Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. 



Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo letu tutakwenda kujifunza changamoto kubwa inayoharibu furaha ya mafanikio.

Rafiki, licha ya watu wengi kupambana kutafuta na kuwa na maisha mazuri lakini kuna changamoto kubwa bado inawasumbua. Changamoto ambayo inawafanya watu wengi kushindwa kufurahia maisha ya mafanikio hapa duniani. Hakuna mtu ambaye hapendi furaha katika maisha yake ndiyo maana tunaweka juhudi mbalimbali kupata kitu fulani ili tuwe na furaha.

Changamoto kubwa inayoharibu furaha ya mafanikio siyo nyingine bali ni changamoto za kiafya. Hatuwezi kufurahia maisha kama tuna changamoto za kiafya. Watu wengi wanaweka juhudi kubwa katika kutafuta mali lakini wanasahau eneo moja muhimu ambalo ni eneo la afya. Kama vile unavyojali vitu vingine vivyo hivyo katika afya unatakiwa kujali pia.

Afya ndiyo utajiri namba moja duniani. Watu wanapokuwa na afya hawaoni umuhimu wake mpaka pale wanapoikosa. Kama unafanya uwekezaji katika maisha yako basi uwekezaji wa afya ndiyo uwe namba moja. Wengi hawajali miili yao kabisa wengine wamegeuza miili yao kuwa kama choo yaani kila aina ya uchafu ni ruhusa kuingia. Cha kushangaza zaidi wale vijana ambao ndiyo wanategemewa ndiyo wamekuwa mstari wa kwanza kuharibu miili yao. Kama eneo muhimu ambalo unapaswa kuwa na ubinafsi nalo basi ni eneo la afya yako kiujumla.

Kama vile ulivyokuwa mgumu kwenye pesa vivyo hivyo kuwa mgumu kwenye afya. 

Hapa nina maanisha kuwa bahili sana wa kupenda afya yako kuliko kitu kingine chochote kile. Kama hujali afya yako na una maliza muda mwingi hospitali utaweza je kufurahia maisha yako ya kimafanikio hapa duniani. Maisha ni furaha lakini hakuna furaha ya maisha kama hakuna afya njema ya mwili. Miili yetu ndiyo hekalu muhimu ambalo kila mmoja wetu ndipo mahali anapoishi.

Mwili wako ndiyo nyumba yako, ndiyo mahali ambapo unaishi siku zote. Kama ukisafiri lazima utaondoka na mwili wako huwezi kusema hata siku moja naomba ukae na mwili wangu mimi ninasafiri. Popote pale unapoenda unaenda na mwili wako kwani ndiye rafiki wa kweli unayetembea naye popote pale unapoenda. Unaweza ukaenda sehemu mbalimbali na watu lakini hata siku moja huwezi kuingia kila sehemu na watu bali utaingia wewe na mwili wako.

Mpenzi msomaji, sisi kama binadamu tuliopewa akili tunaalikwa kuzitumia akili zetu vizuri ili tuweze kuijenga dunia. Hatuwezi kuifanya dunia kuwa bora kama afya zetu ni mbovu. Hatuwezi kuleta maendeleo katika taifa letu kama ruti za hospitali haziishi, kama kila siku tunakuwa tunahangaikia magonjwa yanayoandaa miili yetu tutawezaje kufanya kazi?

Kila mmoja wetu anatakiwa kujali sana afya yake. Kama unatakiwa kula vizuri kula vizuri kama unatakiwa kufanya mazoezi fanya mazoezi vizuri. Kubali vyote vikupite lakini usikubali kupitwa na afya yako maana kama afya yako siyo nzuri huwezi kwenda kokote kule. Kubali kulipia gharama mapema ili usije kulipia kwa riba kubwa. Sasa ndiyo muda muhimu kwako wa kuweza kubadilisha afya yako usisubiri mpaka ulazwe ndiyo ujue unaumwa bali chunguza afya yako mara kwa mara kadiri uwezavyo.

Ndugu, tusipowajibika kutuza afya zetu basi afya nayo anatuadhibu kwa kutupa magonjwa kupitia miili yetu. Ukiwa mzembe katika eneo la afya huwezi kukwepa adhabu ya magonjwa na kuna watu wengine wamekuwa wakijihisi tu wako tofauti wanakimbilia kumeza dawa za kutuliza maumivu. Mwili unakuwa umeshazoea dawa mpaka inafikia hali ya ukroniki tena. Kila mtu ana matatizo yake, hakuna mtu ambaye yuko salama kwenye kila idara ya maisha yake lakini usikubali kutengwa na afya yako.

Hatua ya kuchukua leo, kama unapenda kufurahia maisha basi kubali kuzingatia kanuni za afya lakini pia jali afya yako. Kuwa mbinafsi na afya yako kuliko kitu kingine chochote na fanya mwili wako uwe hekalu na siyo choo kila mtu anatupa takataka anazojua yeye. 

Hakuna maisha bora bila kuwa na afya bora.

Mwisho, kila mmoja wetu awe balozi namba moja wa afya yake, cheza na yote lakini usicheze na afya yako. Jali mwili wako vizuri kwa kuupatia vyakula bora vinavyojenga mwili na kuupa kinga dhidi ya magonjwa. Kubali kulipia gharama juu ya afya yako kwani maisha ni afya na bila afya bora hakuna maisha bora.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi. Asante sana.