Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda.


Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda jinsi ya kutawala uwepo wako na kuacha alama hapa duniani.

Uwepo wako mahali unawaathiri watu kwa namna gani? watu wanajisikiaje siku wakikukosa eneo ulilopo, watu wanakutegemea kwa kitu gani? uwepo wako una madhara kwa jamii uliyopo? Kuna watu wapo kama vile hawapo yaani wapo sehemu lakini hakuna mtu anayeona tofauti kama upo au hapo yaani unakuwa huna madhara yoyote chanya kwa jamii.

Nafasi yako kama mzazi unaitendea haki vizuri? Nafasi yako mahali ulipo unaitendea haki ipasavyo? Ni kweli watu wengi siku hizi wamekuwa ni wajane katika mioyo ya watu yaani kama ni kufa wameshakufa siku nyingi katika mioyo ya watu licha ya kuwa wazima. Inawezekana wewe ni kiongozi lakini umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya watu unaowaongoza. Inawezekana wewe ni mzazi lakini umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya watoto kwa sababu hawaoni athari yako katika maisha yao.

Inatakiwa kuishi maisha ambayo usipokuwepo watu wanajua haupo kabisa. Yaani una mchango fulani katika maisha yao. Kama upo sehemu au haupo na watu hawaoni mchango wako basi ujue hauna thamani. Kwa sababu mtu yeyote mwenye thamani lazima ataacha pengo tu wakati hayupo.

Tunaalikwa kujichunguza katika maisha yetu binafsi je maisha tunayoishi yana athari gani kwa wenzetu? Tusipokuwepo tunaliliwa au watu wanaona kawaida tu? Jichunguze kama umekufa tayari katika mioyo ya watu au la.

Kama unacheza mpira hakikisha unatawala namba yako ua nafasi yako kuonesha uwepo wako. Kama wewe ni mwalimu hakikisha unatawala masomo yako kuhakikisha uwepo wako upo pale. Kama wewe ni kiongozi hakikisha unatawala nafasi yako kuonesha uwepo wako wa uongozi. Tunaalikwa kutawala nafasi zetu tulizonazo vilivyo vizuri.

Kuonesha uwepo wako ni kutawala vizuri kile unachofanya. Kama una watoto hakikisha unatawala kuonyesha uwepo wako kama mzazi. Kama unaishi na mwenza wako basi hakikisha unatawala nafasi yako kuonesha uhai wa mahusiano yenu. Usikubali mtu acheze namba yako yaani hakikisha namba yako unaicheza vizuri hata usipokuwepo watu wajue kweli leo fulani hayupo. Kazi zako unavyofanya kwa ubora ndiyo jinsi unavyoonesha kutawala .

Rafiki, popote pale unapoenda onesha uwepo wako kwa kuacha alama. Mtu akikujaribu kukuuliza kitu basi acha alama kwa kumjibu majibu mazuri mpaka ashangae mwenyewe. 

Mtu akikupa kazi yake umfanyie hakikisha unaitawala kazi yako na kuacha alama katika maisha yake. Siku mtu anaangalia kazi uliyomfanyia lazima afurahi na moyo wake kwa kusema hakika fulani amenifanyia kazi kwa ubora.

Hatua ya kuchukua leo, usikubali kutoitendea haki nafasi yako hapa duniani. Kama unaishi hapa duniani basi fanya kitu ili mtu ajue kweli fulani yuko duniani. Na siku unakosekana watu wajue kweli nafasi yako haiwezi kujazwa na mtu. Kama ni namba yako ya mpira icheze kwa ubora wa hali juu na usikubali watu wakuchukulie wa kawaida kwani kawaida ni kama umeshakufa katika mioyo ya watu.

Kuwa sehemu bila kuonesha umuhimu wako ni sawa na chumvi isiyokuwa na thamani. 

Hivyo jitahidi kufanya vizuri kazi zako. Onesha thamani uliyonayo katika maisha ya watu kwa kufanya hivyo utakuwa umetawala jina lako na uwepo wako pia hapa duniani.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi. Asante sana.