Ndiyo kuna wateja wasumbufu, wateja ambao wanayafanya maisha yako kibiashara kuwa magumu mno. Wateja wanaotaka kunufaika wao bila ya kujali biashara yako. Wateja wanaotaka kupata zaidi kwa kutoa kidogo. Wateja wanaokopa na hawalipi. Wateja ambao wakishakopa wanahama kabisa.

Lakini nisichotaka wewe ufanye ni kukaa na kuanza kuwalalamikia wateja wa aina hii. Kuanza kujiambia isingekuwa wateja hao basi ungekuwa mbali kibiashara. Kwa kuruhusu wateja wawe kikwazo kwako kufanikiwa kibiashara.

Nakuambia usifanye hivyo kwa sababu sioni sababu yoyote kwa nini ufanye.

Kwa mfano, kuna mteja alishawahi kukulazimisha umuuzie? Hakuna. Wewe mwenyewe ulimkaribisha mteja, na kumfundisha au kumvumilia tabia ambayo alianza kuonesha tangu awali. Na sasa inaumiza biashara yako.

SOMA; Mteja Hatakuonea Huruma…

Sasa kulalamika haitasaidia lolote, unachopaswa kufanya ni kuchukua hatua. Na hatua ya kwanza kabisa ni kusitisha huduma kwa mteja ambaye anakuumiza kichwa kwenye biashara.

Na hatua ya pili, ni kuchagua wateja wako vizuri. Chagua wateja ambao wanauhitaji kweli wa kile unachouza, wanathamini na kujali unachofanya, na hapo weka juhudi zako zote kuhakikisha wateja wako hao wanapata huduma bora kabisa.

Ukijikuta ulichagua vibaya, basi chukua hatua kwa yule ambaye anaendelea kuwa  kikwazo kwenye biashara yako.

Lazima ukubali kwamba siyo kila mtu anaweza kuwa mteja wa biashara yako, hata kama ana uhitaji kabisa wa kile unachotoa. Biashara ni mahusiano, kama mtu hawezi kuwa na mahusiano mazuri, hawezi kuwa mteja mzuri.

Unapofanya haya, hakikisha matatizo hujayaanzisha wewe, kati yako na mteja wako. Maana kama wewe ndiyo chanzo cha matatizo, utafukuza wateja wote na kubaki wewe na biashara yako, kinachofuata kifo cha biashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog