Kitu kinachoongoza kuua biashara nyingi ni fedha. Pale mzunguko wa fedha unapoanza kusua sua, biashara inaanza kuyumba na hatimaye kufa. Ndiyo maana nimekuwa nasema, mzunguko wa fedha kwenye biashara ni sawa na mzunguko wa damu kwenye mwili wa mtu. Ni vitu muhimu sana kwenye uhai wa mtu.
Lakini kuna kitu kingine muhimu ambacho biashara inapaswa kuwa nacho. Kitu hicho ni pumzi. Pumzi ni muhimu kwa binadamu, bila pumzi unakufa.
Pumzi kwenye biashara, ni uwezo wa biashara kuendelea kujiendesha hata kama haizalishi faida. Yaani iwapo biashara inaenda bila faida, au inaenda kwa hasara, je inaweza kujiendesha kwa muda mrefu kiasi gani?
Pumzi ni uwezo wa kulipia gharama za kuendesha biashara bila ya kutoa fedha kwenye biashara. Kama unaweza kulipia gharama za biashara kwa mwaka mzima, yaani kodi, pango, mishahara na matumizi mengine, biashara yako ina pumzi kubwa.
Hii ni dhana muhimu sana ya kuifikiria na kuifanyia kazi kwa sababu watu wengi wamekuwa wanaendesha biashara kwenye kona ya kuanguka. Yaani biashara, kifedha inakuwa kwenye kona mbaya ambapo chochote kidogo kikiigusa, inaanguka vibaya.
Hapo unakuta biashara inategemea kila kitu kutoka kwenye faida ya kila wakati, ikiwa ni kodi, pango, mishahara na gharama nyingine. Sasa inapofika wakati ambapo biashara haiendi vizuri, labda siyo msimu wake, biashara inaumia sana.
Unahitaji kuwa na pumzi angalau ya mwaka mmoja mbele, na hii itakuwezesha wewe kuendesha biashara ukiangalia maono makubwa zaidi kuliko kumezwa na matatizo madogo madogo ya kila siku.
SOMA; Biashara Yako Ni Kuwafurahisha Watu…
Pia pumzi hii itakuwezesha kufanyia kazi changamoto yoyote ambayo inaisumbua biashara, bila ya kuhofia biashara kushindwa kujiendesha. Kwa mfano kumetokea tatizo la wateja kupungua na hivyo mauzo kuwa kidogo, unaweza kufanyia kazi hilo wakati biashara inaendelea. Au kuna hasara inapatikana kwenye biashara, unaweza kufanyia kazi wakati biashara inaendelea.
Mwisho pumzi itakusaidia kuvuka nyakati ngumu kibiashara. Kila biashara huwa ina aina yake ya msimu, na misimu hii hujirudia kila mwaka. Kwa kuwa na pumzi ya mwaka mzima, biashara yako itaweza kwenda vizuri hata kama msimu siyo mzuri.
Ninachosema rafiki, jua gharama zako za kuendesha biashara kwa mwaka mzima, pale unapoanza mwaka wako wa kibiashara. Halafu hakikisha unazo fedha za kukuwezesha kuendesha biashara yako mwaka mzima, hata kama hutatengeneza faida. Kama gharama hizo ni kubwa na huwezi kutenga sasa, kuwa na akaunti maalumu ambayo utakuwa unatenga kiasi cha fedha kwenda huko. Ni bora kuanza na kidogo kuliko kukosa kabisa.
Unaweza kuona ni fedha nyingi umeziweka bila kazi, lakini ni muhimu mno kwako, kama una ndoto kubwa kibiashara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
