Kuna watu huwa wanaingia kwenye biashara kwa kusudi la kutengeneza faida, kupata fedha za kuendesha maisha yao, ni kitu kizuri, maisha lazima yaende na fedha ni muhimu. Lakini umuhimu wake unaenda mpaka pale mtu anapoondoka kwenye hofu ya kukosa fedha, na hapo ndipo mtu anaona kuna kitu anakosa kwenye maisha yake.

Faida ni nishati ya kuchochea kusudi. Unapokuwa na kusudi kubwa zaidi kupitia biashara yako, faida inakuwezesha wewe kuendelea kufanyia kazi kusudi lile. Hivyo utaweza kuweka juhudi kubwa, lakini ukiwa unafanyia kazi kitu kikubwa kuliko faida pekee.

Kwa njia hii, hata unapofikia uhuru wa kifedha, hupati hali ya kukosekana kwa kitu, kwa sababu utakuwa unaendelea kufanyia kazi kusudi lako ambalo unalifanyia kazi kupitia biashara au chochote unachofanya.

Hili ni muhimu sana kufahamu kabla hata hujaingia kwenye biashara, au kama umeingia bila ya kulijua, ni muhimu kukaa chini na kutafakari kwa kina kusudi lako ni nini.

SOMA; Njia Mbili Za Kuongeza Faida Na Moja Ya Kuepuka Sana….

Jiulize kusudi la maisha yako ni nini, na unalitimizaje kupitia biashara unayofanya. Pia jua kwa nini unafanya biashara hiyo, kama fedha zikiwekwa pembeni. Na siyo lazima kila mara ufanye biashara inayoendana na kusudi lako au unayoipenda, kuna wakati utahitaji kufanya aina tofauti za biashara ili kupata fedha au mtaji zaidi wa kufanya ile biashara ya kusudi la maisha yako.

Hivyo, usiache biashara yako sasa kwa sababu siyo kusudi la maisha yako, au huoni ikiwa sehemu ya maisha yako, badala yake endelea kufanyia kazi kusudi hilo, na usisahau.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog