Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaoingia Kwenye Biashara Na Wale Wenye Ndoto Za Kuja Kufanya Biashara.

Habari za leo rafiki?

Hii ni barua ya wazi kwa vijana wote wa kitanzania ambao wanaingia kwenye biashara au wana ndoto za kuja kufanya biashara siku za mbeleni. Nimekaa chini kukuandikia barua hii wewe rafiki yangu, baada ya kuona vijana wengi wakianguka na kushindwa kwenye biashara kwa jambo moja ambalo wangeweza kulifanyia kazi.Nimebahatika kuwa nawashauri watu wengi wanaopanga kuingia kwenye biashara. Pia nimepata nafasi za kuwashauri wengi ambao wanapata changamoto za kibiashara, zinazowapelekea kupata hasara na hata biashara kufa kabisa.

Kitu kimoja kikubwa ambacho nakiona kwa vijana wengi, ni kutokuipa biashara muda ambao inastahili kupewa. Hili ni kosa kubwa, ambalo linaua biashara nyingi mno.

Mara zote ninapoandika kuhusu biashara, huwa naifananisha biashara na kitu kimoja, mwanadamu. Kwa kila hali, biashara inafanana kabisa na ulivyo mwili wa mwanadamu. 

Nimekuwa nasema damu ya biashara ni fedha, hivyo mzunguko wa fedha ndiyo uhai wa biashara kama ilivyo mzunguko wa damu kwa mwanadamu.

Sasa kwa mfano huu wa kuifananisha biashara na mwanadamu, biashara mpya inakuwa kama mtoto mchanga. Sasa kama umewahi kulea mtoto mchanga unajua nini namaanisha hapa. Mtoto mchanga anahitaji muda mwingi mno kuliko mtu mwingine yeyote. Mtoto mchanga anaweza kulia usiku kucha na hivyo ukawa na kazi ya kumbembeleza. Mtoto mchanga anataka kulishwa, kusafishwa, kila kitu ni tegemezi kwa mzazi au mlezi.

Hivi ndivyo ilivyo biashara yoyote mpya, inahitaji muda mwingi zaidi kuliko biashara nyingine yoyote ile. Biashara mpya inahitaji muda mwingi wa mwanzilishi wa biashara hiyo. Inahitaji mtu awe makini usiku na mchana, ili kuweza kuhakikisha biashara hiyo inasimama.

Biashara mpya inakuwa inakula tu na haizalishi, hasa mwanzoni. Inakuwa inahitaji mtu aweke kazi ya ziada, ambapo itamchukua muda zaidi. Unapoanzisha biashara usiku na mchana hauna tofauti kubwa, kwa sababu mchana utahudumia wateja, usiku utaboresha biashara.

Biashara mpya inakuhitaji usahau mambo ya kijamii kwa muda, usahau mapumziko kwa muda, na ukazane zaidi ya kawaida. Biashara mpya inakuhitaji uwe na uwezo wa kifedha wa kuiendesha, hata kama haiingizi faida siku za mwanzoni. Inahitaji wewe uwe na kiasi cha fedha ambacho kitaiwezesha biashara kujiendesha, kugharamia mahitaji yote ya kibiashara.

Kama ambavyo mtoto mchanga anahitaji uangalifu asife, ndivyo biashara inavyohitaji usimamizi na uangalizi wa karibu mwanzoni ili isife.

Matatizo ya vijana, na wengine ambao wanaingia kwenye biashara, ambayo yanapeleka biashara kusua sua na hata kufa ni haya;

1. Kutoweka muda wa kutosha kwenye biashara.

Huwa nashangazwa sana na mtu anaanzisha biashara, lakini hataki maisha yake ya kijamii yabadilike. Yaani mtu anaanzisha biashara mpya, lakini bado anataka kila siku aendelee kuangalia tv, aendelee kuangalia michezo mbalimbali, kila jioni awe na marafiki wakipiga soga. Anataka aamke asubuhi na kwenda kwenye biashara na jioni arudi mapema kusubiri tena siku inayofuata.

Kwa vijana ndiyo kabisa nashangazwa na mtazamo ambao wengi wanaanza nao biashara. 

Mtu anatenga kabisa muda wa kutoka au kutofanya biashara yake ili aweze kuangalia michezo, hasa wa mpira wa miguu wa timu anazofuatilia. Yaani kijana anaanza biashara, na wakati huo anataka aangalie michezo yote ya ligi ya uingereza, ujerumani, hispania na ligi nyingine kubwa. Hapo bado awe hai kwenye mitandao ya kijamii, makundi ya wasap, bado afuatilie siasa zinazoendelea, na biashara istawi.

Hakuna kujidanganya zaidi ya huku. Kwa kifupi ni kwamba mkakati wa aina hiyo haufanyi kazi kwenye biashara mpya, kamwe.

2. Kutokuweka kazi na usimamizi wa kutosha kwenye biashara.

Vijana wengi hufikiri kitu pekee unahitaji ili kuingia kwenye biashara ni mtaji. Hivyo hukazana sana kutafuta mtaji, wanaupata, wanafungua biashara, na kwa kuwa wana mambo mengine, wanaajiri watu wa kusimamia biashara hizo. Kinachotokea ni kila siku kuna changamoto mpya kwenye biashara. Wanaweza kubadili wasimamizi kadiri wawezavyo, wanaweza hata kuwaweka ndugu wakifikiri tatizo ni kukosa uaminifu. 

Lakini kinachotokea ni kukosana na watu na mpaka ndugu.

Kila biashara mpya ina changamoto, tena nyingi. Usipokuwa karibu na biashara yako hutawaelewa wanaokuambia kuhusu changamoto, na hutaweza kufanya maamuzi sahihi. 

Wale unaowaweka kusimamia, hawana uchungu kama wewe, hivyo wanaweza kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri.

Hata uwe umebana kiasi gani, hakikisha unapata muda wa kuifuatilia biashara yako kwa karibu sana. Hakikisha unaisimamia moja kwa moja, hakikisha unaielewa nje ndani. 

Usijidanganye kwa kuajiri umemaliza kila kitu, unachokuwa umefanya ni kutafuta mtu wa kumlipa ili abebe lawama zako.

3. Kuinyonya biashara.

Mtu anaanzisha biashara leo, halafu kesho, au mwezi ujao anataka aanze kutoa fedha kwenye biashara na kutumia. Anajiambia kabisa biashara ni yangu na fedha ni zangu, kwa hiyo natumia na nitakuja kurudisha. Hakuna sumu inayoua biashara kama hiyo.

Tukirudi kwenye mfano wetu wa mtoto mchanga, ni sawa na kumnyima mtoto maziwa na kuanza kumkamua kabisa, kuanza kutaka na yeye atoe maziwa ili mtu ayafaidi. Kitu ambacho hakiwezekani.

Usitegemee biashara siku za mwanzoni, iache biashara ijiendeshe yenyewe na muhimu zaidi uweze kuisaidia biashara pale inapokwama. Lakini kama utaanzisha biashara ambayo unataka ndani ya siku chache uanze kuitegemea, ni bora tu utumie hizo fedha unazopanga kuanzia biashara, na upunguze kujisumbua.

Nafikiri unaona namna makosa ya kawaida yanavyokuwa na madhara makubwa kwenye biashara changa. Muhimu ni kuilea biashara changa kwa umakini kama wazazi na walezi wanavyolea watoto wachanga kwa umakini.

Mambo muhimu kuhusu biashara changa unayopaswa kuyafahamu;

1. Tafiti za kibiashara kwenye nchi zinazoendelea, zinaonesha asilimia 80 ya biashara zote zinazoanzishwa hufa ndani ya miaka mitano tangu zinapoanzishwa. Hivyo miaka 5 ya kwanza ya biashara yako ni kipindi cha hatari.

2. Biashara mpya inapaswa kuwa na uhakika wa kujiendesha angalau kwa mwaka mmoja hata kama itakuwa haitengenezi faida. Hivyo jua gharama za biashara yako na jiandae mapema kabla hujafikia wakati ambao huna tena fedha za kuendesha biashara.

3. Ukienda kuomba mkopo benki kupitia biashara, kigezo ni angalau biashara hiyo iwe na miezi 6. Miezi sita ya mwanzo ya biashara, ni wakati muhimu mno, hapo kosa lolote dogo litaua kabisa biashara.

Nimalize barua hii kwa kuwahamasisha vijana kuingia kwenye biashara wakiwa wamejiandaa. Unapoingia kwenye biashara, usiingie kujaribu, bali ingia kufanya hivyo jitoe kufanya kweli. Ni ngumu na zina changamoto, lakini uzuri ni kwamba zinawezekana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA 

MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: