Habari za leo rafiki yangu,

Juma lililopita nilikuuliza swali muhimu kuhusu fedha, ambalo lilikuwa wazazi wako wamekufundisha nini kuhusu fedha? Nimepata mrejesho kutoka kwa baadhi ya marafiki na kwa kweli wamefunguka sana namna ambavyo tabia zao za kifedha ni zile za wazazi wao, na ambazo haziwapeleki pazuri. Tutalifanyia kazi hilo kwenye semina ya mwezi huu wa saba 2017 ambapo nitakupa maelekezo zaidi mwisho wa makala hii.Leo nimekuja na swali jingine muhimu zaidi ya lile la wiki iliyopita, na swali hili linalenga elimu ya fedha tunayotoa au kupanga kutoa kwa watoto wetu. Kama huna mpango wowote wa kuwa na watoto kwenye maisha yako, unaweza kuishia hapa, maana yanayoendelea hayatakuwa na msaada sana kwako. Ila kama una watoto, au una mpango wa kuwa na watoto baadaye, ni MUHIMU SANA USOME MAKALA HII hata kama hutashiriki semina, lakini ninajua wewe rafiki yangu, utaondoka na kitu ambacho kitakusaidia sana kwenye maisha yako, na kitasaidia vizazi vijavyo pia.

Nakumbuka siku za nyuma kidogo tulikuwa tumekaa na ndugu kwenye mazungumzo ya kawaida, tukajikuta tumeingia kwenye mazungumzo ya watoto. Nilishtushwa na kauli ya ndugu mmoja, kijana tu, aliyesema mimi nitapambana usiku na mchana kuwaandalia watoto wangu maisha mazuri wasipate tabu nilizopata mimi. Nikamwuliza maisha hayo mazuri unayopanga kuwaandalia ni yapi? Akajibu nahakikisha kila wanachotaka wanapata, na wanaanza maisha wakiwa na nyumba, gari na mali ambazo nimewatafutia. 

Nikamwuliza hivyo tu? Akasema ndiyo. Nikamwuliza sasa wao watapambana kufanya nini kwenye maisha yao? Alikoelekea ni kwamba na wao watapambana kuwaandalia watoto wao.

Kwa utafiti wangu kwa watu wengi, hakuna maandalizi ya kutosha kwa watoto linapokuja swala la fedha. Na hapa hakuna lawama kwa sababu sisi kama wazazi hatukuwa na maandalizi ya kutosha, na hatukutumia muda wetu kujiandaa kifedha, na hivyo hatuna maandalizi bora ya kuwapa.

Katika hili la maandalizi ya watoto kifedha, pamekuwa na makundi matatu ya wazazi;

Kundi la kwanza; nitahakikisha wanangu hawateseki kama mimi.

Hili ni kundi la wazazi ambao labda walipitia changamoto za kifedha kwenye maisha yao, na hivyo kuona hali hiyo siyo sawa na hawataki watoto wao waipitie. Hilo ni jambo zuri, hakuna anayependa kuona watoto wake wanateseka.

Lakini utekelezaji wa hilo ndiyo unawaharibu watoto, na kwa dunia ya sasa, inakuwa hatari mno.

Wote tumekuwa tunaona mifano mingi ya wazazi wanaokazana kutengeneza mali nyingi kwenye maisha yao, kuwapa watoto wao kila kitu, lakini wanapofariki, mali zile nazo zinapotea kabisa. Watu wengine wamekua wanahusisha hilo na imani za kishirikina, kwamba watu hao walipata mali hizo kwa masharti fulani ya kichawi na hivyo wakifa zinapotea.

Lakini wote huo ni uongo, ukweli ni kwamba wazazi wanakuwa wanakazana kuwalinda watoto wao wasiteseke. Hivyo kwanza wanahakikisha hawapati shida yoyote kwenye maisha, hawakosi chochote wanachotaka, na zaidi wanawaandalia maisha ya baadaye. 

Kwa kuwajengea nyumba za kuishi, magari ya kutumia na hata biashara za kuwazalishia.

Wanachosahau wazazi wa kundi hili ni kuwashirikisha watoto wao hatua kwa hatua kwenye mambo hayo. Wanaamini watoto hao muda wao bado na wanapokuja kustuka, watoto wameshakuwa na mtazamo ambao haufai kurekebisha.

Tatizo la fedha ni moja, kama mtu ana mtazamo wa matumizi pekee na siyo wa kuzalisha zaidi, hata apewe fedha nyingi kiasi gani hazitamtosha. Sasa watoto wa kundi hili, wanakuwa wamejengewa mtazamo wa matumizi. Na hakuna shida yoyote inayotokea wakati wote wazazi wanapokuwa hai. Kwa sababu misingi ya uzalishaji bado wanaisimamia. Ni pale wazazi wanapofariki, ndipo changamoto huanza. Misingi ya uzalishaji haipo, matumizi makubwa na kinachofuatia ni mali kuuzwa.

Kundi la pili; watoto nao lazima wateseke kama mimi mzazi wao nilivyoteseka.

Upo mtazamo wa wazazi wengine kwamba kwa sababu wao waliteseka, ndipo wakapata akili ya maisha, basi watoto wao lazima nao wateseke ili nao wapate akili ya maisha. 

Mzazi anakuwa na uwezo mzuri lakini maisha ya watoto yanakuwa ya taabu sana. Ni kweli hali kama hiyo inaweza kumjengea mtoto kujitegemea mwenyewe, lakini inamuumiza zaidi.

Kuta tofauti ya wewe mzazi kukulia kwenye shida kwa sababu uliona kabisa wazazi wako hawana namna, na mtoto wako kukulia kwenye shida huku akiona wewe mzazi ungeweza kuwasaidia, inawaumiza zaidi. Unaweza kutengeneza chuki kubwa na watoto, wakafanikiwa kweli lakini mkawa watu ambao hamuwezi kukaa sehemu moja.

Na ipo mifano mingi ya watoto ambao wamewakana kabisa wazazi wao, hasa wa kiume, kwa sababu ya mtazamo huu wa wazazi.

Kundi la tatu; ninawaandaa watoto wangu, waje kunisaidia baadaye.

Kundi la tatu la wazazi ni wale wanaoamini kwamba wanateseka kwenye maisha yao kwa sababu wanawaandalia watoto wao maisha mazuri ya baadaye. Na kwa sababu hiyo, watoto wao wana jukumu la kuja kuwatunza watakapokuwa wazee. Kwa sababu wao walitumia maisha yao kuwaandaa. Hawa nao hawajengi msingi mzuri wa kifedha kwa watoto, na kama hiyo haitoshi, wanawaongezea mzigo kwenye maisha yao.

Nimewahi kuandika hili na nilikumbushe tena hapa, hasa kwa wazazi vijana kwamba watoto siyo uwekezaji, watoto ni wajibu wetu katika kuhakikisha maisha yanaendelea hapa duniani. Hivyo hakuna mkataba wowote wa kuingia na mtoto wako kwamba unateseka maisha yako kwa ajili ya maisha yake. Kwa sababu mtoto huyo hakukupa wewe mkataba wa kumpata. Najua hili linaweza kuwashangaza wazazi watu wazima, ambao walishaweka mipango hii zamani, lakini kwa wazazi vijana, nasisitiza sana hili, jijengee misingi yako ya kifedha wewe, na mjengee mtoto misingi ya kifedha, halafu kila mtu awe na maisha bora na yenye furaha, ushirikiano uwepo mzuri na siyo mtoto, tofauti na ule wa kutishiana na kuumizana kisaikolojia. Sisemi uache kuwasaidia wazazi wako na wala sisemi uwaambie watoto wako wasikusaidie, ninachosema ni wewe rafiki yangu, ambaye unapata elimu hii, ujenge misingi mizuri ya kifedha, ambayo itaondoa utegemezi wa moja kwa moja kati yako wewe na watoto wako, siku za baadaye.

Sasa rafiki, kama unavyoona, maandalizi kwa watoto, hasa kwenye misingi ya kifedha, hayapo kabisa. Watu wanaendesha maisha kwa mazoea, na kuwaacha watoto wakiwa hawana msingi. Baadaye kinachofuata ni lawama.

Je unawezaje kuwajengea watoto msingi mzuri wa kifedha ambao utawawezesha wao kuwa na maisha yenye uhuru wa kifedha?

Hili ni swali muhimu unalopaswa kupata majibu yake, na utayapata kwenye semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, semina itakayoanza tarehe 03/07/2017. Ni semina ambayo huna sababu yoyote ile ya kuikosa, labda kama utakuwa umeamua wewe na nafsi yako kwamba umasikini ni ndugu yako ambaye huwezi kumwacha peke yake. Maelezo ya kushiriki semina hii yapo hapo chini;

KARIBU UJIFUNZE ELIMU YA MSINGI YA FEDHA MWEZI WA SABA.

Mwezi wa saba mwaka 2017, nimeandaa semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA (BASIC FINANCIAL EDUCATION). Hii ni semina ambayo nitaiendesha kwa njia ya mtandao, kupitia kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA. Unaweza kushiriki semina hii popote pale ulipo Tanzania na hata duniani. Huhitaji kusafiri au kuacha kazi zako, unachohitaji ni kutenga muda wako mfupi kila siku wa kufuatilia semina hii.

Ili kuweza kushiriki semina hii, unapaswa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Kwa kuwa mwanachama unaweza kusoma makala nyingi kwenye blog ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni ya wanachama tu, pia unakuwa kwenye kundi la wasap ambapo kila siku unapata tafakari na kila jumapili tunakuwa na madarasa ambapo tunajifunza mambo muhimu kuhusu mafanikio.

Kuwa mwanachama unapaswa kulipa ada ya mwaka ambayo ni tsh 50,000/= ambapo ada hii inakwenda kwa mwaka mmoja tangu siku unayolipa. Ada inalipwa kwa namba 0755 953 887 au 0717 396 253 majina Amani Makirita. Ukishalipa ada tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 na nitakuweka kwenye kundi.

Semina hii ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, siyo semina ya kukosa kwa mtu yeyote yule ambaye yupo makini na maisha yake. Fanya malipo leo ili uweze kujihakikishia nafasi ya kushiriki semina hii ya kipekee sana kwako.

Karibu sana tujenge msingi imara wa kifedha kwetu na kwa vizazi vyetu. Chukua hatua kwa kufanya malipo leo ili kuweza kushiriki semina hii nzuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA 

MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.