Changamoto kubwa ya biashara nyingi kwenye mzunguko wa fedha ni madeni. Biashara unaanza vizuri, inakuwa na bidhaa na huduma zote, wateja wanaanza kukopa, wakiahidi kulipa wanapopata fedha zao. Lakini wateja wengi wanakuwa siyo waaminifu, wanapopata fedha hawalipi madeni, na mbaya zaidi wanahama biashara yako na kwenda sehemu nyingine. Hili limekuwa linawaathiri wafanyabiashara mara mbili, kwanza linawakosesha fedha wakati bidhaa wameshatoa, na pia linawapunguzia wateja.

Pamekuwepo na misemo mingi ya kibiashara kama mkopo umesafiri, au hapa cash tu na mingine, lakini hii imekuwa haisaidii, kuna wakati wafanyabiashara wanateleza na kujikuta wameshakopesha na hapo mambo yanaanza kwenda vibaya.

Najua hii ni changamoto nzito na hivyo leo nataka twende nayo taratibu sana, ili kila mfanyabiashara aweze kujenga msingi wa biashara yake na kuepuka kurudishwa nyuma na mikopo.

Inaanza na hofu ya usipokopesha hutapata wateja.

Nimekuwa nashauri watu wengi wanaokuja kwangu na changamoto hii, kwamba wamekopesha na sasa mali hawana na wateja wamehama. Kadiri tunavyojadili kwa kina naona hofu inayokuwa imeanza ndani yao. Hofu hiyo ni mfanyabiashara kuona kama hatokopesha basi hatapata wateja kwenye biashara yake. Kwa sababu kila mtu anakopesha, basi inamlazimu na yeye akopeshe.

Kingine ni ile hali ya kwamba wateja ni waaminifu kwako na siku moja tu wamepungukiwa. Na kuwa wateja wana mahusiano mazuri na biashara, unawakopesha, siku ya kwanza kidogo, wanalioa vizuri, wanakuja na hitaji jingine kubwa kidogo, unawapa, wanalipa. Wanakuja na hitaji kubwa zaidi, unawapa, na hapo wanashindwa kulipa na shida inaanza.

Unachopaswa kujua ni kwamba, wateja wanajenga mazoea kwa namna unavyoendesha biashara yako.

Ngoja nikuambie kitu, wateja wanakuelewa na kujenga mazoea kwa namna unavyoendesha biashara yako. Kwa mfano kama biashara huwa haikopeshi, wateja wanajua wazi na wanaambiana kwamba ukienda sehemu fulani hawakopeshi, hivyo nenda na fedha yako kamili au nenda sehemu nyingine. Ikiwa biashara yako inakopesha wateja watakuja na kila sababu ya kutaka kukopa. Na pia wataambiana kama unataka mkopo, nenda kwa mfanyabiashara fulani.

Kuwakopesha wateja siyo kuwabakiza kwenye biashara.

Hili liko wazi kabisa, unapokopesha, unawakimbiza wateja. Hata kama siyo wote, lakini unapunguza wateja, kwa sababu wapo ambao watakopa, na watashindwa kulipa, watahama na kwenda kununua sehemu nyingine.

Sasa wewe umewauzia kwa mkopo ukiamini kwamba usipowapa mkopo watakuhama, unawapa mkopo halafu wanakuhama. Hapo unakuwa umepata hasara mara mbili, umepoteza bidhaa ambazo hujalipwa, au utasumbuka mpaka ulipwe, na pia umepoteza mteja. Ni bora ungepoteza mteja tu kuliko kupoteza mteja na sehemu ya mtaji wako.

SOMA; Tabia Moja Itakayokuwezesha Kudhibiti Matumizi Ya Fedha Zako.

Hitimisho; usikopeshe.

Tengeneza msimamo wa biashara yako, hatukopeshi. Na hilo liwe ndiyo unalosimamia. Utatoa huduma kwa wateja ambao wanaweza kulipia fedha tasilimu. Jitahidi sana usivunje msimamo huu.

Unapokuwa unaanza biashara, au unakuza biashara yako, hili ni muhimu sana, maana wakati huu ukikopesha na mteja akakusumbua, anaiharibu sana biashara. Biashara ikishakuwa kubwa ndiyo linakuwa muhimu zaidi kwa sababu wateja wanapoanza kukusumbua wanakurudisha nyuma.

