Biashara za karne hii ya 21 zimebadilika sana, lakini bado watu wengi wanafanya biashara zao kama vile tupo kwenye karne ya 19. Watu wanafanya biashara zao kwa mazoea na hili linawagharimu sana.
Kuna bango moja huwa nashangaa kuliona mpaka leo kwenye maeneo ya biashara, au hata kwenye risiti za baadhi ya biashara. Bango hili linakuwa na ujumbe kwamba BIDHAA IKISHAUZWA HAIRUDISHWI.
Ujumbe huo una dharau na kiburi cha hali ya juu sana kwa wateja wa biashara yako. Hivyo nakusihi, kama una bango la aina hiyo kwenye biashara yako, au umeandika ujumbe huo kwenye risiti au eneo lolote la biashara yako, ondoa ujumbe huo.
Kwa nini uuondoe?
Kwa sababu hauna maana yoyote, hauna faida yoyote kwako na biashara yako na unaharibu mahusiano yako na wateja wako.
Najua wengi wanafikiri ukiruhusu mteja kurudisha bidhaa unakaribisha uzembe kwa sababu anaweza kuharibu halafu akarudi kudai nyingine. Ni fikra nzuri, lakini siyo ukweli. Mteja wa kweli, hawezi kufanya hivyo. Na zaidi kama unauza kitu bora ambacho kinamsaidia kweli mteja, hakiwezi kuleta shida ya aina hiyo. Na iwapo kitaleta shida, hata kama ni uzembe wa mteja, bado ni mteja wako, hivyo mnapaswa kufanya kazi pamoja, ili kufanya maisha yenu wote kuwa bora.
Sijui tunaelewana?
Kwa sababu unapomwambia mteja mali ikishauzwa hairudishwi unajua ni ujumbe gani unampa?
Nunua kwa hatari yako mwenyewe….
Ukishaondoka hapa usirudi tena…..
Ukinunua hii bidhaa wewe ni mjinga….
SOMA; Usimpe Mteja Majukumu Ambayo Siyo Yake….
Ni kweli, huo ndiyo ujumbe unaokuwa unawapa wateja wako. Na zamani ulifanya kazi kwa sababu watu hawakuwa na sehemu nyingine ya kununua, fikiria duka moja la kijiji, inabidi ununue tu. Lakini zama hizi ambapo hapo ulipo kuna wafanyabiashara wengine wasiopungua watano, unachofanya ni sawa na kuwaambia wateja wako kanunue kwa wengine, ukija hapa shauri yako kwa yatakayokukuta!
Ni kweli mteja anaweza kufanya uzembe utakaopelekea bidhaa uliyomuuzia kuharibika. Lakini unajua kwa maelewano mazuri na mteja wako unaweza kumuuzia bidhaa nyingine? Au hata kumpa bidhaa nyingine na baadaye ukaendelea kufanya naye biashara nyingine?
Zipo njia nyingi bora za kutatua matatizo yako na wateja wako, lakini ya kuwaambia wakishanunua hawawezi kurudi tena, siyo njia bora.
Uza bidhaa au huduma ambayo unaiamini kwa ubora wake, hata kama hutengenezi mwenyewe, kisha tengeneza wateja bora kabisa wa biashara yako. Na hapo utaweza kuendesha biashara ya maelewano na wateja wako.
Makampuni yote makubwa yalishagundua wateja wananunua zaidi wanapokuwa na uhakika (guarantee) ya kwamba bidhaa ikiwasumbua watasaidiwa. Na sasa makampuni mengi yanaenda mbali zaidi na kuahidi kurejesha fedha iwapo mteja hataridhika na kile alichonunua. Wanafanya hivyo wakiwa tayari wana uhakika na bidhaa au huduma yao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
