Habari za leo rafiki yangu?

Mwezi huu wa saba wa mwaka huu 2017 nitaendesha semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA. Hii ni semina ambapo tutajifunza mambo ya msingi kabisa kuhusu fedha, ambayo hatujawahi kufundishwa popote pale, siyo shuleni wala nyumbani. Katika maandalizi ya semina hii, ambayo nitakupa taarifa zaidi mwishoni mwa makala hii, nilitoa nafasi kwa wasomaji wote kuniandikia ni mambo gani wangependa kujifunza kwenye semina hii.Nimepokea maoni mengi sana kutoka kwa wasomaji kuhusu mambo ambayo wangependa kujifunza kwenye semina hii. Mambo mazuri kabisa kuanzia kutengeneza fedha, kuongeza kipato, kuweka akiba, kuondoka kwenye madeni, kuwekeza na hata kuwatengenezea watoto uhuru wa kifedha.

Lakini pia yapo maoni mengine ya wasomaji yameonesha changamoto kubwa za kifedha ambazo watu wanazo, lakini wasingepaswa kuwa nazo. Yaani kwa namna ambavyo wameweka mipango yao ya kifedha, wamejitengenezea changamoto kubwa sana ya kifedha.

Maoni haya yalikuwa ni ya wasomaji ambao wana uwekezaji mkubwa kwenye maeneo mbalimbali, yaani ukihesabu ni mamia ya mamilioni, lakini katika maisha yao ya kila siku, bado wana changamoto za kifedha. Kwa kifupi ni kwamba mtu ana uwekezaji mkubwa, lakini anapohitaji fedha kwa mambo yake mbalimbali, inakuwa tatizo.

Hapa ndipo nilipoona kosa moja kubwa ambalo watu wanafanya kwenye uwekezaji, na linawaletea changamoto za kifedha. Japo tutajifunza hili kwa kina kwenye semina hii itakayoanza mwezi wa saba (maelezo zaidi yapo mwisho wa makala hii), nimeona tuanze kulijadili hili leo ili liwe msaada kwa wengi, hata wale ambao watakosa semina (japo itakuwa jambo la ajabu kwako kuikosa).

Tuanze na uwekezaji.

Unaposikia uwekezaji akili yako inafikiria nini? Unapata picha gani?

Sitakulaumu kama unachoona ni mashamba na nyumba. Kwa sababu asilimia 99 ya watanzania hatujawahi kupata darasa lolote kuhusu uwekezaji, basi huwa tunawekeza kwa mazoea. Kwa kuangalia wengine wanawekeza wapi na sisi kukazana kuwekeza kama wao.

Hivyo watu hupambana sana kuhakikisha wanajenga nyuma, wananunua mashamba na viwanja vingi na kuwa na mali nyingine za thamani. Ukipiga mahesabu ya mali wanazomiliki ni thamani kubwa sana. Ila wanapokutana na changamoto inayowahitaji kuwa na fedha za karibu, wanakuwa hawana. Na hilo linawasumbua kwa kuona pamoja na utajiri mkubwa wa mali, fedha bado ni tatizo.

Kosa kubwa sana ambalo watu wamekuwa wanafanya kwenye uwekezaji ni kuwekeza fedha zao zote kwenye maeneo ambayo hayazalishi fedha kwa haraka. Na wanafanya hivi kwa sababu hawajawahi kupata elimu yoyote ya uwekezaji, wao wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya, kuwa na mali nyingi zaidi.

Ndiyo unaweza kuwa na mashamba, nyumba au viwanja ambavyo kwa jumla vina thamani ya mabilioni, lakini je ukihitaji milioni 100 ndani ya siku chache zijazo unaweza kuzipata? Au mali zako zina thamani ya milioni 100, lakini ukipata tatizo linalohitaji milioni moja huwezi kulipata. Unaweza kuwa na mashamba au viwanja unavyoambiwa vina thamani kubwa, lakini je kila mwezi vinakuingizia kiasi cha fedha? Hapo ndipo tatizo kubwa linapoanzia, na wengi kuteseka huku wakihesabu mali zao kwenye mahesabu ni thamani kubwa.

Iko hivi rafiki, unapofanya uwekezaji, unapaswa kuangalia urahisi wako wa kupata fedha iwapo unaitaka upo kiasi gani, hii kwa kiingereza inaitwa FINANCIAL LIQUIDITY. 

Yaani kwa mali ulizonazo, ni kwa uharaka kiasi gani unaweza kupata fedha taslimu?

Fedha taslimu ndiyo inayokuwezesha wewe kufanya yale unayohitaji kufanya, iwe ni mipango uliyonayo au dharura inayojitokeza.

Ukiwa na akiba ya muda mrefu benki ni rahisi kuigeuza kuwa fedha taslimu, japo pia unaweza kuingia gharama.

Ikiwa umewekeza kwenye soko la hisa au umenunua vipande, siyo rahisi kupata fedha taslimu haraka, lakini haikuchukui muda sana kupata.

Ukiwa umewekeza kwenye mali kama ardhi au nyumba, inakuchukua muda mrefu zaidi kuzigeuza kuwa fedha taslimu. Hata kama mali hiyo ina thamani kubwa na ukaamua kuuza kwa bei rahisi, bado inachukua muda mpaka iuzwe. Hivyo unajikuta unazo mali, lakini fedha ni shida.

Sasa mengi zaidi tutajifunza kwenye semina, ila je ufanyeje ili kuondoka kwenye hali hii? Hali ya kuwa na mali nyingi ila fedha taslimu kwako ni shida?

Zifuatazo ni hatua muhimu sana unazopaswa kuchukua;
Moja; jua aina mbalimbali za uwekezaji.

Tafadhali sana rafiki yangu, shiriki semina hii ya mwezi wa saba. Kuwekeza siyo kununua ardhi na kuwa na nyumba pekee. Zipo aina nyingi za uwekezaji ambazo unapaswa kuzijua na kuzifanyia kazi.

Na katika uwekezaji wako, lazima ugawe mtaji wako kwenye mafungu mbalimbali, kiasi fulani kiende kwenye mali, kingine hisa, kingine hatifungani na kadhalika.

Mbili; jua namna uwekezaji unaofanya unavyokuzalishia faida.

Unapaswa kujua uwekezaji unaofanya unakuzalishiaje faida. Kuna uwekezaji ambao kila baada ya muda unapokea faida, au riba au gawio. Huu ni uwekezaji kwenye biashara au hisa au hatifungani. Uwekezaji huu ni mzuri kwa sababu unaendelea kukuletea fedha huku msingi wako ukiendelea kuzalisha.

Pia kuna uwekezaji ambao faida yake inatokana na kupanda kwa thamani. Kama unamiliki ardhi au nyumba, huenda faida kubwa unaipata pale unapouza mali hizo hivyo unapokuwa na uwekezaji wa aina hii lazima usubiri.

Tatu; kuwa na akaunti maalumu ya dharura.

Kwa vyovyote vile, hakikisha unakuwa na akaunti maalumu ambayo inakaa fedha za dharura. Akaunti hii huigusi kwa namna yoyote ile, mpaka pale unapopata dharura kweli.
Sasa ni kiasi gani unaweka kwenye akaunti hii, inategemea na gharama zako za maisha. 

Kwa sababu lengo hasa la akaunti hii ni kama kipato ulichonacho sasa kitakatika, uweze kuendelea na maisha badala ya kuuza mali zako, wakati unajipanga.

Hivyo unapaswa kujua gharama zako za maisha kwa mwezi ni kiasi gani. Hapo weka kila kitu mpaka mikopo unayolipa, kila gharama unayolipa kwa mwezi, kuanzia chakula, ada, kodi mbalimbali, usafiri, mavazi na hata fedha ya burudani. Kisha zidisha kiasi hicho mara sita au mara 12.

Hii ina maana kwamba, iwapo lolote litatokea kwenye maisha yako, na kipato chako kikaathiriwa, una uwezo wa kuendelea na maisha kwa miezi 6 mpaka 12 ijayo bila ya kukosa kipato. Hichi ni kipindi kizuri ambapo unaweza kujipanga vizuri na kutengeneza kipato kingine.

Kwa kuwa na akaunti hii ya dharura italinda mali zako pale unapopata changamoto. 

Maana unapokuwa na changamoto na fedha huna, utauza mali zako za thamani kwa bei ya kutupa, kitu ambacho siyo kizuri kwako.

Nakusihi sana rafiki yangu, usikubali kukaa huna akaunti ya akiba.

Tutajifunza mengi zaidi kwenye hili katika semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ambayo itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap. Semina hii ni maalumu kwa wanachama wa kundi la KISIMA CHA MAARIFA. Hivyo kama ungependa kushiriki, na bado hujawa mwanachama wa kundi hili, unachopaswa kufanya ni kulipa ada ya mwaka ya kuwa mwanachama, ambayo ni tsh 50,000/= na kisha unaingia kwenye kundi na kuweza kushiriki semina hii.

Ada hii unayolipa ni ya mwaka mzima, tangu unapolipa mpaka mwaka uishe, yaani miezi 

12. Unapokuwa kwenye kundi hili utashiriki semina hii ya FEDHA, semina nyingine na kila siku unaendelea kujifunza.

Kufanya malipo ili kujiunga tuma fedha tsh 50,000/= kwa namba zifuatazo; mpesa 0755 953 887 tigo pesa na airtel money 0717 396 253 majina ni Amani Makirita. Ukishatuma ada, tuma ujumbe kwa njia ya wasap wenye majina yako kwenda namba 0717396253. 

Nafasi za kujiunga ni chache, hivyo chukua hatua mapema sana rafiki yangu. Karibu sana.
Ninachosema ni hichi rafiki yangu, kama upo makini na maisha yako, kama unataka kuondokana na changamoto za kifedha, hakikisha unashiriki semina hii.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA 

MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.