Hongera rafiki yangu kwa siku hii bora sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora.


Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUJIJENGA KAMA MTU….
Mafanikio hayatokani na kile tu unachofanya, bali pia yanaanza na wewe ni nani.
Hivyo moja ya mambo yanayochochea au kuzuia mafanikio yako ni namna wewe ulivyo kama mtu.
Tabia zako, mitazamo yako, maamuzi yako, ndoto zako, hayo yote yana mchango mkubwa kwenye mafanikio yako.

Lakini kwa kwenda tu namna unavyotaka mwenyewe, au namna wengi wanavyoenda, huwezi kujijenga na kuwa mtu bora.
Kwa sababu ni tabia ya binadamu kufuata njia rahisi,
Ni tabia ya binadamu kuendelea kuishi kama wanavyotaka wao, lakini wapate katokeo bora.
Kitu ambacho huwa hakitokei.

Hivyo rafiki, unahitaji kuweka kazi ili kujijenga wewe kama mtu bora.
Kama ambavyo tunahitaji kuweka kazi ili kuandaa shamba bora la kupanda mazao. Kwa sababu shamba likiachwa lilivyo, linaota magugu.
Maisha yako pia ndivyo yalivyo, yakiachwa yaende kama yanavyojiendea, huwezi kifanikiwa.

Unahitaji kazi kwenye kujenga tabia bora kabisa za mafanikio,
Unahitaji kazi kwenye kutengeneza mitizamo sahihi ya mafanikio.
Unahitaji kazi kwenye kutengeneza mahusiano bora kwa mafanikio yako.
Unahitaji kazi kwenye kuijenga afya bora ya mafanikio yako.

Kazi zote hizo ni nje kabisa ya kuweka kazi kwenye kile unachofanyia kazi kila siku.
Hivyo ni muhimu kukumbuka kazi hizi muhimu za pembeni, maana wengi wamekuwa wanazisahau, wanakazana kufanya kazi zao, lakini hawajioni wakipiga hatua.

Unahitaji kuweka kazi ili kuwa mtu bora, na kuweza kufanikiwa.

Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info