Nilikuwa nasoma kitabu cha mfanyabiashara aliyeweza kufanya makubwa sana, alirithi biashara ya baba yake ya kuuza mvinyo, na akaweza kuikuza mara dufu ndani ya muda mfupi. Kwenye kitabu hicho alikuwa anasema ushauri bora kabisa wa biashara ambao baba yake alimpa ni huu; NENO LAKO LIWE SHERIA AMBAYO HUTAIVUNJA.

Anasema baba yake alimwambia, iwapo ataagiza chupa 100 za mvinyo, na kuwa ameshaweka oda tayari, lakini baadaye akagundua alikosea, alitaka chupa kumi pekee, basi hapaswi kubadilisha oda ile. Badala yake aiache oda kama alivyoiweka, na atajua hizo chupa nyingine 90 atazipeleka wapi, bora hata azinywe zote lakini siyo kubadili neno lake.

Ni ushauri mkali na mzito ambao ukiusoma unaweza kuona kwa nini kukazana na vitu vidogo kiasi hicho, lakini ni ushauri ambao una maana kubwa sana.

SOMA;  Ishi Maneno Yako…

Kitu pekee ambacho kinaweza kukujenga jina kwenye biashara na hata heshima kubwa, ni kutunza neno lako, au kwa lugha nyingine, uaminifu wako. Pale unaposema kitu na kukitimiza, watu wanakuamini. Na hata unapokuwa umekwama, watu watakuwa tayari kukusaidia. Utashangaa watu wanajitolea kukupa nafasi ambazo hukuwa hata unastahili. Watu watakuamini kwa nafasi kubwa na hilo litakuongezea wewe fursa nyingi zaidi.

Ukishaahidi kitu, fanya kila uwezalo kuhakikisha unatimiza ahadi yako. Na kama kila kitu kimeshindikana, badala ya kuja na sababu kwa nini umeshindwa, njoo na kitu mbadala ambacho kitawasaidia watu kwa namna ulivyokuwa umeahidi.

Tunza sana neno lako, ahidi makubwa na timiza makubwa. Ichukulie biashara yako kwa nafasi kubwa sana. Na hakikisha unatekeleza kila unachoahidi.

Biashara ni yako wewe, kwa nini uahidi kitu halafu usitekeleze? Hebu kuanzia sasa fanya neno lako kuwa sheria ambayo utaishi nayo, na hutoivunja kwa namna yoyote ile, ije mvua au lije jua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog