Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. 



Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo letu tutakwenda kujifunza sababu moja kubwa inayokuzuia kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye kile unachofanya.

Natumaini kila mmoja wetu kuna kitu anafanya lakini kila mtu anapata matokeo tofauti au mwingine anapambana kweli kila siku kuhakikisha anapata ushindi kwenye kile anachotafuta lakini hapati. Watu wengi hawapendi maisha ya changamoto hivyo falsafa ya watu wengi ni kupenda kupata kitu bila kuumia na kama kweli unatarajia hivyo kupata bila kuumia unakuwa unakwenda kinyume kabisa na sheria ya asili hivyo basi, kama unafikiria nadharia hiyo basi sahau kusikia kitu kinachoitwa mafanikio katika maisha yako.

Tunapenda kupata vitu au kulelewa kama vile yai bila kupata shida. Tunaishi maisha kama ya watalii tunataka mambo yaende kama vile mtalii anavyokwenda sehemu yoyote kuzuru na kutegemea kupatiwa ukarimu na kupata yote anayohitaji bila shinda. Mtalii yeye akishalipa hela yake hataki kitu kusikia shida au kero itakayomsumbua katika safari yake ndiyo maana yale magari yanayobeba watalii yanakuwa yana kila kitu hivyo kama mtalii amepanda na akasikia gari lako linapiga kelele yoyote basi hawezi kuendelea na safari na hivyo utakuwa umempoteza mteja wako.

Ndugu msomaji, hapa nilikuwa naongelea nadharia yetu sisi binadamu tunavyopenda kupata vitu bila kupata shida kama vile watalii na tunasahau kuwa mtalii hataki shinda kwa sababu amelipia gharama. Kwanini sasa watu wengi tunajikuta tunakomaa na vitu fulani lakini hatupati matokeo mazuri au mafanikio mazuri tunayotaka kwenye yale mambo tunayofanya kila siku?.

Rafiki yangu, mwaka 1968 Mtanzania na mwanariadha anayejulikana kwa jina John 
Stephen Akhwari alikwenda kushiriki mbio za maili elfu tano huko nchini Mexico hivyo kwa namna moja tunaweza kusema alikwenda kuwakilisha Tanzania. Kama tunavyojua kuwa maisha yetu hayakosi changamoto hivyo katika mashindano yake katikati ya mbio aliweza kuanguka na kuumia vibaya goti na bega lake lakini baada ya kuumia hakubali kuacha kuendelea na mbio licha ya kuumia vibaya na kila mtu alijua hawezi kuendelea akiwa na majeraha.

Watu wengi waliweza kuondoka uwanjani na kukata tamaa na kuendelea kuangalia mashindano hayo na kulibakia watu wachache sana lakini yeye hakujali bali aliendelea na mbio licha ya kuumia kwake. Waandishi wa habari walikuwa na shauku kubwa ya kutaja kusikia kutoka kwake kwa nini aliamua kuendelea na mbio? John Stephen Akhwari aliwajibu hivi ‘’ nchi yangu haikunituma kuja kuanza mbio za maili elfu tano, bali nchi yangu imenituma kuja kumaliza mbio za maili elfu tano’’ kwa hiyo mimi na wewe tunaweza kutafakari kauli hii na tutajifunza kitu.

Rafiki, kauli ile iliweza kuwastaajabisha watu wengi, licha mtu kuumia lakini alikomaa kuendelea na mapambano yaani mchezo wa riadha. Kumbe basi, changamoto kubwa au kizuizi kikubwa kinachotuzuia sisi kushindwa kupata matokeo au mafanikio tunayoyataka ni kushindwa kuendelea na mbio na kuishia njiani. Wengi tunapopata changamoto katika kazi zetu tunazofanya kila siku huwa tunaishia njiani na kushindwa kumaliza mbio kwa sababu ya changamoto.

Tumekuwa ni watu wa kuruka ruka leo tunaanza na hiki na tukiona hatupati matokeo mazuri tunayotaka au mafanikio tunaacha kuendelea na mapambano. Tunaweza kusema tunaishi maisha kama vile ya ndege au kipepeo kwa sababu kipepeo kazi yake yeye ni kuruka kutoka ua moja na kwenda lingine huwezi kumkuta kipepeo au ndege ametulia katika mti mmoja hata siku moja lazima aruke hapa na pale. Tunashindwa kupata matokeo au mafanikio kwa sababu ya kushindwa kuvumilia katika mashindano hivyo tukipata tu changamoto kidogo basi ndiyo inakuwa sababu ya sisi kutuzuia kuendelea na mapambano na hatimaye hatupati kile tunachotafuta katika maisha yetu.

Mpenzi msomaji, laiti kama kila mtu angeliongea lugha yake na kusikiliza sauti yake ya ndani yaani ile nguvu ya kusikiliza sauti ya ndani basi watu wengi wangeliweza kumaliza mbio na hatimaye kupata ushindi. Huenda mpaka kufikia leo umesharuka kama kipepeo bila kutulia na kufanya kitu kimoja na kutopata matokeo unayotaka. Tunakazana kuanzisha mambo mengi lakini hatuna hamasa ya kung’ang’ania kumaliza yale tunayoanzisha kila siku katika maisha yetu.

Hatua ya kuchukua leo, hakikisha unapoanzisha kitu komaa nacho mpaka upate mafanikio unayoyataka, usianze mbio na kushia njiani bali ushindi utaupata pale utakapomaliza mbio bila kuishia njiani. Changamoto ni sehemu yetu katika safari ya kutafuta mafanikio hivyo zisikufanye na wewe uishie njiani.

Kwa kuhitimisha, hatuwezi kupata matokeo mazuri kwa kuishia njiani au kuanzisha kitu na kuacha na kukimbilia kingine kabla ya kupata matokeo. Warusi waliwahi kusema kama ukiwakimbiza sungura wawili kwa wakati mmoja huwezi kumkamata hata mmoja.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com