Fahamu Chanzo Kikuu Cha Fangasi Kwenye Majengo Na Mbinu Za Kuziepuka.

Habari za siku rafiki, karibu tena kwenye Makala hii tuendelee kushauriana mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo na uwekezaji wa ardhi na majengo. Katika safari hii ya mafanikio wapo baadhi ya marafiki wanapitia changamoto mbalimbali zinazohusiana na uwekezaji huu. Napenda nikwambie kwamba ni muhimu sana ukatafuta ufumbuzi mapema, usiseme haupo tayari au unasubiri mambo fulani yakae sawa, huu ndio wakati sahihi wa kufanya kila kitu uwezacho.Changamoto zipo nyingi lakini leo nitazungumzia chanzo cha fangasi kwenye majengo na mambo muhimu ya kuzingatia ili kuepuka na kuifanya nyumba yako kuwa mahali safi na salama. Fangasi ni hali inayosababisha majengo kuoza kutokana na kuathirika na hali ya unyevunyevu wenye kemikali mbalimbali zilizopo kwenye ardhi. Fangasi husababishwa na kuwepo kwa hali ya majimaji kwenye nyumba kwa muda mrefu kutokana na chemchem, mvua au matumizi ya maji mengi. Fangasi husababisha kuoza kwa kuta, sakafu, nondo na malighafi mbalimbali kwenye nyumba. Pia huchochea nyumba kushambuliwa na mchwa kutokana na kuwa imeozeshwa na unyevu uliopo. Zifuatazo ni sababu kuu za majengo kupata fangasi na mbinu muhimu za kuziepuka.

  1. KUTOZINGATIA VIGEZO VYA USANIFU MAJENGO


Katika safari yangu ya kitaaluma nimefundishwa kuwa ujenzi unaweza kufanyika mahali popote kwenye ardhi maadamu umezingatia vigezo vyote kukidhi hali ya mazingira ya eneo la ujenzi. Ujenzi holela unaoendelea kufanyika unasababisha hasara na hali ya wasiwasi kubwa katika ubora na usalama wa wakazi. Wengi wetu tumejenga maeneo yenye ardhi ambayo muda wote wa majira huwa imetota maji ambayo huwa yana mchanganyiko wa kemikali mbalimbali za kimazingira. Nasikitika kusema wengi hawakufuata taratibu za kisanifu hali inayosababisha kuoza kwa majengo na hatimaye kuchakaa haraka. Usanifu wa majengo huratibu mfumo na muundo wa nyumba ili iweze kupambana na mazingira husika, ikiwemo hali ya majimaji isisababishe madhara yoyote kwenye nyumba. Muundo wa msingi wa nyumba na mpangilio wa maeneo yanayotumia maji kwa wingi kama vile bafu, vyoo, jiko na mifumo yote ya maji ni mambo yanayozingatiwa sana na wasanifu majengo ili kupambana na tatizo hili. Ni vema ukamuona mtaalamu wa ujenzi kwa ushauri kabla ya ujenzi ili akupe mbinu mbalimbali kutokana na mazingira halisi ya eneo lako.

  1. KUTUMIA MALIGHAFI ZISIZO NA UBORA

Ni muhimu sana kuzingatia ubora wa malighafi zote utakazotumia kwenye ujenzi wa nyumba yako ili idumu kwa muda mrefu pasipo kufanya marekebisho yasiyo na ulazima. 

Karatasi ngumu za plastiki, Matofali, nondo, milango, madirisha na malighafi zote zinapaswa kuhojiwa ubora wake kabla hujatumia. Pia tumia mabomba ya maji safi na maji taka yenye ubora kuepusha kuvujisha kwenye kuta na sakafu endapo yatapasuka na kusababisha hali ya unyevunyevu kwenye kuta jambo ambalo huathiri hata mifumo ya umeme. Malighafi dhaifu haziwezi kuhimili changamoto za mazingira yenye unyevunyevu kwa muda mrefu, ni hasara na kadhia kwa wakazi. Hata kama haupo kwenye maeneo ya majimaji utaratibu wa ubora upo palepale, mvua za upepo zinaweza kulowanisha ukuta kwa nje lakini zikakuletea madhara hadi ndani hasa kubanduka kwa rangi. Epuka propaganda za masoko huria za vifaa vya ujenzi ukashindwa kuhoji ubora na matumizi sahihi kwa chochote unachonunua kwa sababu unatoa pesa na sio mawe.

  1. KUTOZINGATIA UTAALAMU WAKATI WA UJENZI


Mara nyingi huwa nawakumbusha marafiki kuwa ni lazima ujiridhishe na ubora wa fundi wako kabla hujampa jukumu la ujenzi kwenye nyumba yako kuepuka kuwa uwanja wa kufanyia mazoezi. Hakikisha unatandika karatasi ngumu ya plastiki kwenye msingi wa nyumba, msingi usiwe chini sana kutoka usawa wa ardhi, hakikisha gata zinafungwa vizuri kuepuka kuvujishia maji kwenye kuta, tumia saruji na epuka rangi, niru na gypsum kwenye maeneo yenye matumizi ya maji, zingatia matumizi sahihi ya rangi kwenye kuta na sakafu, epuka mzunguko mkubwa wa mabomba ya maji safi na maji taka, jitahidi nyumba iwe upande wenye mwinuko na mashimo ya maji taka au visima yawekwe pembeni upande wa chini. Kama umejenga paa lenye zege hakikisha unafanya usafi mara kwa mara na kutoruhusu kuhifadhi maji hata kama umeweka malighafi zisizopitisha maji. 

Ujenzi unahitaji umakini na usimamizi wa hali ya juu sana kuhakikisha ubora unazingatiwa kwenye kila hatua. Ubora wa fundi ni muhimu sana ili kuepuka matatizo yanayotokana na ufundi hafifu, nyumba sio nguo endapo itakosewa utarudisha kwa fundi akubanie zaidi. Chochote kwenye nyumba ni pesa, weka fundi mzuri ili uepuke gharama za matengenezo kwa wakati ujao.

Ni rahisi kupambana na mazingira yenye majimaji kwenye ardhi wakati wa ujenzi kuliko kuzuia baada ya ujenzi kwa sababu ni gharama na inahitaji marekebisho kila baada ya miaka michache kutokana na aina ya malighafi zilizotumika.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888


Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: