Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora.


Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu WATU KUKUZOEA SANA….
Ni tabia ya watu kupenda kuzoea kitu au mtu yeyote,
Halafu wakishazoea wanachukulia poa,
Yaani watu wakishazoea mtu au kitu, huwa hawakipi tena ile heshima ya mwanzo.
Hivyo ni muhimu sana kuepuka watu kukuzoea kupita kiasi, hata kama ni watu gani.

Na njia ya kuepuka watu kukuzoea ni kutoruhusu watu kujua kila kitu kuhusu wewe.
Wengi wanapenda kuweka kila kitu wazi kuhusu maisha yao, na hilo huwafanya watu kuzoea, kuchukulia kawaida na hata kuweza kutabiri au kutegemea hatua gani mtu atachukua kwenye jambo gani.
Hivyo mtu anaweza kukufanyia jambo la hovyo, kwa sababu anajua ni hatua gani utachukua, ambayo labda haitamuumiza au itamnufaisha kabisa.

Lakini watu wanapokosa kukuelewa kwa kila kitu, watu wanapokosa kila taarifa kuhusu wewe, wanakuwa na wasiwasi ndani yao. Hawajui wategemee nini kutoka kwako na hawawezi kutabiri lolote kuhusu wewe. Kwa namna hii watu watachukua hatua kwa umakini na kuheshimika kutakuwepo.

Kamwe usiruhusu mtu aseme wazi kwamba huyu tumeshamzoea, atafanya hivi au vile tu. Waweke watu kwenye giza kiasi kuhusu wewe, na watajipanga wanapotaka kufanya jambo lolote linalokuhusu wewe.

Mazoea huzaa dharau, usiruhusu hilo. Watu wakishazoea kitu, hata kukithamini kitu hicho huwa kunashuka, wanakichukulia poa, kwa kuwa wanajua kipo na watakipata muda wowote. Usiruhusu hilo kwako binafsi kwa mtu yeyote yule kukuzoea kupita kiasi.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info