Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwends kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutakwenda kuweka juhudi kubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NJIA YA MKATO KUKULETEA MIKATO….
Tunaishi kwenye zama ambazo watu wanatumia muda mwingi kutafuta njia ya mkato ya kupata chochote wanachotaka.
Watu hawataki kuweka kazi wala kusubiri, wanachotaka wanakitaka sasa, na kutumia muda mwingi kutafuta njia ya mkato na rahisi ya kupata.
Mtu anataka mafanikio lakini anataka ayapate akiwa anaendelea na maisha aliyonayo, asibadili chochote.
Mtu ameshindwa kusimamia afya yake, mwili umezidi uzito na anatafuta kidonge kimoja cha kunywa ili apunguze uzito.
Mtu ameshindwa kusimamia fedha zake na anatafuta fursa moja ambayo itamwondoa kabisa kwenye umasikini, kwa haraka na bila ya kuweka kazi.
Kwa kifupi rafiki, hivyo vitu havipo.
Njia yoyote ya mkato, kama ipo, itakiacha na MIKATO.
Kwa sababu njia hizi huwa zinafanya kazi kwa muda mfupi tu.
Baada ya muda unarudi pale pale, tena ukiwa na hali mbaya zaidi kuliko ya mwanzo.
Kama ni umasikini ndiyo unakuwa maradufu, kwa sababu njia ya mkato uliyotumia inakuwa imekuingiza kwenye madeni zaidi.
Kama ni afya ndiyo inakuwa hovyo zaidi.
Hivyo rafiki, popote mtu anapokuambua hii njia ya mkato, itumie, usihangaike naye, ondoka haraka sana. Mtu huyo siyo mwema kwako. Huenda kuna kitu anataka kukuuzia, au anataka kukutapeli.
Misingi ya maisha na mafanikio bado ni ile ile,
LAZIMA UWEKE KAZI,
LAZIMA UWE MVUMILIVU,
LAZIMA UWE NA SUBIRA…
Waachie wengine wasioelewa kazi hiyo ya kutafuta mkato, usipoteze muda kwenye hayo, pambana kuweka kazi ambayo itakuletea matokeo bora,
KIBIASHARA,
KIKAZI,
KIFEDHA,
KIAFYA,
KIMAHUSIANO…
Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA
#KochaMakirita