipo mikutano mbalimbali ya watu, ambayo kila mtu anaweza kuhudhuria. Yanaweza kuwa maonesho, mafunzo kama ya semina au mikutano ya kibiashara. Ukishajua wateja wako ni watu wa aina gani, mara kwa mara hudhuria kwenye mikutano ambayo wanahudhuria. 

Huko unaweza kukutana na wengi, kuwaeleza unafanya nini na kuwapa kadi zako za mawasiliano. Siyo wote watakutafuta, ila wenye uhitaji watakukumbuka, na watakutafuta.

Ongea na wale ambao wanaonesha nia ya kuwa na mali, au kujenga. Kisha chukua mawasiliano yao, kila unapokuwa na mali nzuri basi washirikishe.

8. Acha kutumia lugha ambazo watu hawazielewi unapotangaza biashara yako.

Watu wengi wanaofanya biashara ya mali, hasa kwenye viwanja, karibu wote utasikia nina viwanja sehemu fulani, mita moja ya mraba ni shilingi elfu tano. Nina uhakika, zaidi ya asilimia tisini ya watu wanaosikia hilo hata hawaelewi unamaanisha nini. Mita moja ya mraba ina ukubwa gani? Kiwanja kina mita ngapi za mraba? Hayo ni maswali unamwacha nayo mteja ambayo yanamkatisha tamaa.

Badala ya kutumia lugha hizo ambazo wengi hawakuelewi, wewe mwambie aina ya viwanja ulivyo navyo, labda vikubwa, vya kati na vidogo. Na ukiwaambia watu kwa miguu labda miguu ishiriki kwa ishirini wanakuelewa zaidi. Kisha wape bei kulingana na kiwanja, na siyo kwa mita za mraba. Hilo la mita za mraba liache kwenye mipango yako, unapoongea na wateja, wape taarifa za viwanja.

9. Rahisisha kiasi ambacho mteja anapaswa kulipa kupata mali.

Kwenye kutangaza biashara pia, wafanyabiashara wengi kwenye mali, hutaja bei kamili ya kitu. Labda kiwanja milioni 10, au nyumba milioni 50. Wengi wanaposikia fedha nyingi hivyo, hukata tamaa na kuona bado hawajajipanga.

Sasa wewe unahitaji kutengeneza mpango wa watu kulipia kwa awamu, na kulipia kidogo kidogo. Hapo unaweza kuwashawishi wengi.

Kwa mfano, kama una viwanja vya shilingi milioni kumi, na mtu anaweza kulipia kwa miaka miwili, kwa kulipa kila mwezi, miaka miwili ina miezi 24 ambapo mtu anaweza kulipa shilingi 416,700. Ikiwa kiwanja ni milioni tano, hiyo inakuwa 208,400.

Sasa hapo unaweza kumtangazia mteja wako pata kiwanja, eneo fulani kwa shilingi laki mbili kila mwezi. Kwa njia hiyo utapata wengi wa kuongea nao na mtatengeneza mpango mzuri. 

Nina uhakika umeshakaa na viwanja zaidi ya miaka miwili bila kuuza, vipi kama ungetengeneza mpango wa kulipwa kidogo kidogo?

10. Shirikiana na wadau muhimu.

Kwenye biashara ya mali, wapo wadau muhimu sana unaohitaji kushirikiana nao. Wadau hao watakuletea wewe wateja, na wewe utawapelekea wateja, ni nipe nikupe. Wadau hao ni kama ifuatavyo;

Mabenki. Mabenki ni wadau muhimu kwenye biashara ya mali. Mabenki yanatoa mikopo ya fedha na hata mali kwa watu. Tafuta mabenki unayoweza kushirikiana nao, wao wanapopata mtu anayetaka mkopo wa nyumba au kiwanja, wamuunganishe na wewe. Na wewe unapopata mteja anayetaka kiwanja na hana fedha, unamwunganisha na benki hizo. Kwa njia hii kila mtu ananufaika.

Makampuni ya ujenzi pia ni wadau muhimu. Kuna wakati wanapata wateja ambao wanataka nyumba lakini hawajajua eneo gani zuri. Unaweza kufanya nao kazi wakakuletea wateja wa aina hiyo. Pia wewe unapomuuzia mtu kiwanja na akawa na mpango wa kujenga, unaweza kumuunganisha na kampuni ya ujenzi unayoshirikiana nayo.

Haya ni baadhi ya mambo unayoweza kufanya na ukaongeza wateja kwenye biashara yako ya uuzaji wa mali. Fanyia kazi hayo na kama utahitaji msaada zaidi, karibu tufanye kazi pamoja. Tuwasiliane kwa 0717396253.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog