Rafiki,
Leo ni siku mpya ya wiki mpya.
Ni nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo makubwa.


Kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA makubwa sana yanaweza kufanyika kwenye maisha yetu. Ni sisi kuwa na msimamo kwenye haya na kuyaishi kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UNGRATEFUL PEOPLE au WATU WASIO NA SHUKRANI…
Je umewahi kumsaidia sana mtu, ukajitoa sana kwa ajili yake, lakini baadaye hakujali kabisa ulichofanya. Akasahau kabisa na kushindwa kukusaidia wewe ulipokuwa unahitaji?
Je umewahi kumfanyia mtu kitu ukitegemea ajali na kushukuru lakini hata hakuonesha kujali?
Je umewahi kufika mahali na kusema ama kweli SHUKRANI YA PUNDA NI MATEKE?

Huenda kwa namna moja au nyingine ulishajikuta kwenye hali hizo, na kuona namna gani watu hawana shukrani.
Ninachotaka tutafakari kwa kina ni hichi,
Je unapokuwa unamsaidia mtu, unafanya hivyo kwa sababu ni kitu sahihi kwako kufanya, au unafanya hivyo kwa sababu unataka uonekane, ushukuriwe na baadaye ulipwe?
Hapa ni sehemu nzuri sana ya kuanzia, ili kuepuka kuwalalamikia wengine.

Siku za karibuni umekula matunda, labda tuseme umekula maembe, je ulishakutana na mti wowote wa mwembe ukaushukuru? Kwa sababu jamii yake imeleta maembe na umeyafurahia.
Na hata kama una ng’ombe nyumbani, je umewahi kumsukuru kwa maziwa anayotoa? Vipi kuku wanaotaga mayai?

Unaweza kusema viumbe hawa hawastahili shukrani, kwa sababu hawana utambuzi, na hapo utakuwa unajidanganya.
Viumbe hao, wataendelea kufanya kile wanachofanya cha kukunufaisha, hata kama hutoi shukrani, kwa sababu kile ndiyo kitu sahihi kwao kufanya.

Hivyo basi, unapotoa msaada, au unapofanya jambo kwa ajili ya wengine, fanya kwa sababu ni kitu sahihi kwako kufanya. Usifanye kwa sababu unaonekana, au ufanye kwa sababu utapewa shukrani, wewe fanya. Wanaojali watashukuru, wasiojali wataendelea na maisha yao, na wewe endelea na maisha yako.

Wapo watu wengi wasiokuwa na shukrani, ikiwepo mimi na wewe kwenye maeneo kadhaa. Hivyo tusiumie wala kusumbuka sana pale tuliowasaidia wanaposahau tulichofanya.
Tufanye kilicho sahihi na maisha yaendelee.

Uwe na siku njema, uwe na wiki kubwa, ufanye makubwa sana.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info