Hivyo usikopeshe.

Lakini nitakosa wateja.

Kabla hujasema utakosa wateja, je unawajua wateja wako? Je una wateja? Kwa sababu wateja wa biashara hawapaswi tu kuwa watu wanaokuja kununua na kuondoka, bali wanapaswa kuwa watu ambao ni mashabiki wa biashara yako. Watu ambao wanapenda kuona biashara yako inaendelea. Watu ambao wapo tayari kuisaidia biashara yako. Hao ndiyo wateja.

Sasa nirudi kwako, hao unaosema utawakosa, unao? Je unao watu ambao wananufaika sana na biashara yako kiasi cha kuwa tayari kuipigania iendelee kuwepo? Kama unao watu wa aina hii, wanapotaka kukopa basi waeleweshe, ya kwamba iwapo utaanza kukopesha, biashara itashindwa kwenda na utashindwa kuwahudumia tena vizuri. Wateja watakuelewa, na watakuwa tayari kwenda kukopa fedha sehemu nyingine, waje kununua.

Hivyo, tengeneza wateja wa biashara yako, ambao wataielewa nia yako njema ya kutokukopesha, na hao wengine, achana nao. Watalalamika na kutoa maneno mabaya kwako, lakini wataiacha biashara yako salama.

Lakini biashara kubwa zinakopesha, na hata serikali inakopa kwenye biashara.

Watu wengine wamekuwa wanafikiria kwa kuwa biashara kubwa zinakopesha, na taasisi au serikali inaweza kukopa kwenye biashara kubwa, kwa kuuziwa kwa tenda au mkataba na kuja kulipa baadaye, basi na wenye biashara ndogo na za kati nao wanapaswa kukopesha. Nirudie tu kusema ya kwamba, kama bado unakazana kukuza biashara yako, hasa unapokuwa mwenyewe au na wasaidizi wachache, na huwezi kuingia mkataba wa kisheria na unaowakopesha, usikopeshe. Utapoteza muda mwingi kufuatilia mikopo kuliko kuwapa wateja wako huduma bora kabisa.

Mfumo wangu wa biashara ni wa kukopesha.

Wapo watu ambao biashara yao ni kukopesha vitu au fedha na kulipwa kwa awamu au baada ya kipindi fulani. Hawa kukopesha ndiyo biashara yao, lakini pia wanahitaji kuwa na misingi, la sivyo biashara itawasumbua sana.

Msingi wa kwanza na muhimu kabisa, siyo kila mtu anayetaka kukopa ana haki ya kukopeshwa. Lazima viwepo vigezo vya kujiridhisha kwamba mtu huyo anaweza kulipa mkopo au  bidhaa anayokopa. Kwa maana hiyo ana kazi inayomwingizia kipato, na ushahidi upo, au ana biashara inayokwenda vizuri. Pia lazima awe na namna ya kuweza kulipa mkopo, iwapo itashindikana kulipa kwa kipato chake. Hivyo lazima aweke amana mali yenye thamani sana na mkopo anaoomba. Baada ya hapo sasa ndiyo anakopeshwa. Ukikimbilia kukopesha kwa sababu mtu anataka au ana shida sana, utakopesha watu wasio sahihi. Na mbaya zaidi wataenda kuwaambia wenzao kwamba ukienda sehemu fulani unaweza kupata mkopo kwa urahisi. Usisahau pia watu wanadanganya mara nyingi mno, hivyo kuwa makini, sana.

Hitimisho la mwisho.

Usikopeshe, tengeneza wateja wanaoijali sana biashara yako, ambao unawapa huduma bora kabisa na wao wenyewe watakuelewa ukiwaambia hukopeshi.

Kama biashara yako ni ya kukopesha, weka misingi na ifuate, usitoe mkopo kwa kila mtu na jihakikishie mkopo unaotoa unarudi.

Niishie hapo kwa upande wangu, karibu tujadiliane hapo chini, uliza au changia chochote, ili tuweze kujifunza zaidi juu ya hili la mikopo kwenye biashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog