Hitaji kubwa sana la kila mwanadamu, ukishaondoa yale ya kuhakikisha anaendelea kuwa hai, basi ni kujaliwa na wengine, kuonekana wa thamani mbele ya wengine. Hichi ni kitu ambacho watu wanakipigania kweli. Yaani ukiwaangalia watu usoni ni kama wamejibandika ujumbe unaosema TAFADHALI NITHAMINI…. Watu wanapenda sana hilo.

Watu wanapothaminiwa, wanapoona wana mchango, huwa wanafurahi sana, na kufanya zaidi kile kinachowafanya wathaminiwe. Ukitaka kuona hilo, msifie mtu kwenye kitu. Msifie kwa uhakika, siyo kwa kutania, msifie kweli, atafurahi sana, na ataendelea kufanya lile ambalo amesifiwa kufanya.

Biashara yako inahitaji wateja, na siyo wateja wa kuja kununua tu mara moja, bali wateja wanaokuja mara kwa mara, na wanawaleta wateja wengine pia.

Moja ya njia za kuhakikisha wateja wanakuwa sehemu ya biashara ni kuwathamini, kuwafanya wajisikie wa kipekee, kuwafanya wafurahi. Ndiyo maana nasema kwamba, biashara yako ni kuwafurahisha watu. Pale watu wanapojisikia vizuri wanapokuwa kwenye biashara yako, wataendelea kuja.

SOMA;  Kipi Watu Hawataki Kufanya?

Pale watu wanapojibiwa vizuri kwa kile wanachouliza, wanafurahia kuwepo kwenye biashara yako.

Pale watu wanaposaidiwa kwa changamoto wanazokutana nazo zinazohusiana na biashara hiyo, wanajisikia vizuri.

Watu wanapojisikia vizuri na kufurahi, hawawezi kuficha furaha yao, na kinachotokea ni kutoa taarifa kwa wengi zaidi ili nao waje kufurahia.

Je biashara yako inawafanya wateja wako kufurahi na kutamani kuja tena?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog