Kila biashara ina changamoto zake, hii ina maana kwamba kama umekuwa kwenye biashara fulani kwa kipindi kirefu, na umeshajifunza na kuzoea biashara, haimaanishi unaweza kufanya kila aina ya biashara. Utakuwa na unafuu ukilinganisha na ambaye hajawahi kufanya biashara kabisa, lakini bado unahitaji kujifunza kwenye kila biashara mpya unayoingia.

Watu wengi wamekuwa wakiingia kwenye biashara mpya, kwa kutumia uzoefu wa biashara zao za zamani na wamekuwa wanakutana na changamoto kubwa sana kwao. Kibaya zaidi, changamoto hizo zimekuwa zinahamia kwenye biashara zao za zamani, na hivyo kujikuta biashara zote zinakufa.

Unapaswa kuwa makini pale unapoanzisha biashara nyingine, tofauti na unayofanya sasa. Hata pale unapofungua biashara hiyo hiyo kwenye eneo tofauti, unahitaji kuwa makini pia.

Yafuatayo ni mambo muhimu kuzingatia;

SOMA; Maana ya neno HAPANA kwenye biashara…

  1. Hakikisha biashara yako ya mwanzo imeshasimama vizuri na inaweza kujiendesha yenyewe kwa faida. Umeshatengeneza mifumo mizuri, una wasimamizi wazuri na unaweza kuifuatilia kwa urahisi, hata kama haupo kwenye biashara muda wote.
  2. Biashara mpya unayoanzisha, ijitegemee yenyewe, kuwa kama ndiyo unaanza biashara upya. Usiruhusu kila changamoto ndogo unayopata kwenye biashara mpya basi uondoe fedha kwenye biashara ya zamani. Badala yake ifanye biashara mpya kujitegemea yenyewe, ikiwa na bajeti yake yenyewe.
  3. Unapaswa kuwepo kwenye biashara mpya, kipindi cha mwanzoni. Hata kama umepeleka mfumo wako mzuri na wasaidizi unaowaamini, bado unahitaji kuwepo wewe binafsi. Kwa sababu kama tunavyojua, kila biashara mpya ina changamoto zake, hivyo uwepo wako utakuwezesha kuziona kwa ukaribu na kuweza kuzitatua.
  4. Jifunze kama ndiyo unaanza biashara, usipeleke ujuaji na kuona tayari wewe ni mzoefu. Kila biashara ina kipindi chake cha kujifunza, kuna vitu vya ndani ambavyo huwezi kuvielewa mpaka uingie na kufanya. Jifunze kuelewa vitu hivyo kupitia kwa watu wengine wanaofanya.

Fanyia kazi hayo kuhakikisha biashara mpya unayoanzisha inaweza kupiga hatua na kufanikiwa kama ilivyo kwenye biashara yako nyingine iliyofanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog