Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Hii ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.


Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MAMBO HAYATAKUWA MAZURI YENYEWE….

Watu wanapokuwa wanapitia changamoto mbalimbali, hufika mahali na kufikiri ya kwamba mambo yatakuwa mazuri tu.
Watu hukaa na kufikiri kesho itakuwa bora kuliko leo.
Na hayo yote ni kweli kabisa, ila kama tu mtu atachukua hatua leo.
Mambo hayatakuwa mazuri yenyewe, mpaka pale mtu atakapochukua hatua.

Haijalishi unatamani kiasi gani mambo yawe mazuri, lakini lazima wewe mwenyewe uchukue hatua kwanza.
Ni kweli muda unaboresha mengi, lakini lazima juhudi ziwekwe kwanza.
Usikae tu na kufikiri mambo yatakuwa bora.
Hali ikiachwa kama ilivyo, bila ya kuchukua hatua yoyote ile, mambo yanazidi kuwa hovyo.

Hivyo rafiki, kwa lolote unalotaka liwe bora kwenye maisha yako, anza kuchukua hatua sasa, leo hii.
Hatua unazochukua leo ndiyo zinazotengeneza mambo bora zaidi kesho.

Ni hatua gani unachukua leo?

Uwe na siku bora rafiki yangu.

Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info