Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi nzuri sana ya siku hii ya leo katika maisha yako kwani leo ni siku bora na ya kipekee sana katika maisha yako. Hivyo basi, unaalikwa kutumia vizuri muda wako ili uweze kuvuna matunda mazuri unayotarajia kwenda kuyapanda asubuhi ya leo. 

 

Mpendwa msomaji, nipende kutumia nafasi hii kuweza kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja mambo mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Hivyo basi, nakusihi sana tuweze kusafiri kimawazo wote kwa pamoja hadi pale mwisho wa somo letu la leo. Katika somo letu la leo ninakwenda kukushirikisha somo lenye kichwa cha habari kinachosema sumu kali inayoua mahusiano ya ndoa na uchumba je ungependa kujua ni sumu gani hiyo? Karibu sana ndugu msomaji tuweze kujifunza wote kwa pamoja.

Maisha ya ndoa yanadai uaminifu mkubwa, kama tunavyojua uaminifu unalipa kila idara ya maisha yetu. Mahusiano yoyote yaliyokosa uaminifu ni kama meli iliyokosa nahodha hivyo ni rahisi kwenda mrama. Maisha ya ndoa yaliyokosa uaminifu huwa yanajenga vigango vingi nje ya ndoa au kwa lugha rahisi iliyoshika kasi kipindi hiki ‘’michepuko’’. Baadhi ya wanandoa waliokosa uaminifu wameamua kuhalalisha uongo kuwa ukweli, wakidai kuwa na mchepuke ni kitu cha kawaida.

SOMA; THE SCHOOL OF GREATNESS (Mwongozo Wa Kuwa Na Maisha Makubwa, Mapezi Ya Dhati Na Kuacha Jina.)

Mpendwa rafiki, sumu kali inayoua mahusiano ya ndoa na uchumba nayo ni kuanza kumfananisha mwenzi wako na mtu mwingine. Maisha ya mahusiano yanaanza kupoteza ladha pale unapoanza kumfananisha mwenzako na mtu mwingine. Kuongozwa na hisia ndiyo matokeo ya mambo yote haya, kama uliamua mwenyewe kuwa na huyo uliye naye sasa iweje tena uanze kumfananisha na mtu mwingine? Ulimchagua yeye kwa sababu ni wa pekee na kama isingekuwa wa pekee kwa nini uliamua kuwa naye?

Ni tabia ya ajabu na ni sumu kubwa kuanza kuhesabu vile ambavyo mwenzako hana na hapo ndiyo kuanza kuutafuta ubaya na kumuona mwenzako hana thamani na amepoteza ladha. 

Tabia ya kuhesabu mwenzi wako amekosa vitu fulani na kuweka orodha ya litania ndefu ni kumzika mwenzako wakati yuko hai. Hii tunaona watu wanavyoanza kuzikana yaani jinsi watu wanavyowatoa wenzi wao katika mioyo yao na hatimaye kuishi maisha ya ujane wakati wenzi wao bado wako hai. Kuhesabu mambo ambayo mwenzi wako amekosa ni sawa sawa na kumchunguza bata na kuhakikisha awe msafi muda wote.

Rafiki, kumfananisha mwenzi wako wa ndoa na mtu mwingine ni ile tabia ya kuanza kutothamini kile ambacho mwenzako anacho. Hii inasababishwa na kuwa na tamaa ya kuongozwa na hisia ya vitu. Unaangalia kwako hakuna nini na kuanza kufananisha na mtu mwingine. Mambo kama haya huwa ndiyo yanapelekea kuwa sumu katika mahusiano na hatimaye wenzi kuanza kupotezeana thamani au kupoteza ladha kwa mwenza wake. 

Ukishamwona mwenzako hana thamani ni sawa na chakula kilichokosa chumvi hivyo mara nyingi chakula kilichokosa chumvi kinakuwa hakina ladha ndivyo basi utakavyomwona na mwenzako wa ndoa au wa mahusiano ya uchumba.

Ukianza kutafuta ubaya kwa mwenzi wako huwezi kukosa, aliyekuwa raisi wa Marekani 

Abraham Lincoln aliwahi kunukuliwa akisema, kama ukitafuta ubaya kwa watu hakika huwezi kukosa, hivyo tarajia kuupata. Unaalikwa kumpenda mtu kulingana na mazuri yake lakini kama ukianza kutafuta amekosa nini hakika tarajia kupata hicho alichokosa. Ukitafuta ubaya kwa mtu yeyote yule hakika utaupata na huwezi kukosa kwani kila mtu ana madhaifu yake.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza kwenye kitabu cha The DNA of Relationships(Vinasaba Vya Mahusiano).

Hatua ya kuchukua leo, usimfananishe mwenzi wako na mtu mwingine na mchukulie yeye ni wa pekee sana kuliko wengine. usitafute ubaya kwa mwenzi wako kwani ukitafuta ubaya huwezi kuukosa hata siku moja. Mjali na mpende kama alivyo bila kuongozwa na hisia za vitu ambavyo mwenzi wako hana.

Mwisho, maisha ya ndoa yanadai uaminifu na upendo wa kweli na siyo upendo wa vipimo. 

Hivyo tunaalikwa kutowafananisha mwenzetu na watu wengine kwani unapoanza kumfananisha ndiyo sumu yenyewe itakayokwenda kupoteza ladha katika mahusiano yako ya ndoa na uchumba.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza kila siku. Asante sana.