Ni siku mpya ambayo tumebahatika kuiona tukiwa na hamasa kubwa kuhakikisha tunapambana kutimiza malengo yetu mbalimbali ambayo tumejiwekea, na lengo kuu ni kujikwamua dhidi ya umaskini wa kifikra na kiuchumi. Pamoja na hayo pia tuendelee kuwafariji marafiki wenzetu ambao wanapitia changamoto mbalimbali za kijamii na kiafya ambazo kwa namna tofauti zinawafanya wajisikie wapweke katika mapito yao. Kwetu sisi iwe ni chachu na fursa ya kuongeza juhudi katika kufikia uhuru wa kifedha kupitia maarifa mbalimbali tunayojifunza kupitia Makala hizi.

Mara nyingi ninapokutana na marafiki wanaohitaji ramani za majengo au ushauri pale wanapofikia hatua ya kutaka kuanza ujenzi, jambo la kwanza huwa ni kutaka kufika na kuona kiwanja kwa ajili ya vipimo mbalimbali vya kisanifu. Kwenye hatua hii ndipo huwa natambua vizuri changamoto zinazowakabili watanzania wengi kwa mambo yanayohusu viwanja. Wengi hawafahamu kusoma ramani za viwanja, jambo ambalo linawanyima haki ya kutambua fursa ambazo zitawaletea manufaa endapo wangetambua vema na kufanya uchaguzi wa viwanja mahali sahihi. Leo nitazungumzia mambo muhimu unayopaswa kuyazingatia wakati wa kuchagua kiwanja kwa ajili ya matumizi ya makazi au biashara

  1. MAHALI KILIPO KIWANJA


Katika safari hii ya mafanikio kila mmoja wetu ana ndoto yake anayotamani siku moja kumiliki nyumba ya aina fulani na mahali fulani iwe kweli kutokana na vigezo alivyojiwekea. Je mji gani unataka umiliki kiwanja, lengo la kumiliki kiwanja, vipi ukuaji wa mji huo hasa ongezeko la watu, je upo mahali sahihi katika kufikia lengo lako. Hili huwa ni jambo la kwanza kuzingatiwa kwa yeyote mwenye dhamira ya kweli, Ila changamoto kubwa huwa inakuja ni kwa jinsi gani unaiweza kuifanya ndoto hiyo kuwa kweli. Usiwe kama bendera fuata upepo au maji kufuata mkondo, popote utakaposikia umekimbilia. Ufahamu unapaswa utangulie mengine yafuate, kwa kufanya hivyo utakuwa unajihakikishia ushindi wa kufikia lengo kwa uhakika.

  1. UMBO LA KIWANJA


Umbo la kiwanja huathiri sana usanifu wa ramani na maamuzi yote yanayohusu ubora, ukubwa na mwonekano wa nyumba. Hakikisha unachagua kiwanja ambacho kina umbo linaloeleweka, unapaswa ujiulize kama mwanafunzi, je kiwanja unachotaka kununua kina umbo gani ambalo ukimwambia mwingine atakuelewa kirahisi kwa mwonekano wa mapana na marefu. Je kiwanja unachotaka kununua kitatosheleza mahitaji na matumizi ambayo unatarajia endapo utafanikiwa kukinunua. Je unahitaji kiwanja kilicho kwenye mlima, tambarale au kwenye mteremko. Mambo haya yatakusaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi ili kukidhi kiu yako ya kuwa na kiwanja ambacho kitakidhi malengo yako wakati na baada ya ujenzi. Kwa marafiki mnaochagua viwanja milimani mkumbuke kuwa kuna wakati utakuwa mzee, mgonjwa au watakuja wageni wa makundi maalumu kama vile watoto, wajawazito na walemavu. Ni vema mkakumbuka kuweka usalama na miundombinu rafiki baada ya ujenzi kukamilika ili kuepukana na hatari zisizojulikana.

  1. UWEPO WA HUDUMA ZA JAMII NA UCHUMI


Huduma za jamii na uchumi kama vile ofisi za serikali, viwanda, elimu, afya, maji, usafiri, huduma za fedha, maeneo ya michezo, burudani, nyumba za ibada, soko na mawasiliano ya simu na mitandao ya tovuti. Haya na mengine mengi yanapaswa kuzingatiwa sana wakati unakusudia kununua kiwanja mahali ulipokusudia. Mambo haya huainishwa kwenye ramani za viwanja, hivyo unapaswa kuuliza na kuelewa vizuri kuwa umezungukwa na viwanja vyenye matumizi ya aina gani. Na kama eneo lako halijapimwa ni vema ukawaona wataalamu wa mipango miji wa eneo husika, watakueleza eneo lako litakuwa limezungukwa na viwanja vyenye matumizi ya aina gani, usihofu wapo kwa ajili ya kukuhudumia wewe.

  1. ATHARI YA HALI YA HEWA


Uwezo wetu wa kiakili na kimwili umetofautiana katika kuhimili mazingira ya aina tofauti, athari za mvua, joto, baridi, upepo na matetemeko ya ardhi ni matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa. Hivyo kabla ya kununua unapaswa ujitathmini kuhusu hali ya hewa ya mahali hapo kama utaweza kuimudu. Ni muhimu sana ukachagua kiwanja kizuri kilichopo kwenye mazingira rafiki na salama. Epuka mazingira ya kushawishiwa na wengine ikiwa wewe utajitathmini na kutambua athari hasi dhidi yako.

  1. UWEPO WA MIUNDOMBINU


Miundombinu muhimu kama vile barabara, mawasiliano, nishati mbalimbali, mifumo ya maji safi na maji taka inapaswa izingatiwe katika hatua zote wakati wa kukagua maeneo ya viwanja utakapoenda. Miundombinu bora huweka mazingira katika hali ya usalama na huchochea maendeleo ya jamii na uchumi katika mji. Miundombinu bora huepusha mafuriko na hurahisisha usafirishaji na mawasiliano ya kijamii na kiuchumi. Tatizo lipo kwenye maeneo ambayo hayajapimwa, ni vigumu sana kuwepo kwa miundombinu rafiki ikiwa hakutakuwa na usimamizi wa mipango miji na vijiji, kila mmoja atajenga anavyojua yeye na uwezo wa kufikiri tumetofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine, mwisho wa siku yanageuka kuwa makazi hatarishi.

  1. MATUMIZI HALISI YA KIWANJA


Kila kipande cha ardhi kimepangwa matumizi yake, hivyo ni muhimu ukafahamu vema matumizi halisi ya kiwanja unachohitaji ili kiweze kukidhi malengo yako. Kwenye ramani ya mipango miji na vijiji kila kiwanja huandikwa matumizi yake kama vile makazi, biashara, shule, soko, michezo, mazishi, viwanda, nyumba za ibada, maeneo ya wazi, maeneo ya hifadhi, huduma za jamii na maeneo ya kitalii. Umakini unahitajika sana katika kufanya maamuzi yanayoendana na lengo lako. Na kama eneo lako halijapimwa ni vema ukawaelimisha wengine na mkafanya utaratibu wa kupimiwa. Kwa sasa wapo wataalamu na kampuni nyingi za upimaji viwanja, usisite kuwasiliana nao endapo utahitaji ushauri au msaada wowote, usisite kuwaona, wapo kwa kazi hiyo.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888


Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com