Watu wengi wenye elimu kubwa wamekuwa wakishindwa kwenye biashara, huku wenye elimu za kawaida au za chini kabisa wakifanikiwa sana kwenye biashara. Hii ni kwa sababu, kufanikiwa kwenye biashara, haihitaji akili nyingi, na wakati mwingine akili nyingi zinakuwa kikwazo.

Watu wenye elimu kubwa wamekuwa wakifikiria na kuchambua sana mambo, kiasi cha kuchelewa kuchukua hatua. Inapojitokeza fursa nzuri ya wao kutumia, huchambua sana mpaka wanapokuja kuchukua hatua inakuwa imeshachukuliwa na kila mtu.

Wakati mwingine pia elimu imekuwa inamfanya mtu aone biashara ndogo siyo hadhi yake, kwa kiwango chake cha elimu hawezi kufanya kazi ndogo ndogo za kwenye biashara.

Kikubwa zaidi, ni mtazamo ambao elimu inajenga juu ya watu. Kwa mfano elimu ya ngazi ya shahada, cheo chake ni afisa. Kama mtu ana shahada ya elimu basi huyo ni afisa elimu (Education Officer), kama ana shahada ya udaktari basi huyo ni afisa tabibu (medical officer), na kadhalika. Sasa dhana hii ya uafisa, inakuwa imemwandaa mtu kwenda kusimamia wengine zaidi ya yeye kufanya. Biashara inahitaji mtu ufanye zaidi kuliko kusimamia.

SOMA; Falsafa Ni Maisha Na Siyo Cheo Wala Elimu.

Hivyo, kuepuka kurudishwa nyuma na elimu yako kwenye biashara, anza upya, anzia chini kabisa.

Unapoingia kwenye biashara, ingia kama mjinga ambaye upo tayari kujifunza kila kitu. Ingia kama mtu ambaye upo tayari kufanya kila kitu. Usiingie kwa dhana ya kusimamia, bali ingia kwenye dhana ya kufanya.

Pia usiogope sana kupoteza kwenye kila hatua unayochukua. Jua kuna wakati utapoteza, na pia kuna wakati utapata. Jaribu mambo mengi na jifunze kwenye kila jambo.

Mwisho kabisa jitengenezee tabia za mafanikio kwenye biashara, tabia za kujituma na kujitoa, uaminifu, nidhamu na uvumilivu, zitakuwezesha kuvuka changamoto mbalimbali na kufanikiwa kwenye biashara.

Unapoingia kwenye biashara, ni vyema elimu yako kubwa ukaiweka pembeni kwa muda, na kujifunza kila kitu kinachohusu biashara yako, na kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog