Biashara rahisi kufanya, thamani yake ni ndogo, na biashara ngumu kufanya, thamani yake ni kubwa.

Kwa maneno mengine, biashara rahisi kufanya faida yake ni kidogo, na biashara ngumu kufanya faida yake ni kubwa.

Watu wengi wamekuwa wakikimbilia kutafuta biashara rahisi kufanya, biashara ambayo haitawapa stress, biashara ambayo wana uhakika wa kupata faida kwa haraka. Ukweli ni kwamba, biashara ya aina hiyo kabisa hakuna, na kama ipo inayokaribiana na hiyo, basi inafanywa na wengi. Si wengi wanataka urahisi!

Sasa biashara inapokuwa inafanywa na wengi, kinachotokea ni wanaofanya biashara hiyo kugawana wateja waliopo. Hivyo hata mtu aweke juhudi kubwa kiasi gani, ni kama kunakuwa na ukomo wa kipato, kwa sababu wateja mara nyingi wanakuwa ni wale wale.

Na kibaya zaidi, kwa kuwa watu wanatafuta urahisi, basi hakuna anayekwenda hatua ya ziada, badala yake wote wanafanya kile kile, na hivyo wateja kutokuona tofauti.

SOMA;  Kama Haiumizi, Haina Thamani…

Kwa upande wa pili, biashara ambazo ni ngumu kufanya, biashara ambazo zina hatari ya kupoteza, biashara ambazo hazina uhakika sana, zinafanywa na wachache, na hivyo wateja kuwepo wengi na wafanyabiashara kunufaika. Wale ambao wanajitoa kweli, na kuweka kazi ngumu inayohitajika, wanawavutia wateja na kutengeneza faida.

Hivyo mambo mawili ya kuondoka nayo hapa mfanyabiashara mwenzangu;

Usitafute biashara rahisi ya kufanya, bali tafuta biashara ambayo unaweza kuwa tofauti na kuwapa wateja kile wanachotaka, ambapo wengine hawapo tayari kufanya hivyo.

Mbili; kama upo kwenye biashara rahisi, au biashara ambayo inafanywa na wengi, angalia namna ya kujitofautisha. Angalia wateja wanataka nini, ambacho wafanyabiashara wengine hawapo tayari kutoa, kisha wewe toa kwa wateja wako. Kwa njia hii utaenda hatua ya ziada na utaweza kufanya makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog