Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambao unatuwezesha kufanya makubwa kwenye maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kukimbizana na fursa…
Wapo watu ambao kila siku kuna fursa mpya wanaikimbiza,
Wakati wanakimbiza fursa fulani, wanakutana na fursa nyingine ambayo ni nzuri kuliko ile ya mwanzo, wanaachana na ya mwanzo na kukimbiza fursa hiyo mpya.
Haiwachukui muda mwingi kwenye fursa mpya, utawakuta na fursa nyingine tena…
Hii ni changamoto kubwa na ni kikwazo cha kufikia mafanikio makubwa.
Kwa sababu mafanikio hayatokani na ni fursa zipi umeziwahi, bali yanatokana na uwezo wa mtu wa kuchagua kitu fulani na kukifanyia kazi kweli.
Mafanikio kwenye chochote ambacho mtu anafanya, yanahitaji muda mrefu, kazi kubwa na uvumilivu.
Hakuna mafanikio makubwa na ya kudumu yanayokuja haraka na hila ya kazi.
Hivyo rafiki, tuliza akili yako, chagua fursa ipi unafanyia kazi, na weka kazi. Ukishachagua fursa hiyo, achana na nyingine kwa kipindi ambacho unajenga fursa yako hiyo.
Weka masikio yako pamba na macho yako yawe pale kwenye kile unachofanya.
Utaambiwa mengi sana kuhusu fursa mpya, lakini achana nayo na fanyia kazi fursa uliyoichagua kwanza.
Kukimbizana na kila aina ya fursa kuna tafsiri tatu;
1. Hujui ni nini unataka kwenye maisha yako, hivyo unajaribu jaribu kila kitu ukiangalia labda wapi patakufaa.
2. Ni mvivu ambaye hupendi kuweka kazi wala kukutana na changamoto, hivyo unapoanza kufanyia kazi fursa na ukakutana na changamoto, badala ya kutatua unaangalia fursa nyingine.
3. Unatafuta njia ya mkato ya mafanikio, ambayo haipo.
Cha kufanya;
Chagua fursa utakayoifanyia kazi, inayoendana na ndoto kubwa na maono ya maisha yako, kisha weka kazi, muda na uvumilivu. Mengine achana nayo kwanza, yatakupotezea tu muda wako.
Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.
http://www.makirita.info